Thursday, January 16

TAASISI za Ifraji Zanzibar Foundation na Milele Zanzibar Foundation zawafariji wanafunzi Utaani.

 

NA ABDI SULEIMAN.

TAASISI ya Ifraji Zanzibar Foundation na Milele Zanzibar Foundation, zimekabidhi vifaa mbali mbali kwa wanafunzi wa skuli ya Sekondari Utaani vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 40.

Wanafunzi hao ambao bweni lao la kulalia lilipata mtihani wa kuungua moto wiki iliyopita, huku vitu vyao mbali mbali vikiteketea katika tukio hilo.

Akizungumza katika hafla ya kupokea msaada huo kwa wanafunzi 64 wa kidato cha sita kwa hatua ya kwanza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, alizishukuru taasisi hizo kwa kuwajali wanafunzi hao pamoja na kuguswa na tukio hilo.

Alisema taasisi hizo zimekuwa za kwanza kuwasaidia wanafunzi hao baada ya tukio lililotokea, kwani msaada huoumefika katika kipindi muwafaka ikizingatiwa mwaka huu wanafunzi hao wanafanya mitihani.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuona taasisi zinasaidia jamii, nilipokuwa wizara iliyopita matukio mengi yakitokea ila sikuona misaada, hii inadhirisha kuwa suala la elimu ni jambo muhimu na kila taasisi inaguswa na suala hilo”alisema.

Aidha aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanathamaini michangoa inayotolewa na wadau mbali mbali nchini, kwa kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alizipongeza taasisi hizo kwa kuwajali wanafunzi hao, huku wakitambua thamani ya elimu.

“Tunafahamu hii sio mara ya kwanza kwenu kujitokeza kusaidia huduma za kijamii, Milele na Ifraji mumekua taasisi za mfano, sasa ombo langu ni kuwaangalia kwa namna yoyote wanafunzi hao katika kipindi cha Ramadhani”alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya IFRAJI Zanzibar Foundation Pemba Abdalla Said Abdalla, alisema taasisi yake imeamua kuchangia shilingi Milioni 20 kwa ajili wanafunzi wa kidato cha sita kwa hatua ya kwanza.

Alisema vitu ambavyo wanafunzi 64 wa kidato cha sita watapatiwa ni Vita mbaa, kanga 128 kila mmoja kanga pea mbili, taula 64 kila mmoja taula moja, viatu pea 128 kila mwanafunzi pea mbili, magodoro 64, pamoja kalkuleta sayantifiki kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi kila mmoja moja na fedha taslimu shilingi elfu 70 kwa kila mwanafunzi.

Aidha Abdalla aliwataka wanafunzi hao kuzidisha juhudi katika masomo yao na kusahau kilicho tokea, ili kuweza kufanya vizuri katika masomo yao.

Naye mwakilishi kutoka bodi ya Milele Zanzibar Foundati, Ali Bakari Hamadai alisema milele pia inachangia shilingi Milioni 20, kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano hadi kidato cha kwanza skuli hiyo.

Alisema tukio lililotokea linahudhunisha wananchi wengi, jambo sio zuri na kwamba hakuna mtu aliyepata na ajali hiyo zaidi ya kuharibika kwa vifaa vyao.

MWISHO