Monday, November 25

YETA yakutana na wanafunzi wa Skuli ya Konde na Mgogoni Sekondari

NA ABDI SULEIMAN.

JUMUIYA ya Kuwezesha Vipaji vya vijana Pemba(YETA),imewataka wanafunzi Skuli ya Konde Sekondari na Mgogoni Sekondari, kuhakikisha wanakuwa makini katika kipi ndi hiki cha uchumaji wa zao la karafuu kwa kuepukana na vitendo vya udhalilishaji vinavyoweza kupelekea migogorio katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa na mjumbe wa Jumuiya hiyo Haroub Ali Nassor, alipokua akizungumza na wanafunzi wa skuli hizo ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kujenga uwelewa kwa vijana, katika kuzuwia ukatili na migogoro katika kipindi cha mavuno ya zao la karafuu Pemba.

Alisema YETA imeweza kukutana na wanafunzi 154, konde Sekondari wanafunzi 68 na Mgogoni Sekondari wanafunzi 86 lengo ni kupunguza na kuzuwia migogoro na udhalilishaji kipindi cha mavuno hayo, ikizingatiwa wanafunzi ndio waathirika wakubwa kwenye matendo hayo.

“Sisi tumeamua kujikita zaidi kwa vijana kama hawa wlioko maskulini, ili wao waweze kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao katika kutokomeza hili,”alisema.

Aidha Haroub aliwataka wanafunzi hao kuwa mabolozi kwa wanafunzi wenzao na jamii, iliyowazunguruka ili mafanikio makubwa yaweze kupatikana.

Akiwasili mada kwa wanafunzi katika kuzuwia masuala ya udhalilishaji na migogoro, kipindi cha mavuno ya zao la karafuu Mwezeshaji Sada Aboubakar Khamis, alisema vitendo vya udhalilishaji bado ni janga kubwa lililopo katika jamii, hivyo wanafunzi wanapaswa kuwa na makini katika kipindi hiki cha uchumaji wa karafuu.

Alisema kipindi hiki matukio mengi ya udhalilihaji na ubakaji hutokea katika mashamba ya mikarafuu, huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake, kisingizio ni ukoataji wa mapeta.

Aidha aliwataka wazazi kuwa karibu sana na watoto wao, hususna katika kipindi cha uchumaji wa karafuu, sasamba na kuwauliza juu ya wingi wa karafuu wanapozipata wakati sio vibarua.

“Sote tunajua kama Mpeta umekatazwa na hautakiwi, wapo wanaoenda mpeta na kuiba karafuu za watu, wengine wanaenda kwa mambo yao ikiwemo kufanya mapenzi na ubakaji mwengine unatokea humo humo”alisema.

Naye Dk.Ali Yussuf Ali ambaye ni mwezeshaji, alisema kipindi cha Karafuu Mogogoro mingi hutokea katika jamii na kusababisha uvunjifu wa amani, ajambo ambalo linapaswa kupingwa kwa nguvu zote.

Alisema lazima wanafunzi wanapaswa kujitambua ili kuona migogoro hiyo haitokei, kwa kuelimisha jamii na wanafunzi wenzao hasa kipindi cha mavuno ya zao la karafuu.

“Migogoro mingi inayotokea ni ukataji wa mikarafuu, wizi wa karafuu na ukataji wa matawi, jambao ambalo mwisho wake hupelekea uvunjifu wa amani baina ya mwenye shamba na vibarua na wananchi,”alisema.

Aidha Dk.Ali aliwataka vijana kulinda matamanio yao na kujitambua, pamoja na kuepuka upokeaji wa zawadi kiholela zisizokuwa za masingi.

Hata hivyo aliwataka kutambua kuwa vitendo vya udhalilishaji kipindi cha mavuno ya karafuu vinapelekea kutokea kwa migogoro na uvunjifu wa amani.

Nao wanafunzi wa skuli ya Konde Sekondari na Mgogoni Sekondari Wilaya ya Micheweni, wameipongeza Jumuiya ya YETA kwa kufika na elimu hiyo katika kipindi hiki cha mavuno ya Karafuu katika mkoa wa Kaskazini Pemba.

Walisema watahakikisha elimu hiyo wanaifikisha kwa jamii na wanafunzi wenzao, kwa lengo la kuondosha migogoro na udhalilishaji katika kipindi hichi.