Monday, November 25

Vijana wawili wakamatwa na misokoto 677 ya dawa za kulevya aina ya bangi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limewakamata vijana wawili baada ya kupatikana na misokoto 677 ya dawa za kulevya aina ya bangi katika eneo la Machomane Wilaya ya Chake Chake.

Vijana hao ni Rashid Rajab mwenye umri wa miaka 32 mkaazi wa Machomane Chake Chake na Akida Mbega Bakari mwenye umri wa miaka 36 mkaazi wa Mkoani Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Richard Tadei Mchomvu alisema, watuhumiwa hao walikamatwa Januari 29 mwaka huu majira ya mchana huko Machomane wakiwa na misokoto 677 ya dawa za kulevya aina ya bangi.

“Mtuhumiwa Akida ni mkaazi wa Morogoro, hivyo kuna uhusiano mkubwa kati yake na mtuhumiwa Rashid, ambapo bangi inalimwa Mkoani huko na kuisafirisha kuileta Pemba”, alieleza Kamanda huyo.

Akijibu suala kuhusu uingiaji wa dawa hizo, alisema kuwa uhalifu ni taaluma kama taaluma nyengine, hivyo wahalifu hutumia njia mbali mbali kuhakikisha wanapitisha madawa hayo.

“Wahalifu wanaficha dawa za kulevya kwenye mizigo ya bidhaa nyengine zinazokuja Pemba, wanaichanganya kwenye magunia ya mbatata, vitunguu na sehemu nyengine, hivyo wanapita bandarini bila kuonekana”, alieleza.

Alisema kuwa, kutokana na mashirikiano mazuri kati yao na wananchi, ndipo wanafanikiwa kuwakamata wahalifu hao mara baada ya kufika kisiwani hapa.

Aliwaomba wananchi kuzidisha ushirikiano ili kuendelea kuwakamata wahalifu, jambo ambalo litasaidia kujenga Taifa imara.