Thursday, January 16

Wazanzibar watakiwa kuutunza utamaduni wao ili kuwavutia watalii zaidi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI wa Unguja na Pemba wametakiwa kutunza utamaduni wao, ili wanapokuja wageni kuwe na vitu vya kuwaonesha ambavyo vitawavutia zaidi.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea vituo vya utalii kwa waandishi wa habari na timu za watembeza watalii Zanzibar, iliyofanyika kisiwani Pemba Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Leila Mohamed Mussa alisema, ipo haja ya kuendeleza utamaduni wao ili wageni wavutike na mambo yaliyopo.
Alisema kuwa, utalii wa Zanzibar unabebwa na utamaduni uliopo, hivyo iwapo utabadilika na kuwa kama wa kwao, itakuwa hakuna kitu cha kuwaonesha, hivyo wananchi wahakikishe vitu vilivyopo wanavipa vipaombele ili kusaidia kukuza utalii visiwani hapa.
“Tusibadilike tukawa kama wao itakuwa hatuna vitu vya kuwaonesha, wageni wetu wanapenda tunavyovaa, tunavyokula, tunavyoongea, ngoma zetu, michezo mbali mbali ikiwemo mchezo wa bao, hivyo tuvipe vipao mbele vitu hivi”, alisema Waziri Leila.
Aidha aliwataka wakulima kuzalisha vitu ambavyo vitauzika katika mahoteli ikiwemo bidhaa za viungo na hiyo ndio dhana ya utalii kwa wote kwamba kila mmoja anufaike kwa nafasi yake.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo Waziri Leila alisema, ni kutumia watu ambao wana ushawishi mkubwa kwa jamii watembelee, kuona na kupata taarifa zake ili na wao wawashawishi wananchi mbali mbali wa ndani na nje kutembelea vivutio hivyo.
“Tunaamini kwamba waandishi wa habari na timu ya watembeza watalii Zanzibar zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahamasisha wageni kuja kutalii katika visiwa vyetu, kwani hapa tunaondoka na dhamira ya kuhakikisha wanatangaza kupitia kurasa (page) zao za mitandao ya kijamii”, alisema.
Alifahamisha kuwa, Pemba ina vivutio vingi na adimu, hivyo ikiwa vitatangazwa itafunguka kiutalii na lengo la Serikali la kutala kuiinua Pemba kiutalii litafanikiwa na wananchi watafaidiaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya watembezaji na waongozaji wa misafara ya Utalii Zanzibar (ZATO) Khalfan Ali Hussein alisema, Disemba 17 mwaka jana walifanya mkutano na kutoa mapendekezo ya kufanya utalii wa ndani, ili kuhakikisha wanaibua changamoto za kiutalii katika maeneo ya vivutio, jinsi ya kuvitangaza na kuwashawishi raia wa ndani na nje kutembelea maeneo hayo.
“Tunaamini kwamba ziara hii itazaa matunda kwani tuna vyombo vya habari vingi hapa na sisi wana ZATO, tutakaa pamoja kuyajadili na kufanyia kazi, hivyo wananchi tudumishe amani, upendo na masikilizano kwani ndio chachu ya kuleta uchumi na maendeleo katika nchi”, alisema Mwenyekiti huyo.
Nae Mratibu wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba Khamis Ali Juma alisema kuwa, timu za watembeza watalii ndio wanatembeza na kupanga watalii, hivyo kupitia ziara hiyo wanatumai itaisaidia Pemba kufunguka kiutalii.
“Wengi wao walikuwa hawaijui Pemba na vitu vilivyomo na ndio maana tunapata wageni wachache mno, lakini naamini sasa watakuja kwa wingi, nawaomba wananchi tushirikiane pamoja kuupokea utalii kisiwani hapa kwani ni uchumi na unaleta neema na naahidi utaendana na utaratibu wa maisha yetu, mila na silka zetu kwa hiyo tusiuogope”, alifahamisha.
Washiriki wa ziara hiyo walisema kuwa wamefarajika sana kuona vivutio vya utalii kisiwani Pemba, wamevutika sana na mazingira mazuri yaliyopo na wamejifunza vitu mbali mbali, ambapo wameahidi kuvitangaza vivutio hivyo.
Ziara hiyo ya siku mbili ya kutembelea vivutio vya utalii iliwashirikisha waandishi wa habari, timu ya watembeza watalii Zanzibar pamoja na wadau mbali mbali mbali wa Utalii.