NA ABDI SULEIMAN.
KAMISHENI ya Ardhi Pemba, imesema moja ya faida ya uhaulishaji wa ardhi kisheria kupitia bodi ya uhaulishaji ardhi, ni kuepukana na utapeli wa uzaji wa ardhi zaidi ya mara moja ambayo hupelekea kutokea kwa migogoro mara nyingi.
Hayo yameelezwa na Naibu Mrajis wa Ardhi Pemba Asha Suleiman Said, wakati alipokua akiwasilisha mada Sheria na taratibu za ardhi katika utatuzi wa migogoro, mkutano uliowashirikisha masheha na baadhi ya wananchi wa Micheweni na kufanyika ukumbi wa mikutano Micheweni.
Alisema wananchi wanapata faida nyingi sana wanapohaulisha ardhi zao kisheria, ikiwemo kuepuka na migogoro isiyo ya lazima, kujua mipaka yake halisi pamoja na ardhi yake kuwa iko mikono salama muda wote.
Naibu Mrajis huyo alisema changamoto kubwa hivi sasa ni migogoro ya ardhi isiyomalizika, huku ardhi ikiendelea kuwa muhimu sana duniani kote.
“Moja ya sababu inayopelekea kutokea kwa changamoto ni kuwepo kwa migogoro, inayotokana na kutokujuwa utaratibu wa kupata hati miliki ya ardhi”alisema.
Akizungumzia migogoro ya ardhi alisema wananchi wengi kutokujua taratibu za uhaulishaji wa ardhi, ardhi ya zanzibar kutokua na vikuta halisi, badala yake wananchi kuendelea kutumia vikuta vya kijadi.
Naye afisa usajili wa Ardhi Pemba Yussuf Hamad Kombo, alisema katika mauziano ya ardhi ni bora kutumika kwa bodi ya uhaulishaji wa ardhi, ili kuepusha migogoro ya ardhi na vizuri kwa mununuzi kutokulipa pesa mwanzo.
Hata hivyo alisema faida ya usajili wa ardhi serikali inakuwa ndio dhamana wa ardhi hiyo, huku akiwataka wananchi kufuata taratibu za kisheria.
Wakichangia katika mkutano huo Mariyam Said Juma, alisema elimu bado inahitajika vijijini, kwani wananchi wanauziana kiholela kila kitu bila ya kufuata taratibu zozote zile.
“Ukweli tuseme bado jamii imekua ngumu kufika bodi ya uhaulishaji wa ardhi, wanapotaka kuhaulisha ardhi zao kama elimu itafika basi mialama yote yatafuata sheria”alisema.
Naye Faki Kombo Hamad sheha wa shehia ya Mjenzi Micheweni, alisema migogoro ya ardhi imo na inaweza kutokea muda wowote, kwani unaweza kukuta shamba linauzwa kwa zaidi ya watu watatu.
Mapema mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, alisema maeneo mengi migogoro ya ardhi imekua ni mtambuka, kesi nyingi zimekua zikijitokeza mashamba au ardhi kuuziwa kwa watu zaidi ya watatu kwa kitu kimoja.
Alisema sasa ili kupunguza kwa migogoro sheria zilizopo zinapaswa kufuatwa kikamilifu, huku akiwataka watendaji wa kamisheni ya ardhi kusimamia ipasavyo sheria hizo, sambamba na wananchi kuelewa nyaraka za ardhi ni muhimu katika masuala ya ardhi.
Kwa upande wake mratib wa kamisheni ya ardhi Pemba Said Saleh Makame, alisema faida ya kusajili ardhi kisheria inasaidia ardhi husika kuondokana na migogoro ya mara kwa mara na inakua salama muda wote.
MWISHO