Monday, November 25

RC Mattar awaasa waendesha bodaboda.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MKUU wa Mkoa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud amewataka waendesha bodaboda kufanya kazi kwa nidhamu, kuzingatia utaratibu na sheria za barabara, ili kuepusha matatizo yanayoweza kutokea.

Akizungumza na madereva wa bodaboda katika ukumbi wa Mesi ya Jeshi la Polisi Chake Chake, Mkuu huyo alisema, hapendi kuona mtu yeyote anabugudhiwa, ananyanyaswa au kudhulumiwa, hivyo wahakikishe kwamba wanafuata taratibu na sheria zote za barabara.

Alisema kuwa, hatua wanazozichukua hawakusudii kumuumiza mtu, hivyo ni vyema kwa madereva hao kujiongoza wenyewe katika kuchukua tahadhari wanapokuwa barabarani, ili asiwaathiri wananchi wengine.

“Musisubiri kusimamiwa na mamlaka zinazohusika, nyinyi ni watu wazima, fuateni utaratibu na sheria zinazotakiwa, ili kuepusha matatizo na majanga ikiwemo ya ajali”, alisema Mkuu huo.

Aidha aliwataka madereva hao wa bodaboda kuzisajili bodaboda zao kuanzia Januari 28 hadi Febuari 15 mwaka huu na endapo kuna ambae hakujisajili, ikifika Febuari 16 hatoruhusiwa kufanya kazi.

“Ikifika Febuari 16 mwaka huu, hukusajiliwa, tukikukamata utachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa faini, tujitahidi kwa sababu hizo ndio ajira zenu”, alisema.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Richard Tadei Mchomvu alieleza kuwa, wanaona fahari kuwa na vijana ambao wamejikita katika biashara ya bodaboda kwa ajili ya kujipatia kipato, lakini hawaridhiki na wanavyotoa huduma kwa wananchi.

“Wanaendesha mwendo wa kasi, hawavai kofia ngumu, wanapakia idadi kubwa ya abiria na hawafuati taratibu nyengine za kisheria, kwa hivyo wanahatarisha maisha yao na ya abiria wao”, alisema Kamanda huyo.

Alisema, kuanzia mwaka 2020 hadi hadi kufikia mwaka 2021, kuna wananchi na madereva 19 ambao wamefariki na 12 kujeruhiwa ambao wamepata ajali zitokanazo na bodaboda.

Nae Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa huo Shawal Abdalla aliwataka madereva hao kutii sheria za usalama barabarani bila ya kushurutishwa, ili kuepuka malalamiko katika jamii.

“Fujo hazina maana, nyinyi mnafanya biashara na mnatarajia kipato kitakachowasaidia kimaisha, hivyo iwapo hamtofuata sheria mutaingia mashakani na hamutoweza kufanya biashara”, alifahamisha.

Mwenyekiti wa Bodaboda mkoa huo Kassim Juma Khamis aliwataka madereva hao kuyafanyiakazi yote waliyoelekezwa kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla, kwani biashara yao ndio tegemeo lao.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kusini Pemba Amour Hamad Saleh alisema, lengo la mkutano huo ni kuhakikisha madereva wa bodaboda wanafuata sheria zote za barabarani bila ya kushurutishwa.

Januari 15 mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa huo lilifanya operesheni katika maeneo mbali mbali kwa lengo la kupambana na uhalifu, ambapo walikamata vyombo vya moto vya miguu miwili 72 vikiwa na makosa mbali mbali ya usalama barabarani.