Wednesday, January 8

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS AWAONGOZA WAUMINI WA KIISLAMU KATIKA HAULI YA MAALIM SEIF

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, jana ameongoza Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, waumini wa Kiislam na wananchi mbali mbali katika Hauli ya kumkumbuka na kumuombea Dua maalum Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

Dua hiyo maalum imefanyika huko Masjid Jibirili Mkunazini jijini Zanzibar na ilisimamiwa na Sheikh Abdurahman Alhabshy kwa khitma na nyiradi mbali mbali za kumuombea maghfira Marehemu Maalim Seif.

Waliohudhuria katika dua hiyo ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Ndugu Juma Duni Haji, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wake Zanzibar, Salim Abdalla Bimani, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, Wanachama na Viongozi waandamizi wa ACT-Wazalendo, masheikh, waumini na wananchi mbali mbali visiwani hapa.

Marehemu Maalim Seif alifariki dunia tarehe 17 Februari mwaka jana huko Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu na kuzikwa siku ya pili yake kijijini kwao Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo sasa ametimiza mwaka moja tokea kufariki kwake.

Marehemu Maalim hadi anafariki alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT- Wazalendo na pia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, wadhifa ambao aliutumikia kuanzia tarehe 8 Disemba 2020 hadi tarehe 17 Februari 2021 alipofariki Dunia.

Mapema wiki iliyopita Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Othman Masoud Othman aliungana na viongozi mbali mbali wa ACT-Wazalendo pamoja na wakaazi wa Pemba kulizuru Kaburi la Marehemu Maalim Seif huko Mtambwe pamoja na kumuombea dua.

Hafla ya dua ilifanyika pia jana Kijijini kwa Marehemu Maalim Seif, Nyali Mtambwe alikozikwa ambapo viongozi na wananchi mbali mbali wa kisiwani Pemba walihudhuria.

Marehemu Maalim Seif ambaye alikuwa mwanasiasa mkongwe, alitumikia nyadhifa mbali mbali za kisiasa na serikali ikiwa ni pamoja na nyadhifa za Waziri Kiongozi na Waziri wa Elimu kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar wadhifa ambao aliushikilia katika vipindi vya awamu mbili tofati, baada ya maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye ACT-Wazalendo.

Marehemu Maalim Seif pia atakumbukwa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Afrika na kwingineko duniani kutokana na michango na ushawishi wake katika mageuzi ya siasa , sera, fikra na falsafa mtambuka kupitia nyanja mbali mbali za maisha ya jamii, uchumi, upinzani, maendeleo na maridhiano, sambamba na siasa za demokrasia ya kiliberali ulimwenguni.