Thursday, January 9

TUWAJENGEE UELEWA WABUNGE ILI KUKUZA UFANISI – MHE. OTHMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza matumaini ya Serikali kwa uongozi mpya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kujenga mwelekeo wa kuongoza kwa ufanisi na kulivusha Taifa kimaendeleo.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa akiongea na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Tulia Ackson aliyewasili hapo ili kujitambulisha.
Amesema uongozi huo unayo fursa ya kukuza mashirikiano kwa kuzingatia nafasi yake kwa Watanzania na pia Sheria zinazopitishwa Bungeni ambazo zinaathiri moja kwa moja mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sambamba na maisha ya watu, hapa visiwani.
“La muhimu pia ni namna ya kuzishirikisha ipasavyo taasisi husika za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano ili kujenga uelewa zaidi katika muundo halisi wa uongozi na kwaajili ya kuleta maendeleo yenye ufanisi”, amesema Mheshimiwa Othman.
Aidha Mheshimiwa Othman amelishauri Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujenga uelewa mpana kwa wabunge juu ya sekta mbali mbali zikiwemo za uchumi, diplomasia, usalama, utamaduni na maendeleo kwa ujumla, utakaozingatia pia athari za utendaji na majukumu yake ikiwemo utungaji wa sheria, zinazoigusa Zanzibar kama nchi yenye mipango yake inayojitegemea.
Akitilia mkazo umuhimu wa kukuza uelewa Bungeni, Mheshimiwa Othman ametolea mfano michango na mijadala ya baadhi ya wabunge ambayo kimantiki inakosa ‘afya’ kutokana na utambuzi finyu juu ya hadhi na nafasi ya Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Othman amezungumzia haja ya uchapishaji wa Miswada na Sheria mbali mbali zinazopitishwa na Bunge katika Gazeti Maalum la Serikali, huku akiahidi kuwa milango ipo wazi katika kuendeleza mshikamano na Mhimili huo muhimu wa Dola.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Tulia Ackson ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuipa mashirikiano taasisi yake na kuahidi kuongoza kwaajili ya maslahi ya wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Akieleza utayari wa uongozi wake uliochaguliwa hivi karibuni, Mheshimiwa Tulia amesema, “tunawategemea sana kama ambavyo tumekuwa tukishirikiana, tunaomba muendelee kutushauri, nasi tutakuwa tayari kutekeleza”.
Katika ujumbe huo, Mheshimiwa Tulia aliongozana na watendaji wake mbali mbali akiwemo Katibu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Mathew Kiuzo.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa  Zanzibar