NA ABDI SULEIAMN.
WANANCHI wa Kisiwa cha Kokota kilichopo nje kidogo ya Wilaya ya Wete, wamesema kuwepo kwa huduma ya umeme ya uhakika ndani ya kisiwa hicho, utaweza kuinua hali za maisha yao na kuuza samaki wao katika masoko yoyote wanayoyataka.
Wamesema kwa sasa imekua ni shida kwa mvuvi kubakia na samaki wake baada ya kurudi baharini, kutokana na kutokuwa na sehemu ya kuwahifadhi.
Hayo waliyaeleza wakati walipokua wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kumalizika kwa zoezi la usajili kwa ajili ya kuungiwa huduma ya umeme na wafanyakazi wa ZECO Pemba.
Khamis Haji Kombo mkaazi wa kisiwa cha Kokota, alisema wamekua na furaha kubwa baada ya kuona kazi ya miuondombinu ya umeme kufika, ili kurahisisha shuhuli za bishara zao za Samaki na Pweza.
“Sasa tumeanza kujiona ni wananchi wa awamu ya nane kweli, sisi kwetu umeme mpaka tuvuke kwenda wete simu zetu kuchaji mtihani, ila kufika kwao ZECO ni matumaini tosha ya kuanza kupata huduma hiyoo,”alisema.
Kesi Ali Kesi Mkaazi wa Kisiwa cha Kokota, alisema mabadiliko makubwa wanatarajia kutokea, ikiwemo kukua kwa biashara hata ZAWA wafika na kuwachimbia kisima cha maji.
Aidha aliwataka wadau wa maendeleo kujitokeza kusaidia shuhuli vipaza sauti katika mskiti wao wa Ijumaa, pamoja na mambo mbali ili wananchi waweze kusikia hutuba na adhana zinazoaziniwa msikitini hapo.
”Tunajua umeme ni moja ya kitu kinachorahisisha maendeleo ya sehemu yoyote ile, hivyoi ni wazi sasa wananchi wa njau tutegemee mabadiliko hayo”alisema.
Kwa upande wake Afisa mawasiliano na huduma kwa wateja ZECO Pemba Haji Khatib Haji, alisema jumla ya kaya 65 zimesajiliwa ili kuungiwa huduma hiyo ya umeme kati ya kaya 96 zilizomo ndani ya kisiwa hicho.
Alisema wananchi wa Kokota wamepata bahati ya peke yao ya kuungiwa umeme kwa shilingi Elfu 50000/= jambo ambalo ni tafauti na maeneo mengine.
“Tumetoa ofa hii ya pesa ndogo kulipa, ila hata hivyo baadhi yao wameshindwa tumetoa ofa ya Umeme wa Mkopo mtu kulipa elfu 30000/= pia mtu hana, jamani fursa inapokuja hairudi tena”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo iliyotolewa na ZECO, ya kupata huduma hiyo ya umeme kwa kuhakikisha wanaungiwa umeme ndani ya nyumba zao.