Thursday, January 9

SERIKALI YA MAREKANI YAKABIDHI VIFAA TIBA VYA OKSIJENI KWA HOSPITALI NNE ZA RUFAA ZA MIKOA KUSAIDIA MATIBABU YA UVIKO-19.

 Dar es Salaam,

Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kushirikiana na Shirika la Save the Children nchini Tanzania wamekabidhi msaada wa vifaa tiba vya oksijeni kwa hospitali nne za kanda za rufaa kwa ajili ya udhibiti wa kesi za wagonjwa mahututi wa UVIKO-19. Waliohudhuria katika hafla hii ni, Mganga mkuu wa Serikali na mgeni rasmi Dkt. Wedson Aifello Sichalwe; Mkurugenzi wa kitengo cha kukabiliana na Maandalizi ya Dharura (EPR), Wizara ya afya, Dkt. Elias Kwesi; Mkurugenzi wa Afya wa USAID, Bi. Ananthy Thambinayagam na Bester Mulauzi, Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Save the Children.

Vifaa vilivyotolewa ni vile vinavyotumika katika mfumo wa matibabu ya upumuaji (oxygen cylinders, handheld gas monitors, pulse oximeters, glucometers, gauges and flowmeters with humidifiers, and oxygen cylinder carts). Vifaa hivi vitawawezesha watoa huduma za afya wa mikoani kutoa huduma bora itakayookoa maisha, huku vikisaidia juhudi zinazoendelea za serikali ya Tanzania kupambana na UVIKO-19. Makabidhiano haya pia yanadhihirisha dhamira endelevu ya Marekani ya kuwasaidia Watanzania katika kipindi chote cha janga hili.

Serikali ya Marekani inatambua ugonjwa wa UVIKO-19 kama changamoto ya kimataifa inayohitaji mwitikio wa kimataifa. Kama mfadhili mkubwa zaidi wa afya wa masuala ya kibinadamu na maendeleo endelevu, Marekani inaendelea kuongoza mwitikio wa misaada ya kibinadamu na afya duniani kwa janga hili la UVIKO-19. Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania, serikali nyingine na marafiki wengine na washirika katika kukabiliana na janga hili. Zaidi ya hayo, tunaendelea kuongoza jitihada za kimataifa dhidi ya UVIKO-19 kupitia mbinu ya kina inayojumuisha sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kidini na mengine.

Kutokomeza janga hili la UVIKO-19 huanza na chanjo. Marekani imetoa dozi milioni 450 za chanjo kwa nchi 110, ikiwa ni mchango mkubwa zaidi kuliko nchi nyingine zote kwa pamoja. Hii inajumuisha zaidi ya dozi milioni 5 za chanjo zilizotolewa kwa Tanzania. Mbali na michango ya Serikali ya Marekani ya chanjo hadi sasa, shirika la USAID limewekeza jumla ya dola milioni 27.5 nchini Tanzania kusaidia kukabiliana na athari za janga hili. Tumefanya hivyo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha upatikanaji ziadi wa chanjo za UVIKO-19. Tumeshirikiana na Serikali ya Tanzania kupunguza maradhi na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa kuwasaidia madaktari kujua jinsi ya kuwatibu wagonjwa na kuwa na vifaa vya kutosha vya kusaidia wagonjwa. USAID pia imezuia madhara ya janga hili kwenye miradi ya VVU/UKIMWI na wanufaika wake.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa afya USAID, Bi. Ananthy Thambinayagam alisisitiza dhamira ya Marekani kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania na wadau kama shirika la Save the Children kutokomeza janga hili la UVIKO-19.

“Janga la UVIKO-19 ni kati ya changamoto kubwa zaidi kwa afya, ustawi, na usalama wa kiuchumi wa watu wote. Ni lazima tushirikiane kushugulikia janga hili kwa uharaka,” alisema Bi. Ananthy Thambinayagam, Mkurugenzi wa afya USAID.