NA ABDI SULEIMAN.
MWENYEKITI wa bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)Balozi Mstaafu wa Tanzania na Meja Jenerali Mstaafu Issa Suleiman Nassor, amesema wafanyakazi wa Mamlaka hiyo Pemba, wanapaswa kuthamini kazi yao na kutoa huduma nzuri kwa wananchi wanaowahudumia.
Alisema kazi ya kutoa huduma ya maji kwa wanachi, bila ya kunungunika na masimango wala malalamiko ni sawa na ibada tosha kwao, hivyo wanapaswa kubadilika kufanyakazi kwa umakini na kuweka mbekle maslahi ya watu.
Mwenyekiti huyo wa bodi ya Wakurugenzi ZAWA, aliyaeleza hayo katika kikao cha kujitambulisha kwakwe kwa wafanyakazi wa ZAWA Pemba, kilichofanyika Machomanne Mjini Chake Chake.
Alisema kila mfanyakazi anapaswa kuthamini na kuijali kazi yake, kwa kutambua umuhimu wake ikizingatiwa kazi yake ni ya kuhudumia jamii katika suala zima la maji safi na salama.
Aidha alifahamisha kuwa kumekua na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya huduma ya maji wanayopatiwa, kwani tokea Mapinduzi ya mwaka 1964 hadi leo wanatoa huduma ya maji kwa asilimia 55% wakati wanatakiwa kufikia 91%.
“Tunatakiwa kupambana kwa nguvu zetu zote kutoka 55% hadi tufike 91% ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama kwa umakini sana,”alisema.
Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, alisistiza suala la nidhamu kwa kila mfanyakazi kujua wajibu wake katika kazi, sambamba na kukemea suala la wizi wa vifaa na kusema kuwa kwa sasa wizi wa vifaa vya zawa hawatokuwa na nafasi tena.
Hata hivyo mwenyekiti huyo, alisema kwamba bodi hiyo ni mpya ila ni tafauti na bodi nyengine zilizopita, kwani hataki kuona wanawake na watoto wanaendelea kupata shida ya maji kwa kutembea masafa marefu.
Naye Mkurugenzi Mkuu ZAWA Zanzibar Mhandisi Dkt.Salha Mohamed Kassim, aliwataka wakusanyaji wa mapato ya ZAWA kuachana na visingizo visivyokuwa na sababu, kama sehemu imekosa vifaa wanapaswa kuwasilisha taarifa kwa mkurugenzi wao.
Alisema tayari kuna mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato hayo unakuja, hivyo baada ya kukamilika kwake utawasilishwa katika maeneo yote ili kuona mapato hayo yanakusanywa ipasavyo.
“Kwa sasa tumekua na mazowea ya zamani katika ukusanyaji wetu, ndani ya miaka miwili kila mtu anataona mabadiliko makubwa katika mamlaka yetu itakua ni tafauti na miaka iliyopita,”alisema.
Aidha aliwataka wafanyakazi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa mashirikiano makubwa, ili kuona huduma wanazotoa zinawafikia wananchi ipaswavyo.
Naye mkurugenzi wa ZAWA Ofisi ya Pemba Omar Mshindo Bakari, alisema Pemba inawafanyakazi zaidi ya 200 na wamegawika katika wilaya nne, kila wilaya inajitosheleza katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wao wafanyakazi wa ZAWA Pemba, wamesema muda mrefu wamekosa fedha za likizo kwa wafanyakazi, pamoja na ustaafu kwao ikizingatiwa tayari kuna wengine wameacha mayatima, ilhali upande wa unguja fedha hizo wanapatiwa.
Aidha wakizungumzia ukosefu wa baadhi ya vifaa kama vile katika sehemu ya ukusanyaji wa mapato ikizingatiwa wanatakiwa wakusanye ndio watumie huku vifaa vimeharibika zaidi ya miezi miwi sasa kwa upande wa Mkoani.