Thursday, January 9

SMZ INATAMBUA UMUHIMU WA WATAALAM WA TEHAMA NCHINI

SERIKALI ya Mapinduzi  Zanzibar inatambua umuhimu ya kuwa na wataalam wa TEHAMA wabobezi wenye ujuzi mahiri kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa. 
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Rahma Kassim Ali alieleza hayo katika hafla ya ufunguzi wa Semina ya wataalamu wa TEHAMA iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Mhe. Rahma amesema Serikali zote mbili zimewekeza kwa kiasi kikubwa katika kutoa elimu ya TEHAMA kulikowezesha kuzalisha wataalamu ambao kutokana na mabadiliko ya kasi wanahitaji kuwendelezwa ili kukabiliana na changamoto za maendeleo ya TEHAMA.
Alieleza kuwa, Mbali na kuendeleza wataalamu wa TEHAMA, SMZ kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imekuwa ikitoa  ushirikiano wa kutosha katika kukuza ubunifu na tafiti mbali mbali katika TEHAMA.
Aidha, aliipongeza juhudi za Tume ya TEHAMA Nchini kwa kuanza kusajili wataalam wa TEHAMA  ikiwemo wataalam kutoka Zanzibar ambao wameanza kunufaika na Mpango (program) za Tume za kuwaendeleza kupitia mafunzo na kubadilishana ujuzi na uzoefu.
Katika hatua nyengine Waziri Rahma Kassim Ali alisema suala la Kutambua na kusajili wataalam wa TEHAMA linatokana na Sera ya CCM na maelekezo na viongozi wakuu wa Nchi ambapo amewahimiza wataalam wote wa TEHAMA Zanzibar kujisajili katika Tume ya TEHAMA.
“Ninahimiza waajiri wote ikiwemo Serikali kama mwajiri Mkuu kuanza kutumia wataalam wa TEHAMA waliosajiliwa” Alisema Waziri Rahma.
Amefafanua kuwa kufanya hivyo katika kuweka mkazo kupitia Tathnia ya TEHAMA itaiwezesha Nchi kuendana na mabadiliko katika uchumi wa dunia ambao matumizi ya TEHAMA ni makubwa yamepiga hatua.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Rahma Kassim Ali aliitaka Tume ya TEHAMA kwa kushirikiana na taasisi za TEHAMA Zanzibir ikiwemo Idara ya Mawasiliano, Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar (ZICTIA), Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na nyinginezo kuanzisha Mpango (Program) mahsusi za kuendeleza Kampuni changa na wabunifu  wa TEHAMA.
“TEHAMA ni moja ya nguzo muhimu ya uchumi wa kidijitali (Digital economy) katika Karne hii ya 21” Alieleza Mhe. Rahma
Alieleza kwamba, Ilani ya CCM inatambua kuwa dunia hivi inapita katika mapinduzi ya nne ya viwanda maarufu kama “4th Industrial Revolution (4IR)” yanayowezeshwa na TEHAMA, hivyo Taifa linahitajika kujipanga ili kufanikisha mageuzi (transformation) kuelekea uchumi wa kidijitali ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji zinategemea teknolojia za juu za TEHAMA.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakar alieleza kuwa, Katika zama hizi TEHAMA ni nyenzo muhimu kwa kuiwezesha jamii kushiriki ipasavyo katika Uchumi wa Kidijital (Digital Economy).
Pia alisema TEHAMA imetoa fursa mbali mbali ikiwemo kufanya biashara za kibenki kwa njia ya simu na internet pamoja na kufanya shughuli za kila siku (e.bussiness).
Katibu Mkuu Hamil alieleza kuwa, pamoja na mafanikio yaliofikiwa Nchini lakini bado Zanzibar iko nyuma katika matumizi ya TEHAMA kutokana na changamoto ya watu wake kutokutumia teknolojia ya TEHAMA katika kutatua matatizo yanayoweza kupatiwa ufumbuzi.
“Nawaombeni wataalamu wa TEHAMA tuitendee  haki taaluma yetu ili kuirahisishia Serikali shughuli zake za kiutendaji” Alisema Katibu Mkuu Hamil Bakar
Alisema katika kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanaongezeka kwa jamii ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla Serikali imejenga vituo kumi (10) kwa lengo la kutoa Elimu na kuwasogezea karibu huduma hizo wananchi waliopo katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Simson John Mwela Alieleza kuwa pamoja na maendeleo yaliofikiwa lakini kuna athari kubwa inaweza kujitokeza kwa taifa endapo Nchi hatakuwa makini kwa kuwatambua wataalam wake ikiwemo kutokua na uhakika wa usalama wa mifumo ya TEHAMA pamoja na kutegemea wataalamu kutoka nje ya Nchi hali ambayo italigharimu Taifa pesa nyingi.
Kaimu Mkurugenzi Samson alimueleza Mhe. Waziri kuwa, zoezi la kuwasajili wataalam wa TEHAMA limeanza na linaendelea vizuri ambapo kuanzia 2020 wataalam Mia nane Sitini na Nne (864) kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar wamesajiliwa katika maeneo Thelasini na Moja (31) ya Ubozezi wa TEHAMA.
Alisema pamoja na zoezi hilo kuendelea Nchi nzima lakini kasi ya usajili wa zoezi hilo kwa upande wa Zanzibar bado mutikio ni mdogo, ambapo hivi karibuni Semina kama hiyo itafanyika Kisiwani Pemba ili nao wapate muamko wa kujisajili.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeipa shabaha Tume ya TEHAMA kukusanya wataalam Elefu Tano (5,000) ifikapo 2025.