Serikali ya Tanzania kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imetoa tamko kuhusu ongezeko la bei za bidhaa nchini humo .
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa wafanyabiashara nchini kuacha tabia ya kupandisha bei ya bidhaa za ujenzi kiasi cha wananchi kushindwa kuzipata bidhaa hizo kwa gharama nafuu na kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika.
Majaliwa ameyasema hayo siku ya Alhamisi Februari 10, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa Msalala (CCM), Iddi Kassim katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni jijini Dodoma.
Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya serikali kuhusiana na mfumko wa bei za vyakula ikiwemo mafuta, sabuni na vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na majibu.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kumejitokeza kupanda kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Amesema upandaji ambao wakati mwingine ni wa makusudi unafanywa na wafanyabiashara wasiowaaminifu.
Hata hivyo aliongeza kuwa upandaji huo wakati mwingine husababishwa na upandaji wa malighafi.
Amesema miongoni mwa makusudi hayo ni wazalishaji kuzalisha bidhaa kidogo na hivyo kutengeneza upungufu mtaani ili bei zipande.
‘Njama’ za wafanyabiashara
Aidha, amesema kumekuwa na utamaduni wa uovu wa wafanyabiashara wa kukaa kwa pamoja na hivyo kusababisha bei za bidhaa kupanda.
“Ndio maana Waziri (Dk Kijaji) ametoka hadharani kutueleza mkakati wa Serikali. Naunga mkono mkakati huo lakini natoa agizo kwa wafanyabiashara kuacha tabia hiyo ovu inayopelelea jamii kushindwa kupata bidhaa kwa gharama nafuu,” amesema.
Majaliwa amesema wafanyabiashara wamekuwa wakiwekewena mikataba na Serikali na pia wakati wanajenga mazingira wezeshi ya biashara nchini, jambo kubwa lilikuwa ni kupata bidhaa kwa wingi, kwa bei nafuu na kuwezesha kupatikana wakati wote.
Waziri Mkuu amesema hata hivyo wafanyabiashara wengine wameanza kukiuka hayo.
“Serikali itaendelea kuchukua hatua kali na kusimamia upandaji wa bei hizi zisiendelee kupanda wakati wote. Naagiza Taasisi yetu ya FCC kusimamia haki za wafanyabiashara katika kufanya biashara, ihakikishe inafanya ukaguzi wa kina kwa bidhaa zinazozalishwa na mauzo yao walinganishe na uzalishaji wao kwa mwaka,” amesema.
Amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wafanyabiashara wanaoweka mkakati wa kuisumbua jamii kwa kununua bidhaa kwa bei ya juu bila sababu yoyote.
CHANZO CHA HABARI BBC SWAHILI.