Thursday, January 16

ZANTEL YATOA ELIMU KWA WAFANYABIASHAR KUTUMIA MFUMO WA LIPA KWA SIMU

NA MGENI KOMBO.

WAFANYABIASHARA wametakiwa kutokuogopa kutumia huduma ya LIPA KWA SIMU, kwa sababu ya usalama wa fedha zao na uwekaji wa kumbukumbu za bishara.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Masoko Zantel Rukia Iddi Mtingwa, wakati alipokua akiitambulisha huduma hiyo kwa wafanyabiashara na mawalaka wa huduma ya EzyPesa Kisiwani Pemba.

Alisema wafanyabiashara wanapotumia huduma hiyo atakapoondoka jioni, hatolazimika kubeba fedha mkononi alizofanyia biashara kwenda kuweka benk, badala yake huzipata wakati muwafaka katika akounti yake ya biashara.

Aidha alisema faida nyengine kwa mfanyabiashara anayetumia huduma hiyo, atakapokwenda kutoa kwa mara ya kwanza hakutakua na mkato wa Kampuni na mikato mwengine yowote kwenye fedha zake.

“Huduma hii ni nzuri sana kwa wafanyabiashara, fedha zake zitakuwepo sehemu salama na ataondokana na kadhia ya kurikodi kitu kila anapouza, kumbukumbu zake zote atazipata kupitia miamala anayouza,”alisema.

Naye Meneja wa Mauzo na usambazaji Pemba Said Massoud Ali, alisema huduma ya LIPA KWA SIMU ni rahisi na wala haipotezi muda kwa wafanyabiashara wala mteja.

Alisema huduma hiyo pia inawezesha kulipia kwa kutumia mitandao yote na sio ZANTEL peke yake, pamoja na kutumia Application maalumu na kuscan QR Code.

Kwa upande wake Afisa wa EzyPesa Pemba Salama Mzee, alisema mfumo wa huduma hiyo tayari inatumiwa na watu zaidi yua 3000 kwa Zanzibar na zaidi ya 300 kwa Pemba.

Alisema huduma hiyo ya LIPA KWA SIMU inatumiwa kwa wafanyabiashara na watoa huduma, huku huduma EzyPesa inatumiwa na watu wote wanaotumia mtandao huo.

Akitoa ushuhuda juu ya matumizi ya huduma hiyo, mfanyabiashara Abdillah Ali Hamad kutoka Wete, alisema huduma hiyo mwanzo ilikuwa ikimpatia tabu wakati wa kutumia, lakini sasa ameona faida yake na kumuongezea idadi ya wateja.

Alisema huduma hiyo imemrahisishia kutumia miamala mingi zaidi ya simu, kwani watenja wake wanaona ni jambo la kawaida kwao kuliko kulipia pesa mkononi.

“Hivi sasa kuna wateja wanabaki majumbani na wanalipia na baadae anamtuma mtoto wake dukani na kuja kuchukua bidhaa zake alizolipia”alisema.

Naye mfanyabiashara Kassimu Kishuka ameiyomba Kampuni ya Zantel kutoa elimu kwa jamii juu ya utoaji wa huduma hiyo kwa simu kwani waliowengi hawana.

MWISHO