Thursday, January 16

VIONGOZI wa Dini Kisiwani Pemba kuunda kamati itakayosimamia na kufuatilia utoaji wa elimu ya Mirathi kwa jamii.

 

NA ABDI SULEIMAN.

VIONGOZI wa Dini Kisiwani Pemba, wanakusudia kuunda kamati itakayosimamia na kufuatilia utoaji wa elimu ya Mirathi kwa jamii, ili kuepusha migogoro ya mali zinazoachwa na marehemu.

Viongozi hao wamesema migogoro mingi hutokea kwa jamii, baada ya mmoja ya wanafamilia kuondoka duniani na kuacha baadhi ya mali, na kushindwa kurithisha hali inayopelekea kutokea kwa migogoro na wengine kunyimwa haki zao za mirathi.

Viongozi hao waliyaeleza hayo katika mkutano wa siku moja, juu ya uhamasishaji wa mirathi katika jamii, ulioandaliwa na Jumuiya ya KUKHAWA Pemba kupitia mradi wa haki ya umiliki wa ardhi Pemba na kufanyika mjini Chake Chake.

Walisema ucheleweshaji ugawaji wa mirathi unachangia kwa familia kutokuelewana kwani umiliki wake zaidi ni wanaume na kukosa uwadilifu katika matumizi yake na kusahau wanawake kuwapa haki zao.

Mohamed Khatib Ishak kutoka Machomanne, alisema upo umuhimu wa kuhakiki mali kabla ya kugaiwa baada ya mtu kufariki dunia, ili kuweza kujulikana kwa mali hiyo pamoja na uhalali wake.

“kufanyika kwa jambo hilo kila mtu atakuwa anapata haki zake, imezoeleka mwanamke kunyimwa haki yake ya mirathi kwa visingizio vingi,”alisema.

Naye Suleiman Ali Salu kutoka Mkoani, alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwahamasisha wanajamii anapotokea mtu kufa, mali za marehemu zinapaswa zirithishe ili kila mwenye haki kupataka haki yake.

Kwa upande wake shekhe Yussuf Abdalla Ramadhani kutoka Chake chake, aliwataka viongozi wenzake wa dini kutoa elimu kwa njia yoyote kuwa suala la mirathi ni muhimu baada ya mmoja ya wanafamilia kufariki dunia.

“Ipo siku jamii itafahamu na itaelewa umuhimu wa mirathi, sisi viongozi wa dini tutumie nafasi zetu hata ikawa kutengeneza hutuba na mambo mengine ili jamii iweze kufahamu umuhimu wake”alisema.

Naye Shekhe Mohamed Rashid Said alisema ipo haja ya kuanzishwa kwa somo la mirathi katika madras za Qurani, ili kufundishwa watoto tokewa wakiwa wadogo.

Mwenyekiti wa bodi ya KUKHWA Ali Mohamed Ali, aliwataka viongozi hao wa dini kuwa mabaolizi wazuri katika kushajihisha jamii juu ya suala zima la mirathi ifanywe kwa mujibu wa sheria na dini.

Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya KUKHAWA Talib Ali Rajaba, alisema familia nyingi zinatawaliwa na tamaa za dunia, wakati dini imeshaeleza kila kitu juu ya suala la mirathi.

Mratib wa mradi huo Zulekha Maulid Kheir, alisema mradi huo ulianza 2019,2020 na 2021 huku viongozi wa dini wanahamasa kubwa katika jamii, pia wanaufahamu zaid juu ya mambo mbali mbali juu ya mirathi.

Alisema mwaka 2019 waliweza kuwafikia watu 4022, wanawake 1968 wanaume 2054, mwaka 2020 waliwafikia wananchi 1224 wanawake 537 na wanaume 687, mwaka 2021 waliwafikia wananchi 1705 wanawake 825 wanaume 880.