Saturday, March 15

Waziri Mkuya: Waandishi ibueni changamoto za watu wenye ulemavu.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Saada Mkuya Salim amewataka waandishi wa habari visiwani Zanzibar kuibua changamoto zinazowakwaza watu wenye ulemavu ili kuiwezesha Serikali kuziona, jambo ambalo litasaidia kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisema kuwa, watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinahitaji kutatuliwa, hivyo ni jukumu la waandishi kuziibua na kuzitangaza ili nao wapate haki zao zinazostahiki.
Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa siku mbili kwa waandishi wa habari katika Ukumbi wa Hoteli ya Maru Maru mjini Unguja.
“Kila mmoja kwa nafasi yake ana jukumu la kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapatiwa haki zao na nyinyi waandishi ni sauti ya wasio na sauti, hivyo tujitahidi kuwasemea wenzetu hawa”, alisema Waziri huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mradi Jumuishi wa Vyombo vya Habari Kanda ya Afrika kutoka Shirika la kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari Jackie Lidubwi aliwataka waandishi kuandika habari ambazo hazitowaumiza watu wenye ulemavu kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.
“Waandishi mnajitahidi kuandika habari nyingi lakini baadhi yenu mnawaumiza watu wenye ulemavu na sio kuwasaidia, hivyo muwe makini katika kuandika ili wapate haki zao stahiki”, alisema mkuu huyo.
Nae Mkuu wa program kutoka Internews Shaaban Maganga alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanawajengea uwezo, ujuzi na maarifa namna ya kuandika habari za watu wenye ulemavu kitaaluma zaidi, ili kuacha kuwaumiza watu hao.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Juma Salim Ali kutoka SHIJUWAZA  aliwasisitiza waandishi wa habari kuangalia uwezo wa watu wenye ulemavu wanapoandika habari zao, jinsi wanavyoweza kuchangia ujenzi wa taifa na sio kuandika madhaifu yao pekee.
Kwa upande wao waandishi wa habari walieleza kuwa, mafunzo hayo yatawajengea uwezo mkubwa katika kuandika na kuripoti habari za watu wenye ulemavu bila kuwakwaza.
“Kuna habari ambazo tunaandika kwa lengo la kuwasaidia kumbe tunawaumiza, tutajitahidi kuhakikisha tunafuata taratibu zinazotakiwa, ili kuona na wao wanapata haki zao zinazostahiki “, alisema.
Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Maru Maru mjini Unguja, ambapo mad mbali mbali ziliwasilishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika habari za watu wenye ulemavu wa weledi.