Wanafunzi wa Nigeria, Ghana na Somalia ni miongoni mwa mamia ya raia wa kigeni waliokwama katika mji wa kaskazini-mashariki wa Sumy nchini Ukraine ambao umekuwa ukishikiliwa na majeshi ya Urusi kwa siku kadhaa.
Hakuna chakula sokoni, mashine za benki hazifanyi kazi na wanafunzi wanakunywa theluji iliyoyeyushwa baada ya kukosa maji.
Mwanafunzi wa Kihindi, Vipin Yadav, ambaye ni sehemu ya kundi lililokwama katika jiji hilo, anakadiria takriban wanafunzi 1,300 wa kigeni bado wamenaswa huko – ikiwa ni pamoja na watu kutoka Bangladesh, Pakistan na Uturuki.
Katika mahojiano kwa njia ya simu, Bw Yadav aliambia mwandishi wa BBC Danny Aeberhard kwamba hakuna chakula kwa muda wa siku nne hadi tano zilizopita.
Serikali za Nigeria na Ghana zimekuwa zikiwarudisha nyumbani raia wao wanaokimbia mzozo nchini Ukraine. Vikundi vya kwanza vilirudi nyumbani wiki iliyopita.
Zaidi ya wanafunzi 1,000 wa Ghana walikuwa wakiishi Ukraine hadi Urusi ilipovamia nchi hiyo. Taifa hilo la Afrika Magharibi hadi sasa limefanya misheni mbili za kuwarejesha makwao.
Nigeria inatarajiwa kuwahamisha raia 5,000 waliovuka kutoka Ukraine hadi nchi jirani za Romania, Poland na Hungary.