Saturday, March 15

Wanafunzi 17124 wameanza masomo yao ya awali Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa mwaka 2022.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

KIASI Cha wanafunzi 17124 wameanza masomo yao ya awali katika Skuli mbali mbali za Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa mwaka 2022.

 

Kwa upande wa Skuli za maandalizi wanafunzi walioandikishwa ni 4623, walioanza darasa la Kwanza ni 10,090 na Wanafunzi wanaosoma tutu ni 2411.

 

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake, Ofisa elimu Mkoa wa Kaskazini Pemba Khamis Said Hamad alieleza kuwa wanafunzi hao ni wale ambao muda wao wa kuanza  kusoma umefika.

 

Alifahamisha kuwa kwa upande wa Wilaya ya Wete wanafunzi ambao walioandikishwa ni 7,797 ikiwa maandalizi ni wanafunzi 2538 na kwa darasa la awali (darasa la Kwanza) 5259.

 

“Wilaya ya Wete wanafunzi ambao wameandikishwa ni 7,797 ikiwa wavulana ni 4081 na wasichana ni 3716 ambao hao ndio watakaoanza masomo yao kwa mwaka huu,” alieleza Maalim Khamis.

 

Sambamba na hayo Maalim Khamis alieleza kuwa kwa upande Wilaya ya Micheweni, wanafunzi wote ambao wameandishwa ni 9327, ikiwa wanafunzi wa tutu ni 2411, maandalizi ni 2085 huku darasa la Kwanza ni 4831.

 

“Kwa upande wa Wilaya ya Micheweni wanafunzi wa kike ambao wameandikishwa ni 4855 huku wavulana wakiwa ni 4472,” alieleza Ofisa huyo.

 

“Kiujumla wanafunzi wote ambao wameandishwa kuanza masomo yao kwa mwaka huu ni 17,124 ikiwa wasichana ni 9221 na wavulana ni 7603,”alifahamisha Maalim Khamis.

 

Mapema Ofisa huyo alieleza kuwa changamoto kubwa iliyopo ni upungufu wa walimu wanaofundisha Skuli za kwani bado hawakidhi mahitaji.

 

Aidha alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo hulazimika kuwatumia walimu wa Sekondari ili kuongeza nguvu na kuwajengea uwezo mkubwa watoto.

 

“Tunawaomba wazazi kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza sekta ya elimu na kuwataka kutoa michango yao pale inapohitakaji,”alisema Khamis.

 

Kwa upande wa walimu aliwataka kufanya kazi kwa bidii kwani Serikali yao iko pamoja na nao.