Monday, November 25

Mzozo wa Hijabu: Muskaan Khan Mwanamke wa India anayepambania vazi la Hijab.

hijab

Muskaan Khan bila kukusudia amekuwa uso wa upinzani kwa wanawake vijana wa Kiislamu wa India huku kukiwa na mzozo unaoongezeka juu ya hijabu au hijab.

Katika video ambayo imesambaa mitandaoni, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 alionekana akiingia chuoni kwake huku kundi la wanaume likimkaribia.

Wakiwa wamevalia mitandio yenye rangi inayohusishwa na Uhindu na vikundi vya utaifa wa Kihindu – walianza kupiga kelele “Jai Shri Ram” au “ushindi kwa Bwana Ram”.

Walipokuwa wakiendelea kumzonga, Bi Khan, ambaye alikuwa amevaa hijabu, akiwa amefunika uso wake pamoja na gauni refu jeusi, alisimama kidete – akapiga kelele “Allahu Akbar” (Mungu ni mkuu) kwa kujibu.

Punde, wakuu wa chuo walimsindikiza ndani.”Ninachotaka ni kusimama na haki na elimu yangu,” aliiambia BBC kutoka nyumbani kwake katika mji wa Mandya katika jimbo la Karnataka, ambapo video hiyo ilirekodiwa.

“Sina shida na mavazi wanayovaa,” alisema, akiongeza watu wanaweza kuvaa nguo za saffron au vilemba chuoni, kama vile alivyovaa hijabu.

Bi Khan na mamilioni ya wanawake Waislamu nchini India huvaa hijabu na burka kila siku – lakini chaguo hilo limegeuka kuwa la utata katika wiki za hivi karibuni.

kanda ya video ya Khan akilikaripia kundi la vijana ilisambazwa sana
Maelezo ya picha,kanda ya video ya Khan akilikaripia kundi la vijana ilisambazwa sana

Ilianza wakati wanafunzi katika chuo cha awali cha chuo kikuu, sawa na shule ya upili, katika wilaya ya Udupi ya Karnataka, walipoanza kuandamana mwezi uliopita wakilalamikia kupigwa marufuku kwa hijabu – chuo hicho kilisema wanafunzi wanaweza kuvaa hijabu kwenye chuo lakini sio darasani.

Suala hilo tangu wakati huo limetanda wakati shule nyingine zilipoanza kutekeleza marufuku kama hiyo – na limechukua sura ya jumuiya huku wafuasi wa makundi ya Kihindu wakianzisha maandamano kuunga mkono marufuku hiyo.

Maandamano yalipogeuka kuwa ghasia katika baadhi ya maeneo, serikali ya Karnataka ilifunga shule za upili na vyuo – na suala hilo limefikia hata mahakama kuu ya jimbo hilo.

Mahakama ya kikatiba ya majaji watatu itasikiliza kesi hiyo siku ya Alhamisi.

Wakati huo huo, vyuo vikuu vinaonekana kuwa na mgawanyiko huku wanafunzi wa Kihindu wakijitokeza wakiwa wamevaa mitandio ya zafarani.

Bi Khan, bintiye mfanyabiashara wa eneo hilo, anadai kwamba katika kesi yake, hali hiyo ilipangwa zaidi na wanaume ambao walikuwa “wageni” na sio wanafunzi au wanafunzi wenzao.

“Nilifika chuoni kwangu kuhudhuria darasani na nikakuta kuna vijana wengi waliovalia nguo za zafarani,” alisema.

“Walifunga njia yangu na kusema kwamba singeweza kuingia katika eneo la chuo.”

Alipofika getini alisema aliona wanafunzi watatu au wanne waliokuwa wamevaa burka wakirudishwa nyuma na vijana hao.

“Walikuwa wameshika skafu zao na walikuwa wakipiga kelele za Jai Sri Ram. Waliniambia nivue hijabu yangu na hapo ndipo ningeruhusiwa kuingia chuoni kwangu. Walinitisha.”

Lakini Bi Khan alisema alikuwa amedhamiria kupigana. Aliegesha skuta yake na kuelekea darasani kwake, wakati, alisema, “vijana 30-40” walikuja kwake, wakipiga kelele “Jai Shri Ram”.

“Kwa mara nyingine tena, waliniambia nivue hijabu ikiwa ninataka kuingia ndani,” alisema. “Ndio, nilipiga mayowe Allahu Akbar.

Ninapoogopa, ninamwomba Mwenyezi Mungu na ananipa nguvu.” Hapo ndipo mkuu wa shule na walimu walipotoka nje kwa kasi na kumpeleka ndani.

vitambaa vya kichwa vinavyovaliwa na wanawake Waislamu
Maelezo ya picha,vitambaa vya kichwa vinavyovaliwa na wanawake Waislamu

Bi Khan anasema amefurahi kuona pongezi alizopokea kwenye mitandao ya kijamii: “Mapenzi mengi wanayonipa na yananipa nguvu sana. Ninawashukuru sana.”

Pia anaweka wazi kwamba “hatofautishi kati ya Wahindu na Waislamu”. “Wavulana hawa walikuwa hawaniruhusu kujielimisha [mwenyewe] kwa sababu nimevaa hijabu,” alisema. “Kwa hivyo, ninasimama tu kwa ajili ya haki yangu.”

CHANZO CHA HABARI BBC SWAHILI.