NA ABDI SULEIMAN.
WANAWAKE wajasirimali ambao ni wanufaika wa Mradi wa Miliki Uwezo unaotekelezwa Kijana Hai Foundati, wamesema kuwa watahakikisha wanasimamia ipasavyo biashara zao na kufikia malengo waliojiwekea katika vikundi vyao vya ushirika.
Wamesema mafunzo ya Usimamizi wa biashara waliopatiwa na watendaji wa Idara ya Ushirika na CRDB, yataweza kuwafumbua akili zao katika biashara na kuona wanatimiza kile wanachokitaka.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika skuli ya Madungu Sekondari Wilaya ya Chake Chake, mara baada ya kupatiwa mafunzo juu ya usimamia wa biashara kutoka kwa Idara ya Ushirika na benka ya CRDB.
Mmoja wa wanawake hao Mchanga Mussa Said kutoka kikundi cha ndoto zetu, alisema kupatiwa kwa mkopo wa kuwawezesha wajasiariamali kupitia serikali ya awamu ya nane ni fursa kwao ya kukuza biashara zao.
“Utatusaidia zaidi kupelekea mbele matarajio yetu, kwa vile tumeshaanza kupata mafunzo ya mikopo, biashara tutakazozalisha zitaweza kuwa na viwango vikubwa,”alisema.
Alisema kwa sasa biashara yao ya vyombo ipo na inaenda na wakati, kikubwa ni mtaji wakuongezea mwisho kuwa na duka la moja kwa moja.
Aziza Said Ali kutoka Ole, aliishauri serikali kuhakikisha inawafikiria kwa jicho la huruma vikundi vya akinamama na wajane kuwapatia mikopo isiyo na riba wala vikwazo ili kup=fikia ndoto zao.
“Wanawake wengi ni maskini na ndio walioamua kujikusanya kwa pamoja, sasa leo mikopo ikiwaangalia kwa umakini na kuwapatia sio na riba watafikia hatua kubwa,”alisema.
Kwa upande wake afisa Kutoka Idara ya Uwezeshaji Faridi Hamuni Juma, alisema wajariamali wengi wameitikia wito na kunufaika na mikopo hiyo na kusajili vikundi vyao na zoezi la uhakiki linaenda vyema.
Alisema serikali imetenga shilingi Bilioni 81 za Covidi 19 kwa ajili ya wajasirimali tu, huku asilimia 35% inakwenda kwa wanawake, asilinia 5% ni vijana, huku akiwataka wanawake kushajihishana kuunda vikundi vya ushirika ili waweze kunufaika na fedha hizo.
“Serikali ya awamu ya nane imedhamiria kuwainua wajasiriamali kwa asilimia kubwa, jukumu letu kuchangamkia fursa hiyo na fedha hizo hazitokua na ruba hata kidogo,”alisema.
Hata hivyo aliwataka wanawake kuondosha dhana kuwa kila kitu hawawezi na kutegemea ajira serikalini wakati ujasiriamali ni ajira tosha, iwapo atakubali kufuata taratibu na kanuni za ujasiriamali.
Naye meneja wa mradi wa miliki uwezo unaotekelezwa na Kijana hai Foundation Suliman Mwinyun Baitan, alisema wanawake wanapata shida sana kutengeneza malengo, mikakati, ikiwa wataweza hivyo basi watakuwa wajasiriamali wakubwa sana.
Alisema Kijana hai Foundation watahakikisha wanawasimamia ipasavyo wanawake hao, kuhakikisha miradi walioibuni na kuianzisha katika vikundi vyao vinafanikiwa na kuanza kuzalisha.