Monday, November 25

Akamatwa na misokoto 901 ya dawa za kulevya.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limemkamata Mbarouk Khamis Abdalla mwenye umri wa miaka 47 baada ya kupatikana na misokoto 901 ya dawa za kulevya aina ya bangi huko Makombeni Mkoani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Richard Tadei Mchomvu alisema, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 27 mwaka huu majira ya jioni huko Makombeni Mkoani akiwa na misokoto 901 ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Alieleza kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya Jeshi hilo kufanya msako katika maeneo yote ya Mkoa wa Kusini Pemba kwa lengo la kuwaweka wananchi katika hali ya usalama.

“Dawa hizo za kulevya zinatokea Tnga na zinaingizwa kwenye magari ya mizigo yanayotoka Tanga na kupita kwenye bandari zetu, hivyo tunawaomba wananchi wazidishe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuendelea kuwakamata wahalifu”, alisema Kamanda huyo.

Katika tukio jengine Kamanda huyo alisema, walimkamata mtuhumiwa Fatuma Mtoro mwenye miaka 33 wa Machomane Chake Chake kwa kupatikana na boksi kumi (10) ya pombe nyumbani kwake.

“Unywaji wa pombe ovyo umekuwa ni kero kubwa katika Mkoa wetu, watu wanauza na kunywa pombe holela, hiyo haikubaliki kwani kuna utaratibu wa kutoa leseni kwa ajili ya kuuza vileo”, alisema Kamanda huyo.

Aliwataka wananchi wasaidie kutoa taarifa za uhalifu katika Mkoa, kwani kanuni na taratibu za uendeshaji wa maisha na biashara haziruhusu uuzaji wa vileo.

Alisema kuwa, kutokana na mashirikiano mazuri kati Jeshi la Polisi na wananchi, ndipo wanafanikiwa kuwakamata wahalifu hao mara baada ya kufika kisiwani hapa.

Aliwaomba wananchi kuzidisha ushirikiano ili kuendelea kuwakamata wahalifu, jambo ambalo litasaidia kujenga Taifa imara lenye vijana ambao ni nguvu kazi.