Sunday, November 24

Utalii visiwa vidogo vidogo utakavyoimarisha uchumi wa wananchi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

SERIKALI ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussen Ali Mwinyi imelichukua suala la uwekezaji wa visiwa vidogo vidogo Zanzibar katika hatua nyengine ambayo ni nzuri na yenye manufaa kwa nchi.

Agosti hadi Septemba mwaka 2021, Serikali ilitangaza awamu ya kwanza ya uwekezaji, ambapo visiwa vinane (8) vilipata wawekezaji kati ya kumi (10) vilivyotangazwa.

Visiwa hivyo ni Changuu, Pwani, Bawe, Pamunda A na B, Kwale, Chumbe, Misali, Njau na Matumbini A, ambapo kisiwa cha Njau na Matumbini A wawekezaji walishindwa masharti.

Serikali imeweka vigezo maalumu kwa wawekezaji wa visiwa na ikiwa hakufikia, hatopatiwa kwani Serikali iko makini kwenye suala hilo.

Anasema Mkurugenzi Uwekezaji Pemba Al-haji Mtumwa Jecha, awamu ya pili ilitangazwa mwaka huu, ambapo kwa Pemba ni kisiwa cha Matumbini, Jombe na Kwata Kusini na Kashani, Njau na Fundo Kaskazini.

Visiwa hivyo vitakodishwa muda mrefu ili vijengwe hoteli za kitalii zitakazotoa huduma mbali mbali na utakuwa uwekezaji mkubwa utakaoipatia Serikali mapato na kuwanufaisha wananchi wake.

Hiyo ni njia bora ya kuimarisha Utalii kwa sababu itakuwa ni miradi mikubwa na endelevu, hivyo Serikali imeamua kukodisha kama zinavyofanya nchi nyengine ikiwemo Morishias.

Dk. Hussein Mwinyi alitaja miongoni mwa masharti yaliyowekwa kwa muwekezaji ni kuilipa Serikali kwanza kabla hajaanza ujenzi wa mradi wake na aeleze ataweka mradi gani na wenye ukubwa kiasi gani, ili Serikali ijiridhishe kuwa mradi husika hautaharibu mazingira na uwe mkubwa.

Makala haya inaelezea jinsi gani miradi ya kitalii katika visiwa vidogo vidogo Pemba, inaweza kuimarisha maisha ya watu…

Ukodishwaji huo utasaidia maendeleo ya Zanzibar, kwani fedha ziakazopatikana zinatumika katika huduma za kijamii pamoja na kuzalisha ajira kwa wazawa.

Suala la Ajira

Ali Hamad Ali (40) wa Kitambuu Wete anasema, ipo haja kwa wazazi kuelekeza watoto wao mambo ya kitalii, ili mradi ukianza vijana wapate ajira.

“Ni watu watakavyojipanga tu, lakini ikiwa hawatajipanga mapema, watakuja watu wa nchi nyengine, kuchukua nafasi hizo na baadae tubaki kulalamika”, anafahamisha.

Anaeleza, ukodishwaji wa visiwa ni muhimu sana kwani itaimarisha maisha yao kwa namna tofauti kutokana na kutakuwepo huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji safi na salama, umeme, afya na barabara.

“Wataajiriwa katika hoteli hizo na kujiajiri wenyewe kwa kuuza bidhaa mbali mbali na kutembeza watalii”, anafahamisha Kauthar Abeid Omar (20) wa Chasasa Wete.

Zuhura Mgeni Othman Afisa Mdhamini Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba anaeleza, wajamii waliopo ndani na nje ya visiwa hivyo watafaidika na ajira.

“Mwekezaji atahitaji rasilimali kutoka kwa wanajamii ili kuweza kufanyakazi, kuna rasilimali watu na pia vitu wanaozalisha vitahitajiwa na wawekezaji, hivyo watajiajiri”, anaeleza.

Upatikanaji wa masoko ya bidhaa

Hadia Hamad Shehe (35) mkaazi wa Micheweni anaeleza, Serikali na taasisi binafsi zinaimarisha vikundi vya wanawake na vijana katika shughuli za ujasiriamali, ingawa wanakosa soko la uhakika.

Anasema, uwekezaji huo utasaidia upatikaji wa soko la uhakika, kwani watalii watakuja kwa wingi kutembea katika visiwa hivyo.

“Wavuvi wanapewa boti lakini hawana sehemu ya kuuzia samaki wao, lakini zitakapojengwa hoteli za kitalii watauza huko, wajasiriamali watauza mikoba, mboga, matunda na bidhaa nyengine”, anaeleza

Mkaazi wa Jadida Wete Halima Mzee Khamis (27) anasema, miradi hiyo itaimarisha kipato cha wananchi na uchumi utakuwa zaidi.

“Uwekezaji huu unaweza kuipa nchi umaarufu kutokana na watalii wanaoingia, wataitangaza na kuongeza urafiki na mataifa makubwa ambayo yataweza kutoa misaada ya moja kwa moja”, anaeleza.

“Hapa wazawa watapata fursa ya kuuza bidhaa tofauti, ikiwemo za vyakula, mikoba, mafuta na dawa zinazotengenezewa karafuu, mkaratusi, mwani”, anafahamisha Mohamed Khamis Shehe (44) wa Uweleni Mkoani.

Khamis Ali Juma Mratibu wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba anaeleza, mwekezaji hawezi kuimarika kwenye shughuli zake ikiwa hakuwategemea wajasiriamali, kwani wageni watakaofika lazima watahitaji vitu.

“Wajasiriamali watapata tija na manufaa kwa sababu kuna wanaolima bidhaa tofauti, pia wavuvi watauza samaki kwa wawekezaji hao”, anaeleza.

“Wananchi wawe makini na hili, kwa mfano mwekezaji anahitaji tani moja ya tungule kila siku, ikiwa wananchi watajikubalisha kulima, kutakuwa na soko la kudumu”, anaeleza Mkuu wa Wilaya ya Wete dk. Hamad Omar Bakar.

Mjasiriamali wa ushonaji wa makawa ya kindu nzima, Khadija Sleyum (47) mkaazi wa Tumbe anasema, watanufaika sana kwani watalii wataingia kwa wingi na watanunua bidhaa zao kwa vile ni za kipekee.

“Makawa, vipepeo na mikoba tunayotengeza inawavutia sana watalii na ni mambo ya utamaduni, hivyo soko litakuwa na sisi tujikwamua kiuchumi”, anasema Khadija.

Fat-hiya Mussa Said Mratibu wa TAMWA Pemba anaelezea, watalii wanapoongezeka nchini na wajasiriamali wataongeza soko la bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

“Mtalii anapoona bidhaa ni nzuri, anaweza kununua na kusafirisha kwenye nchi yao, hivyo soko la wajasiriamali litaimarika na wananchi watanufaika kwa ujumla”, anasema.

Haji Khamis Haji Mratibu Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Pemba watahakikisha wajasiriamali wanakidhi vigezo vya kupata mikopo ili waongeze mtaji utakaowasaidia kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora.

“Mikopo itawasaidia kuzalisha bidhaa nyingi, hivyo wawekezaji watazipata za kutosha, hii itawainua sana wajasiriamali wetu”, analeza.

Utunzaji na Uhifadhi wa mazingira

Mkurugezi wa Uwekezaji Pemba Al-haji Mtumwa anasema, kati ya masharti yaliyowekwa kwa muwekezaji ni lazima aielezee Serikali namna gani atazingatia uhifadhi wa mazingira.

“Mchakato mzima wa ukodishwaji tunashirikiana na wadau wa taasisi mbali mbali ikiwemo ya mazingira (ZEMA) katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa hali ya juu”, anafahamisha.

Anafafanua kuwa, Serikali na wananchi hawatokuwa radhi baadha ya miaka kadhaa kupotea viumbe vya baharini ikiwemo matumbawe, hivyo watakuwa makini katika suala uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Mkuu wilaya ya Wete dk. Hamad Omar Bakar anasema, ikiwa kuna mazingira hayako sawa katika maeneo yao, wasaidie upatikanaji wa uhifadhi wa mazingira na faida hizo ziwafike wananchi, ili wajisikie kwamba uwepo wa utalii hauko katika mazingira ya kuwaathiri.

Fatma Hassan Kombo (38) wa Msingini Chake Chake anaeleza, ili utalii uwe nzuri ni lazima mazingira ya karibu yawe mazuri, hivyo wawekezaji watalinda mazingira yanayowazunguka ili waendelee kuwa na soko la muda mrefu.

“Ili kuendelea kuvutia wawekezaji wetu hatuna budi kuisaidia Serikali kuyatunza mazingira yetu, ili yawavutie watalii wanaoingia”, anasema mkaazi wa kisiwa cha Fundo Khamis Faki Mjaka (47).

Ali Juma (32) wa Chake Chake wanashuhudia visiwa vyote kuwa vichafu, hiyo ni kwa sababu wananchi wanashindwa kutunza mazingira, lakini watakapokuwepo wawekezaji itakuwa ndio mwarubaini wake.

“Itasaidia usafi wa mazingira ya visiwa vyetu kwa sababu mwekezaji atalazimika kuboresha na kutunza mazingira ili aweze kufikia malengo yake”, anafafanua kijana huyo.

Alitolea mfano kisiwa cha Chumbe Unguja na Misali Pemba jinsi wawekezaji hao wanavyojitahidi kuyaweka mazingira ya visiwa hivyo katika hali ya usafi.

Fat-hiya Mussa Said anasema, utalii wa sasa ni wa kutunza mazingira, kitu ambacho wanatakiwa wawarithishe watoto wao, ili mabadiliko ya Tabianchi yasiathiriwe.

“Tunapohifadhi mazingira tunasaidia kuendeleza ule uhalisia wa visiwa vyetu ili visipotee na kuufanya utunzaji huo, uwe ni endelevu”, anaeleza.

Wawekezaji wanakuwa na majukumu yao, hivyo watawaongoza wananchi katika suala zima la uhifadhi wa mazingira, ili waendelee kufaidika na uwekezaji huo.

Jinsi inavyoweza kuwasaidia watu wa karibu

Wananchi wa karibu watafaidika zaidi na utalii huo visiwani mwao katika masuala ya ajira na kwenda kuuza bidhaa zao pamoja na kuongeza mashirikiano baina ya wao na wawekezaji.

“Watu wa karibu ni wa mwanzo kunufaika katika Nyanja mbali mbali, kuongeza mashirikiano katika kuchangia maendeleo kwenye visiwa hivyo, ikiwa ni pamoja na kupata huduma za kijamii”, anasema Asha Ali Khamis (30) wa Kipangani Wete.

Faida Suleiman Ali (36) wa kisiwa cha Njau Wete anaeleza, uwekezaji huo utawasadia kunyanyua kipato chao, kwani watakuwa wanafanya biashara na kuuza kwenye hoteli”, anasema.

Fadhila Haji Makame (39) mkaazi wa Makombeni Mkoani anaeleza, utasaidia kunawirisha maisha ya wakaazi wa visiwa hivyo kwa kupata mahitaji yao ya lazima ikiwemo chakula.

Al-haji Mtumwa Mkurugezi Uwekezaji anasema, wananchi wa visiwa hivyo na maeneo ya karibu watanufaika kuanzia hatua ya ujenzi utakapoanza, kwani watapata ajira na kujiajiri wenyewe kwa kuuza biashara zao.

Moja ya kigezo cha maombi ya mwekezaji ni kuhakikisha namna gani watawashirikisha wananchi waliopo katika visiwa hivyo na maeneo ya karibu na ikiwa hakueleza hayo, hatopatiwa visiwa hivyo.

Anawataka wananchi waelewe kwamba, visiwa hivyo haviuzwi na vinakodishwa kwa maslahi ya Taifa, kwani kuna faida nyingi zitapatikana.

“Visiwa vitapata kutunzwa, wawekezaji wanakuja na fedha nyingi ambapo wanapojenga wanahitaji vibarua, wanaajiri wananchi na pia baadhi ya vitu watanunua kwetu, hivyo kutakuwa na mzunguko wa biashara kati ya mwekezaji na wananchi”, anafahamisha.

Anataja zaidi ya dola milioni 200 zimepangwa kuekezwa katika visiwa vile vya awali, ambapo kwa Pemba ni Misali, hivyo fedha zitakazopatikana zitasaidia kuimarisha nchi.

Uimarishaji wa miundombinu

Mkurugeni huyo anaeleza, watatumia miundombinu tofauti kufikia visiwa hivyo ikiwa ni pamoja na kujenga bandari ndogo ndogo na pia kutakuwa na matumizi ya herikopta.

“Tumechelewa kidogo katika uwekezaji huu, hivyo hata kama muwekezaji atajenga bandari tutamruhusu kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi”, anafafanua.

Kwa upande wa maji na umeme, mamlaka hizo zitashirikiana kikamilifu na wawekezaji katika kuhakikisha huduma hizo zinafika katika visiwa vilivvyokodishwa.

Afisa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja kutoka ZECO Pemba Haji Khatib Haji anasema, wamejipanga kufikisha huduma ya umeme katika visiwa vyote, ambapo visiwa kama Fundo, Kisiwa Panza, Makoongwe, Kojani tayari vimeshapata huduma hiyo na sasa watafikisha umeme kisiwa cha Njau na Kokota kwa kutumia umeme wa nguvu za jua.

Suleiman Anas Massoud ambae ni Afisa Uhusiano ZAWA Pemba anasema hawawezi kuchimba visima kwenye visiwa kutokana na maji chumvi ingawa wana utaratibu ulazaji wa bomba mpaka kwenye kisiwa wenyewe.

“Siku zote uwekezaji huwa ni mkubwa hivyo, tunaweza kuchangaza visima katika kuwapelekea maji ama tukaachimbia vyao, siku hizi kuna teknologia ya kuyabadilisha maji ya bahari kuwa maji ya kawaida lakini ni gharama kubwa”, anasema.

Upatikanaji wa kodi kwa Serikali

Anasema Mkurugenzi Al-haji kuwa, kama ilivyo kawaida ya kulipia kodi nyumba, vivyo hivyo kwenye visiwa, wawekezaji watalipa kodi kila mwaka.

Mwananchi Khairat Khamis Saleh (27) wa Gombani Chake Chake anasema, ukodishwaji huo utaongeza pato la Serikali kwani watakaokodishwa watalipa kodi na tozo mbali mbali zitakazoisaidia Serikali kupata mapato yake.

“Wenye hizi hoteli watalipa pesa nyingi tena za kigeni, hivyo hata uingiaji wa pesa za kigeni utaongezeka na kusababisha kuikuza thamani ya shilingi ya Tanzania”, anasema.

Mdhamini Utalii na Mambo ya Kale anasema, kwa vile watawekeza ni lazima watavutia wageni na watakapokuja watanufaisha Serikali kwani watalipia namna mbali mbali, hivyo kodi ya Serikali itaongezeka.

“Tutapata kodi kutokana na uwekezaji utakaokuwepo kwenye visiwa vyetu na nchi itaongeza mapato yake kwani wawekezaji wana uwezo mkubwa”, anasema Jamal Hassan Jamal Mkuu wa Utawala ZRB Pemba.

Nini kifanyike ili kuimarisha zaidi utalii na maisha ya wananchi.

Anasema Khadija Shehe (55) mkaazi wa Tumbe Mashariki, wananchi wasijilemaze zinapokuja fursa na wazitumie kwa lengo la kuwanufaisha.

Salma Hamad Ali (49) Shengejuu Wete, anasema ipo haja wananchi waunge mkono juhudi za Serikali kuhakikisha nchi inapata maendeleo kila kona, kwani uwekezaji ni dhana pana ya kiuchumi.

Salim Said Salim Mkurugezi Dhamana Taasisi ya Viwango Pemba (ZBS) anawataka wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitawapatia alama ya ubora, ili watalii wanunue kwa haraka.

“Alama ya Ubora ni muhimu sana katika bidhaa tunazozalisha, kwani wageni wakiziona itakuwa hawana wasiwasi wa kutumia, hivyo wazingatie vigezo vyote vinavyotakiwa”, anafahamisha.

Hamad Amini Ali Mdhamini Kamisheni ya Utalii Pemba anawataka wananchi waukubali utalii kuwa ni biashara na ni ajira, kwa hiyo waendelee kufaidika kwa kufanya yale ambayo yatawaletea manufaa.

Dk. Mwinyi katika hotuba yake anasema, juhudi za Serikali zimewawezesha kuongeza idadi ya watalii kutoka 260,644 mwaka 2020 hadi kufikia 393,512 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 50.97 pamoja na idadi ya Kampuni za Ndege zinazofanya safari za kuja Zanzibar kutoka 27 hadi 34, Ndege hizo zilizoongezeka zinakadiriwa kuleta zaidi ya watalii 50,000 kwa mwaka.