NA ABDI SULEIMAN.
JUMLA ya wanafunzi 412 kutoa skuli sita katika Wilaya ya Wete na Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamefikiwa na Jumuiya ya Kuwezesha Vipaji vya Vijana Pemba (YETA), kwa ajili ya kupatiwa elimu juu ya kuepuka migogoro na udhalilishaji katika kipindi cha uchumaji wa zao la Karafuu.
Wanafunzi hao waliopatiwa elimu na Jumuiya hiyo ni kutoka skuli za Sekondari Kinyasini, IstiQaama, Mgogoni, Konde, Mabatini na Gando.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, Msaidizi afisa mradi wa kujenga uelewa kwa vijana, katika kuzuia migogoro ya ukatili kipindi cha mavuno ya zao la karafuu Pemba, Omar Abrahman Suleiman, alisema YETA imeona kipindi cha uchumaji wa karafuu matukio mengi hujitokeza kwa jamii ndio wakaamua kutoa elimu hiyo maskulini.
Alisema elimu inapofikishwa kwa wanafunzi ni rahisi kufikia jamii kubwa kwa haraka, kwani wanafuzi huaminiwa na vijana wenzao.
“Wnafunzi wengi hujishirikisha katika masuala ya uchumaji wa karafuu, elimu hii imekuja wakati muwafaka hata matendo haya maovu vijana wakike ndio waathirika wakubwa”alisema.
Hata hivyo Mratib huyo aliwataka wanafunzi na walimu wa skuli hizo, kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika jamii zao ili kuona mavuno ya karafuu yanaendelea kufanyika bila migogoro na matendo ya udhalilishaji.
Akiwasilisha mada juu ya Migogoro kipindi cha uchumaji wa zao la karafuu, Dk.Ali Yussuf Ali alisema jambo linakemewa ni ni vitendo vya udhalilishaji katika kipindi cha uchumaji wa zao la karafuu.
Alisema dunia imebadilika sasa vitendo vingi vimekuwa vikifanyika na waathirika wakubwa ni vijana, hivyo aliwasihi wanafauzi kuendelea kushuhulikia masomo yao na sio mambo mengine.
“Kila mtu anapokuwa skuli lazima anakuwa na malengo yake, sasa nyinyi munapaswa kujuwa malengo yenu na sio kujiingiza katika masuala ambayo sasa hivi muda wake hayajafikia”alisema.
Naye Mwenzeshaji Ashrak Hamad Ali, aliwataka wanafunzi kuzingatia masomo yao kwani changamoto nyingi wanakutana nazo katika kipidni hiki.
Alisema matarajio ni kupungua kwa vitendo vya udhalilishaji kwa wasichana na watoto katika kipindi cha mavuno ya karafuu, kupungua kwa migogoro ya kifamilia inayotokana na zao la karafuu, vijana kusaidia uhamasishaji wa amani ya jamii zao.
“Sote tunajua kipindi cha uchumaji wa zao la karafuu migogoro mingi, hutokea na kupelekea uvunjifu wa amani baina ya mtu na mtu, familia na familia jambo ambalo halifai kutokea”alisema.
Alisema elimu kwa sasa ndio kilakitu hivyo wanapaswa kuachana na kupokea pokea vizawadi, kwa mtu yoyote kwani zawadi hizo zinaweza kuwasababishia majanga baadae.
Elimu hiyo imetolewa na Jumuiya ya YETA Pemba, kupitia utekelezaji wa mradi wa dumisha amani Zanzibar, wakishirikiana na Foundation for civil society na Search for common groud, kwa ufadhili wa umoja wa nchi za ulaya.