NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MTU mmoja amefariki dunia baada ya kupigwa na shoti ya umeme nyumbani kwake Wingwi Mapofu Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo Juma Sadi Khamis alimtaja marehemu huyo kuwa ni Hamad Juma Said mwenye umri wa miaka 32 mkaazi wa Wingwi.
Alisema kuwa, tukio hilo limetokea majira ya saa 10:00 jioni, ambapo Hamad alipigwa na shoti hiyo wakati alipokuwa anafungua friza lake na ndipo mauti yalipomfika.
“Kabla ya kumfika mauti Hamad alikwenda kwenye friza lake kufungua ingawa alipigwa na shoti ya umeme na kufariki papo hapo”, alisema Kamanda huyo.
Alieleza kuwa, chanzo cha tukio hilo ni kwamba, wakati anafungua friza ilitokea shoti ya ghafla na kusababisha kurushwa na kuingia kwenye friza lenyewe, ambapo umeme ulimkamata na baada ya kukaguliwa alikuwa tayari ameshafariki.
“Baada ya kupata taarifa hizi, Jeshi la Polisi tuliwasiliana na Shirika la Umeme pamoja na daktari ili kuweza kushibitisha kuwa ni shoti ya umeme au la”, alisema.
Kamanda Sadi aliwataka wananchi kuwa, wanaposhughulikia nyumba zao kwa mambo ya umeme, ni vyema kuwataarifu Shirika la Umeme kwani wao ni wataalamu zaidi.
Baada ya uchunguzi wa daktari maiti hiyo ilikabidhiwa jamaa zake na tayari imeshazikwa.
MWISHO.