Saturday, January 4

SIKU SABA NGUMU ZA BINT MTANZANIA ALIYETOROKA VITA UKRAINE

Nenyorata Teveli

CHANZO CHA PICHA,NENYORATA TEVELI

Nikama filamu vile, lakini si filamu hii ni simulizi ya kweli inayomuhusu binti wa kitanzania mwenye umri wa miaka 23 aliyetumia siku saba kutoroka mapigano Ukraine.

Wiki moja na nusu iliyopita ungemwambia binti huyu kwamba, leo angekuwa anasimulia masahibu yaliyomkuta pengine angekukatalia. Lakini mambo hubadilika haraka.

Nenyorata Teveli ameishi nchini Ukrane kwa takriban miaka minne sasa. Alikwenda huko kusomea masomo ya udaktari tangu mwaka 2017 akiwa na miaka 18 pekee. Miaka yote hiyo aliyoishi huko hali ilikuwa shwari na aliendelea kupiga msuli ‘kusoma kwa bidii’ ili kutimiza ndoto zake za kuwa Daktari.

Lakini ndoto zake zikakutana na ‘giza’ la risasi na mashambulio ya Urusi yanayoendelea huko Ukraine. Mzozo wa Ukraine unamfanya kila aliyeko huko hasa raia kutoka maita mbalimbali watafute njia za kujiokoa.

Teveli na yeye alijiapiza kujiokoa na siku chache zilizopita akaanza safari ya kuikimbia nchi hiyo.

Safari yake ya kujiokoa na kutoroka Ukraine

Kama ilivyo kwa wanafunzi wengie, muda wa kupumzika huwa Hostel, Taveli na yeye alikuwa Hostel. Anakatishwa usingizi na mlio mkubwa wenye kishindo. Harakaharaka hakujua nini, alipochungulia nje aliona moshi mkubwa na moto ukiwaka katika moja ya maeneo jirani na alikokuwa anaishi. Ilikuwa siku ya kwanza ya mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine, februari 24 mwaka huu.

Anasema milio hiyo yenye kishindo yalikuwa ni mabomu yaliyopigwa kwa takriban dakika 15 mfulilizo. Akiwa mtanzania pekee katika makazi alipokua anaishi na wanafunzi wenzie, wote hawakujua cha kufanya muda huo.

Akalazimika kutoka kitandani kujua nini kinaendelea, Nenyoratha aliona wanafunzi wenzie raia wa Ukrane wakibeba mabegi na kukimbia, wanasema wanaenda kutafuta hifadhi katika miji ya jirani kwani mji wao Kharkiv unashambuliwa na mabomu.

Anasema tahadhari zilianza kutolewa na watu wote kuambiwa watafute hifadhi katika mahandaki. Kwa mujibu wa Nenyoratha nyumba nyingi nchini Ukrane zina mahandaki na hata baadhi ya hosteli zilikua na mahandaki lakini bahati mbaya katika hosteli aliyokuwepo hakukuwa na handaki.

Kwa haraka ilimbidi atawapigie watanzania wenzie kwa njia ya simu angalau kupata haueni ya nini cha kufanya , na kukubaliana kwenye kituo cha karibu cha treni cha chini ya ardhi.

Walianza kutembea kwa woga kwa mafungu akiambatana na wanzania wengine wakiwa hawajui picha halisi ya nini kinaendelea. Katika msafara huo waliongozana na watu wengine wengi kwenda katika hifadhi hiyo wakiamini Kesho hali itakuwa sawa tu.

Nenyorata Teveli

CHANZO CHA PICHA,NENYORATA TEVELI

Chakula, pesa na huduma nyingine muhimu

Wakiwa njiani kwenda kwenye kituo cha treni kujificha kukwepa mabomu kwa woga wa kifo, njiani waliona watu wakikimbilia kwenye maduka kununa vyakula kwa wingi , wengine wakitoa pesa katika mashine za kutolea pesa (ATM).

Na yeye aliona vyema atoe akiba yake ya fedha imsaidie mbele ya safari, akatumia masaa mawili kuifikia ATM aliyohitaji kuitumia na akatumia masaa mawili mengine kwenye foleni, iliyo kuwa ndefu kwa msururu wa watu waliokuwa na woga. Pamoja na kusubiri muda huo kwenye foleni hakufanikiwa kupata fedha.

Muda ulizidi kwenda mpaka kufika kwenye kitup cha treni. Licha ya kufika akili yake ilikuwa ni kupata pesa, bila hivyo asingejua namna gani angeishi. Jioni akalazimika kutoka tena kwenda kwenye ATM na kupata kiwango kidogo cha pesa kama dola 100 sawa na shilingi za kitanzania skama laki mbili.

Kwa ujasiri alikimbia na kukusanya maji na vyakula vikavu ambavyo haviwezi kuharibika na kukimbia kwenye handaki.

Unapokuwa kwenye wakati mgumu, kuzungumza na watu wako wa karibu huleta faraja. Kwa siku mbili mfululizo, Taveli alijificha kwenye handaki na wenzie, lililokuwa na hali ya kawaida tu na huduma za kawaida.

Akatumia muda huo, kuwapigia wazazi wake kwa ushauri na faraja. Akiwa na wenzie watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya mji waliokuwepo, walikutana kwenye kikao chini ya handaki na kukubaliana kupanga mbinu ya kutoroka Kharkiv kuelekea mji wa lviv mji ambao upo karibu na mpaka wa kuelekea Poland.

Pamoja na kukubaliana na uamuzi wa kuondoka alikuwa na woga na hofu kubwa ingawa alikuwa na matumaini ya kufika nyumbani Tanzania.

Safari ya kutoroka Kharkiv kwenda mji wa lviv

Haikuwa rahisi kutoka hapo mosi walikuwa raia wengi wa mataifa mengine, hivyo kuingia kwenye usafiri wa treni ilikuwa ni kwa kugombea. Ili kufanikiwa ilibidi yeye na baadhi walazimike kuacha mizogo yao. Alifanikiwa kuingia kwenye treni hiyo ilijaa sana

lakini aliona baadhi ya watanzania wenzie na raia wengine wengi walivyokosa nafasi ya kuingia kwenye treni hiyo.

Ilikua ni safari ya saa ishirini na nne treni Nenyorata alikua ni miongoni mwa wengi waliokuwa wamesimama kwa siku nzima na kwa safari nzima kutokana na kukosa nafasi Lviv.

Licha ya kubanwa na hajam, ilikuwa ngumu kwenda chooni kutokana na mrundikano wa watu. Nenyo anasema kwa masaa hayo 24 ndani ya treni hakuweza kwenda chooni, hapakuwa na pakukanyaga, wamebanana na watu wengine wamekaa chini hivyo hakuna pa kupita.

Waliwasili Lviv majira ya saa kumi na moja jioni siku iliyofuata wakiwa hoi wamechoka lakini wakishukuru walau wamefika mji wa Ukrane ambao haujapigwa mabomu. Walikuta ndani ya kituo cha treni kumejaa idadi kubwa ya watu na hata nje pia kumefurika.

Baridi lilikuwa kali kiasi cha barafu kunaendelea kuanguka. Nenyo hakujali hali hiyo, ilikuwa ni faraja kwake alijiona yuko salama.

Angalau muda huo waliweza kupata chakula. Huku mamlaka zikichukua taarifa za kila mmoja waliofika kwenye eneo hilo la kituo cha treni katika mji wa lviv.

Usiku ulipoingia zaidi, walilazimika kulala uwanjani, kwenye uwanja wa mpira wa kikapu. Wakitumia matandiko duni waliopoewa na mamlaka.

Siku iliyofuata waliamka mapema na kuanza safari kuelekea kwenye mpaka wa Ukrane na Poland. Ilikua ni majira ya saa tano na nusu asubuhi waliingia kwenye gari kutoka Lviv kuelekea katika mpaka wa Poland na ukrane eneo linaloitwa krakovets.

Kufika Krakow ilikuwa ni kilomita 50, lakini gari waliopanda iliwasogeza kilomita 20 tu.

Nenyorata Teveli

CHANZO CHA PICHA,NENYORATA TEVELI

Foleni kufika mpakani ilikuwa kubwa sana, gari za abiria zilikuwa zimejaa kupita kiasi. Nenyoratha na watanzania wenzake takriban ishirini waliungana na raia wengine wan chi mbali mbali walilazimika kutembea kwa mguu. Walitembea kwa takriban saa moja lakini bado walikuwa wanahitai kutembea kilomita 26 kufika katika kituo cha mpaka huo. Wakazi vijiji vya jirani waliwapa lifti kuwasogeza Kijiji kinachofwata walipo washusha waligeuza kurudi vijijini kwao. Ulikuwa ni msaada mkubwa kwao kwani walipata kupumzika kwa dakika chache kabda ya kuanza kutembea tena.

Walitembea mpaka walipopata lifti nyingine wakafika kwenye kituo kimoja ambapo wanakijiji walikuwa wameandaa chakula na maji kwaajili ya watu ambao hawana chakula na wanapita kuelekea mpakani.

“Kila mwana Kijiji ameleta chakula hapo, hawa niwatu ambao nchi yao ipo vitani hawajui Kesho itakuwaje ila walitujali na kutupa chakula chao bure” Nenyoratha

Nenyoratha na watanzania wennzie waliendelea kutembea kwa mguu ili kuwasili mpakani.

Giza linaingia, wanaona mwanga wa magari na taa kwa mbali. Hawajui wamebakiza kilomita ngapi kufika mpakani. Kwani tayari walikuwa wametembea kwa mguu kwa takriban masaa sita (6). Walipokuwa katika kijiji kimoja, waliambiwa zimebaki kilomita tatu tu, ila wanatembea wanaona hawafiki.

Mwishowe ikiwa ni usiku kiza kimetanda walifanikiwa kuingia katika kituo cha mpaka wa Ukrane na Poland. Hapa walihitaji kupata muhuri wa kutoka Ukrane, lakini iliwabidi wasubiri sana kwani magari yalipewa kipaumbele kuliko watu waliokuwa wakitembea kwa mguu. Walipanga foleni kwa muda mrefu sana mpaka kundi lao lilipoitwa wakapata fursa ya kugongewa muhuri na kuingia poland.

Ilikuwaje walipowasili Poland?

Nenyoratha anasema walipokelewa vyema walipoingia upande wa Poland mpakani.Wanawake na watoto hawakupanga mstari. Hivyo walipanga mstari wakapigiwa tena muhuri wa kuingia Poland. Na hapo walipewa siku 53 za kukaa poland na waliruhusu wakimbizi wote kuingia katika nchi hiyo bila viza.

Moja kwa moja walichukuliwa na kupelekwa katika kambi ya wakimbizi iliyoandaliwa jirani na mpaka na walikuta watu wa maendeo mbalimbali wakipewa malazi na chakula endapo hawana mtu wa kuja kuwachukua hapo. Na kambi ilikuwa inatoa usafiri wa bure kwa wale wote wanao taka kwenda katika miji mingine ya Poland.

Kwa bahati nzuri mwakilishi wa serikali ya Tanzania aliwasili mapema na kuwachukua Nenyoratha na wenzie. Hapo walipelekwa kupanda treni na walipanda bure bila kulipa pesa yoyote kwani serikali ya poland iliidhinisha usafiri wa uma kutolewa bure kwa wakimbizi wote. Na hapo ndipo walipo tengana tena na baadhi ya watanzania wenzie. Baadhi walienda Lublin na wengine walienda Warsaw mji mkuu wa Poland.

Nenyorata Teveli

CHANZO CHA PICHA,NENYORATA TEVELI

Nini Kauli ya Nenyorata sasa na anaendeleaje?

“Mimi sijambo dada Lulu ni uchovu tu, naendelea vizuri ila ningependa kuishukuru sana serikali yetu ya Tanzania kupitia ubalozi wake wa Berlin na Sweden kwa kutushika mkono. Pia kijana Innocent aliyetupokea watanzania kutoka mpakani krakovets-przemysl na kuwa mwenyeji wetu kwa upande wa poland. Bila yeye ingekuwa vigumu ku kwani binafsi nilikua sijui hata pakuanzia katika nchi hii yakigeni. Na mwisho kabisa kuwashukuru ndugu, jamaa na marafiki na watanzania wenzetu wanaotujulia hali na kuwa pamoja nasi katika kila dakika ya hii safari” amezungumza Nenyoratha

1.Kutafuta namna ya kuwatoa wanafunzi wenzetu zaidi ya 200 walio Sumy. Maana hawana namna ya kutoka katika mji wao. Na mji wao upo karibu na border ya Urusi.

2.Utaratibu wa kupokelewa mpakani kwa wale ambao hawajafika mpakani bado. Je wapite mpaka upi ambao hauna foleni na hawata kutana na ubaguzi.

3.Kwa walioweza vuka mpaka tunaomba serikali iweke utaratibu maalumu ya kuwapokea (chakula na malazi). Pesa za huku ziko juu kuliko za Tanzania na sio kila mzazi anaweza mudu hizo gharama. Kuna wengine wameletwa na wafadhili na wao wanalipia ada tu. Hivyo serikali ikiweka utaratibu maalumu utawasaidia sana watanzania ambao hawawezi kumudu hizi gharama za ghafla.

Hayo ni maoni na mawazo ya binti huyu ambaye kichwani kwake bado anawafikiria wenzake waliosalia Ukrane. Na hii leo mji wa Kyviv tayari umeshambuliwa kwa mabomu. Mashahidi wanasema ilisikika milipuko minne mikubwa majira ya asubuhi.

Mungu awatangulie watanzania wote na waafrika wote wanaohangaika safarini kurejea makwao. Na iwe shwari kwa watu wote waliopo Ukrane.

CHANZO CHA HABAFRI BBC SWAHILI.