Monday, November 25

Rais Hussein Mwinyi ameendelea kuvutia wawekezaji kuwekeza Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya “International Holding Company “ (IHC) ya Abu Dhabi ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw.Syed Basar Shueb, kuzungumzia masuala ya Uwekezaji Zanzibar, mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Kampuni hiyo Abu Dhabi leo 18-1-2022, na (kushoto kwa Rais) Balozi wa Tanzania (UAE) Mhe. Balozi Mohammed Abdalla Mtonga na (kulia kwa Rais) Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA Bw, Shariff Ali Shariff.(Picha na Ikulu)

Akiendelea na ziara yake katika  Falme za Kiarabu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi  leo katika muendelezo wa kuvutia wawekezaji alikutana na uongozi wa kampuni kubwa katika Falme za Kiarabu na ya pili kwa  nchi za magharibi ya international holding company (IHC) yenye makao yake Abudhabi kwa ajili ya  kuzindua mpango wa maendeleo ambapo Abu Dhabi imejitolea kuleta Zanzibar wawekezaji wa kigeni.

Dk Mwinyi katika mazungumzo hayo aliwaeleza kwa undani wawekezaji hao wa (IHC) fursa zilizomo katika uchumi wa buluu na kuwaalika wawekeze visiwani Zanzibar.

Alisema Zanzibar kwa sasa inahitaji wawekezaji makini wenye jicho makini la uwekezaji.

Moja ya fursa zilizomo katika uchumi wa buluu ni uwekezaji katika visiwa vidogovidogo vinavyofikia 53 katika bahari ya Zanzibar.

Fursa nyingine zinazoambatana na uwekezaji wa uchumi wa buluu alizozieleza Rais zinazohitaji uwekezaji makini ni pamoja na uchimbaji wa gesi na mafuta uvuvi mkubwa katika bahari kuu ujenzi na kuzifanyia matengenezo meli za uvuvi ujenzi wa bandari kubwa zitazoweza kuhimili meli kubwa za mizigo.

Halikadhalika Rais Dk Hussein Ali Mwinyi amefahamisha yote hayo yatafanikiwa kukiwepo miundo mbinu  mizuri

Katika huduma za kijamii Dk Hussein Ali Mwinyi aliwafahamisha wawekezaji hao umuhimu wa kusaidia huduma za kijamii za elimu na afya na kuanzisha zoni maalum ya kiuchumi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Shariff Ali Shariff akitoa muelekeo wa fursa za uwekezaji kwa waekezaji hao aligusia hali ilivyokuwa ya watalii visiwani humo ambapo licha ya ugonjwa wa uviko Zanzibar iliendelea kupokea watalii 39,512 kati ya mwezi Januari hadi Desemba.

Aliwafahamisha kuwepo kwa fursa za kuwekeza katika kuchakata bidhaa za baharini ujenzi wa boti za uvuvi na kuzifanyia matengenezo pia ujenzi wa mji mwengine utakaoitwa Zanzibar Marina City na kusaidia kilimo cha mwani aliwataka wawekezaji hao pia kusaidia Zanzibar kuwa na kituo cha kukuza vipaji kwa michezo mbalimbali hali itakayoipaisha Zanzibar katika sekta ya michezo.

Shariff alibainisha kuwepo kwa hekta 6000 za ardhi inayohitaji kuendelezwa eneo la Makurunge ardhi ambayo ni mali ya Zanzibar na  inafaa zaidi kwa kilimo.

Baadae Rais Dk Hussein Ali Mwinyi alikutana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia mambo ya Nje Mheshimiwa Sheikh Shajkboot Nahyan al Nahyan ambapo walizungumza mahusiano baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia ufunguzi wa Ubalozi mdogo wa (UAE) Zanzibar pamoja na kurejesha huduma za ndege za (UAE) kuja Zanzibar

Ziara ya Dk Hussein Ali Mwinyi itamalizika kesho Jumatano na anatazamiwa kuondoka Abu Dhabi jioni kurejea Zanzibar.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.