Monday, November 25

Wakandarasi walipwe kwa wakati ili miradi ikamilike kwa muda uliopangwa – Wito

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja  Rashid Hadid Rashid wakati wa  ziara yake   ya kuangalia Maendeleo ya Ujenzi  wa Hospital za Wilaya  Mkoani humo.

 

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akiangalia maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kitogani katika ziara yake ilionzia mkoa wa Kusini Unguja na kumalizia Mkoa wa Mjini Magharibi.

 

(PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR)

NA SABIHA KHAMIS      MAELEZO    

 

Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui ameiomba Wizara ya Fedha kuwalipa fedha kwa wakati  wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa Hospital za Wilaya ili miradi  hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa.

 

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa Hospital za Wilaya katika mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Mjini Magharib amesema ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi kunapelekea ujenzi wa hospital hizo kuzorota.

 

Amesema wakandarasi wanafanya jitihada katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati lakini fedha zimekuwa kikwazo kikubwa katika kutekeleza majukumu yao.

 

“Kila mmoja awajibike kwa nafasi yake, tukisema ZAWA walete maji, maji yaletwe na tukisema ZECO tunataka umeme, walete umeme ili tuweze kukamisha mradi huu katika kipindi cha miezi sita” alisema Waziri.

 

Nao baadhi ya wakandarasi wa hospital hizo wameeleza kuwa huduma ya maji na umeme ni miongoni mwa changamoto zinazdhorotesha maendeleo ya ujenzi wa hospitali hizo.

 

Wakandarasi hao wameahidi kukamilisha ujenzi huo kwa kipindi cha miezi sita kama ilivyopangwa pindipo  changamoto  hizo zitatatuliwa.

 

Ujenzi wa hospital hizo kumi za Wilaya unafadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi kupitia  fedha za mkopo  uviko 19 kutoka  IMF.

 

Wakati huo huo Waziri wa Afya alipokea msaada wa boksi 11 za vitakasa mikono kutoka Jumuiya ya Wazanzibar wanaoishi nchini Canada ili kusaidia hospital za Unguja na Pemba.