NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
ZANZIBAR ni muunganiko wa visiwa viwili Unguja na Pemba.
Kwa miaka mingi sasa visiwa hivi vimekua vikisifiwa katika suala uwepo wa amani ya kutosha visiwani humo.
Viongozi mbali mbali wa serikali, NGOs, mashirika na wadau wamaendeleo wamekua mstari wa mbele kuhimiza suala la amani na utulivu, kabla ya Uchaguzi, wakati na hata baada ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi.
Tumekua tukizowea kuona uvunjifu wa amani hujitokeza zaidi kabla au baada ya kipindi cha uchaguzi mkuu wa vyama vingi, nakusahau muda mwengine na badala yake kutokea vurugu zinazoelekea kwenye mapigano.
Vipo viashiria vingi au sababu na maarufu vinavyopelekea uvunjifu wa amani kama vile kupindwa kwa demekrasia, kucheleweshwa kwa haki, ukosefu wa huduma za kijamii na ubaguzi.
Wengine husahau na wakati mwengine kupuuzia sababu za uwepo wa ajira za watoto kuwa zinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.
WAZAZI
Ali Mtwana Haji (57) ni mkaazi wa shehia ya Tumbe Magharibi, anasema ajira za watoto sio chanzo cha uvunjifu wa amani, kama baadhi ya watu wanavyofikira.
Anasema ijapokuwa serikali inakataza ajira, bado hakujatokea mapigano au mivutano katika maeneo watoto wanapofanyia ajira hizo.
“Mimi bado sijaona mikwaruzo yoyote bandarini kwetu, licha ya vijana baadhi ya siku kufukuzwa na kuwekewa vikwazo,”amesema.
Anasema tatizo ni kubwa bandarini kwao, nashangazwa na mikakati inayopangwa bandarini juu ya kuzuiliwa watoto kutokupara samaki, ilhali pesa wanazopata wanasaidia famili zao.
Mwaka Hamadi Mbwana mzazi (45) anasema ajira sio chanzo kwani kama inavyofiriwa, bali watoto wanachokipata hutumia na familia zao.
“Hatokua mwanangu akirudi anakuja na samaki na vijisenti kidogo, halafu ukamfukuza unataka akatafute pesa wapi, nakazi gani wakati hii ndio kazi nyepesi kwake,”anahoji.
Mjaka Hija Shaali (42) anasema kutokana na hali za maisha suala la ajira kwa watoto wao ni msingi mkuu wa kuendeleza familia zao.
“Naelewa kuwa ajira kwa watoto ni marufuku kuanzia kwa sheha hadi serikali kuu, na hua tunawakataza lakini hakujawahi kutokezea mivutano baina yetu na watendaji wa serikali,”anasema.
Anasema mwaka 2015 watoto walipofukuzwa, baadhi ya wazazi walipinga sana tukio hilo, huku akishutumiana na kuwekeana usahasama baina yao.
Mtumwa Rashid Kai (38) anasema ajira za utotoni chanzo cha uvunjifu wa amani, pale watoto wanapofukuzwa bandarini na wazazi kutokukubali na kuanza kujibizana.
“Tayari baadhi ya watu waliwawekeana uhasama na kusulushishwa, ili mradi watoto wao kuachiwa kuendelea na kazi zao za uparaji wa samaki,”alisema.
Ramadhan Hamad Juma (55)anasema ajira sio chanzo, bali ni mtu kama anataka kufanya matukio maovu anafanya bila ya kuwepo bandarini, kutokana na muda mrefu vijana wanapara samaki na hatujasikia mizozo yoyote.
WATOTO
Yussuf Hija Shaame (14)mkaazi wa Tumbe kaliwa, anasema ajira za utotoni sio chanzo cha uvunjifu wa amani, na wapo muda mrefu bila ya kuhusishwa na matukio maovu bandarini hapo.
Amesema sisi wengi tuliopohapa kila mmoja anajuwa anachokifanya, licha ya baadhi ya wakati madalali hutufukuza ili tuwende skuli.
“Nisipokuja hapo basi nyumbani natetwa, ati watu watakula nini wadogo zangu, imekua ni kazi yangu ya kawaida kwa sasa ila muda wa skuli ukifika nishaondoka,”alisema.
Yassir Shaame Pandu (17) mkaazi wa chimba, tuliwahi kufukuzwa ila baadhi ya wazazi walituombea tukaendelea kuwepo mpaka sasa, hapa sisi wengine tunajiepusha kuingia katika vikundi viovu huko mitaani.
“Kipindi tulipofukuzwa baadhi ya watu walitaka kupigana, kutokana na kutuzuia sisi kisingizio hatuendi skuli wala chuoni, kazi yetu kupara samaki tu”anasema.
Naye Chumu Ramadhan Heri (16) muuza Visheti bandarini Tumbe, anasema kutokana na hali ngumu ya familia yao, hanabudi kufanya biashara hiyo na fedha anazozipata zinasaidia nyumbani kwao.
“Hutokea baadhi ya siku watoto wanafurushwa hapa, zaidi muda wa skuli unapofika na wale wakaidi hukatazwa moja kwa moja kuwepo hapa,”amesema.
Pandu Jafar Ismail (18) anasema ajira sio chanzo cha uvunjifu wa amani, ni mtoto mwenyewe kama ni mkorofi basi atatimiza malengo yake popote pale na sio lazima bandarini hapa.
“Sisi tupo hapa muda mrefu wapo wanaokuja na wakiondoka fedha zao zinaishia kwenye madawa ya kulevya na mambo mengine,”alisema.
WANUNUZI WA SAMAKI
Ramadhani Haji Omar, anasema ukosefu wa elimu ndio chanzo cha wazazi kuwaruhusu watoto kujiingiza katika ajira, licha ya wengine kwenda kwa malengo binasfi, na wapo wanaokwenda kwa kusaidia familia zao kutokana na hali ngumu ya maisha.
“Wapo wanaokwenda kutafuta pesa na kwenda kutafuta dawa za kulevya, akeshalewa chochote atakachokifanya ni sawa kwake, ulevi ni baba wa maasi na hapo amani itaanza kuondoka kwa wenzake,”amesema.
Anasema bandari imekua ni kubwa, inawezekana watoto walianza wawili kipindi hiko, sasa inafika darasa zima lakini hatujawahi kuona uvunjifu wa amani bandarini hapa.
Mariyam Suleiman Mustafa mchuuzi samaki katika soko la Machomanne, anasema uvunjifu wa amani unatokea pale watoto wanapoondosha uwamifu katika utengenezaji wa samaki.
“Ingekuwa wazazi wanauelewa juu ya umuhimju wa elimu kwa watoto wao licha ya hali ngumu ya kimaisha iliyopo, basi sizani kama wange waruhusu watoto wao kujiingiza katika biashara yoyote katika umri mdogo kwa kisngizio tu maisha,” alisema.
WAVUVI WA SAMAKI
Juma Khamis Kambi anasema watoto wamekuwa ni wengi na hata wakikatazwa, wazazi wao wanakuwa wakali kutokana na baadhi yao kutumwa kwa ajili ya kusaidia familia zao.
“Ngalawa au madau yanapofika tu, basi utawaona wanakuja na biashara zao wengine huleta madafu au mafenesi, ili tuwapatie samaki na sisi tunafanya hivyo, wengine wanawauza baadae na wengine wanapeleka kwao,”amesema.
Katika hatua nyengine Kombo sheha Hassan amesema watoto waliopo wanakosa fursa zao za kielimu, kutokana na tamaa za wazazi wao kwa kitu kidogo wanachopata nao kuona ndio kazi kwa mtoto wake.
“bandarini hapa watoto wanaojishuhulisha na ajira ni wengi mmo na uvunjifu wa amani unaweza kuja pale unapowakataza watoto kupara samaki, kuosha madau, kubeba ndoo za madagaa au shazi la samaki,”anafafanua.
MADALALI WA SAMAKI BANDARINI
Abdi Khamis Juma anasema hakuna anayefurahishwa na hali iliyopo katika bandari ya Tumbe, ila ukosefu wa mashirikiano baina ya wazazi na madalali ndio sababu inayopelekea wimbi hilo.
“Baadhi ya Madalali wenzetu na Wazazi hawapo tayari katika hili, sisi wengine tunapoweka mikakati basi wengine wanaivunja na kutuona sisi wabaya,”amesema.
Anasema wapo wazazi wanawatuma watoto wao ndio wakawa wakali katika hili na kuwa tayari kupigana ili wasifukuzwe, hebu tizama mpaka jioni mtoto anafika shilingi 8,000 hadi shilingi 20,000 hutegemea na msimu.
Naye mkuu wa madalali bandarini hapo Mtawa Khamis Haji, anasema watoto waliopo bandarini hakuna hata mmoja anayekwenda skuli, huku wazazi wao wakishindwa kuwafuatilia.
MASHEHA WA SHEHIA ZA TUMBE
Kaimu sheha wa shehia ya Tumbe Mashariki Ali Omar Ali, anasema ajira hizo zinakuwa chanzo cha uvunjifu wa amani, kutokana na ukosefu wa elimu pamoja na umasikini kwa familia.
“Mtu akikosa elimu anaweza kufanya lolote hata kama linaweza kuvunja amani na anacho kitizama yeye ni maslahi yake binafsi, ndio mfano kama hawa wazazi wahaowaruhusu watoto wao kupara samaki,”anasema.
Sheha wa shehia ya Tumbe Magharibi Massoud Khamis Kirando, anasema baadhi ya watoto wanaokwenda bandarini inakuwa ni maagizo kutoka kwa baadhi ya wazazi wao kama sehemu ya kusaidia familia yao.
“Tunapowafukuza sisi huonekana ni maduwi wakubwa kwa wazazi wa Tumbe na vijiji vya jirani, yote ni kutokana na ukosefu wa elimu, ”amesema.
WADAU WA MAENDELEO
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Tumbe(JUMATU) Nassor Suleiman Nassor, anasema ajira zinakuwa chanzo cha uvunjifu wa amani pale usimamizi wa sheria zinapokuwa zinalegalega.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya kupunguza Umaskini na kuboresha hali za wananchi (KUKHAWA) Hafidhi Abdi Saidi, anasema unapomzuwia mtoto asiende kwenye ajira hizo katika umri mdogo,familia haitambuwi wamezuiliwa kwa sababu gani.
“Ukosefu wa elimu kwa watoto, unapelekea kuingia katika vikundi viovu ikiwemo wizi, udhalilishaji na uuzaji ama utumiaji madawa ya kulevya mwishokupelekea familia kugombana,”amesema.
VIONGOZI WA SERIKALI
Diwani wa Wadi ya Tumbe Ali Juma Shaibu, anasema umasikini wa familia ndio chanzo kikuu cha watoto kujiingiza katika ajira za utotoni na wanapokatazwa wazazi wanakua wakali.
“Hakuna siku ambayo watoto wanakua hawapo, siku zote wapo na wala hawaendi skuli, wakikatazwa wazazi wanakuwa wakali na kupelekea uhasama na kuchukiana.
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, anasema mtoto anapojiajiri akiwa mdogo anakosa haki zake za msingi ikiwemo elimu.
Amesema kuwa ajira za utotoni zinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani, kutokana na wazazi wanakuwa wabishani na viongozi wao serikali wanapokatazwa kutokuwaruhusu watoto wao katika ajira.
“Kutokana na wazazi kuwa wabishi juu ya suala la ajira za utotoni ndio maana watoto zaidi ya 7609 wamekatisha masomo na kundi kubwa wapo katika ajira za utotoni,”alisema.
MIKATABA WA AFRICA NA WAUMOJA WA MATAIFA INASEMAJE
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1989 ibara ya 32 , inasema watoto wanahaki ya wanahaki ya kulindwa kutoka na kazi zenye hatairi au mbaya kwao, kupata elimu, afya na maendeleo
wakati mkataba wa Africa wa mtoto wa mwaka 1979 ibara ya 15 kifungu kidogo cha kwanza (1) imepiga marufuku kazi za kiuchiumi, ambazo itapelekea madhara kimwili, akili, afya hata kukosa kimaendeloe.
SHERIA YA MTOTO NO:6/2011
Kwamujibu wa sheria hiyo, kifungu cha 99 hadi 100 vimekataza mtoto kuajiriwa kinyume na sheria kumuajiri au kumtumia mtoto katika kazi zenye madhara.
NINI KIFANYIKE
Abdi Khamis Juma anesema ifike wakati wa wazazi kuacha tabia ya kuwafanya watoto kuwa ndio chanzo cha kuhudumia familia, badala yake kuwahimiza katika suala zima la elimu kwani ndio chanzo cha maisha yao ya badae.
“Vizuri tukawa wakali hapa bndarini petu kuhakikisha watoto hawashirikishi ipasavyo katika shuhuli za uparaji wa samaki, kila mtu kwa wakati wake anapaswa kukea na kulaani kuwatumikisha watoto katika suala zima la uparaji wa samaki,”amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, amesema vijana hawapaswi kushirikishwa kwani kufanya hivyo ni kumkosesha haki yake ya kupata elimu, ikiwa ni haki ya msingi na sio chanzo cha uvunjifu wa amani kama inavyofikiriwa.
hata hivyo ameitaka jamii na wadau wengine kuwa mabalozi wazuri katika suala la kukea na kuwatumikisha watoto, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mikataba mbali mbali ukiwemo mkataba wa Haki za Binaadamu na Mkataba wa Matoto wa Africa.
MWISHO