Thursday, January 9

MWAMUZI FRANK KOMBA KUTOKA TANZANIA AMETEULIWA NA CAF KUCHEZESHA MCHEZO KATI YA AMAZULU NA SETIF AFRIKA KUSINI

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limemteua refa wa Tanzania, Frank Komba kuwa miongoni mwa Waamuzi watakaochezesha mchezo wa hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya wenyeji, Amazulu na ES Sètif ya Algeria) Februari 25, mwaka huu Uwanja wa Mosses Mabhida, Durban nchini Afrika Kusini.

Aidha, CAF pia imewateua marefa wa kike wa Tanzania, Florentina Zablon, Janeth Balama, Glory Tesha na Tatu Malogo kuchezesha mchezo wa Kufuzu Kombe la Dunia kwa Wanawake U20 baina ya Ethiopia na Ghana Machi 13, mwaka huu Uwanja wa Abebe Bekila, Jijini Addis Ababa, Ethiopia.

CAF pia imemteua Meneja wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TPLB), Jonathan Kasano kuwa Mratibu wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya ndugu, Al Merrikh na Al Hilal Februari 25, mwaka huu Jijini Khartoum nchini Sudan.
Naye Meneja Mashindano wa TFF, Baraka Kizuguto ameteuliwa na CAF kuwa Mratibu wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya ndugu pia, GD Sagrada Esperança na Petro Atlético Februari 26 nchini Angola.