Monday, November 25

Ahukumiwa miaka 9 kwenda chuo cha mafunzo na kulipa fidia kwa kosa la kutorosha na kubaka.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MAHAKAMA ya Mkoa Wete imemuhukumu kijana Ali Juma Said mkaazi wa shehia ya Utaani kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka tisa (9) pamoja na kulipa fidia ya shilingi milioni moja baada ya kupatikana na kosa la kutorosha na kubaka msichana wa miaka 14.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa mahakama ya Mkoa A Wete Abdalla Yahya Shamhun baada ya kuona ushahidi uliotolewa mbele ya mahakama hiyo haukuwa na shaka yeyote.

Hakimu huyo alisema kuwa, baada ya kupatikana kwa ushahidi, mshitakiwa alionekana ni mkosa na kumtaka kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka tisa kwa makosa mawili na kumlipa fidia muathiriwa ya shilingi milioni moja.

“Mshitakiwa utakwenda kutumikia chuo cha mafunzo miaka miwili kwa kosa la kutorosha na miaka saba kwa kosa la kubaka na adhabu hizo zitakwenda sambamba”, alisema hakimu huyo.

Mapema wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Juma Mussa Omar aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake yeye na wengine wenye tabia kama hiyo.

Mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Disemba 30 mwaka 2020, bila ya halali alimtorosha mtoto huyo na kumpeleka nyumbani kwake Utaani na kumbaka, jambo ambalo ni kosa kiseria.

Kubaka ni kosa kinyume na kifungu cha 108(1), (3), (d), na 109 (1) sheria ya adhabu, sheria nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.