Thursday, January 9

Profesa Mnyaa akabidhi matofali 25,000 kwa ajili ya msikiti na madrasa za Qurani jimboni kwake.

NA ABDI SULEIMAN.

WALIMU wa Skuli, walimu wa madraza za Qurani na wasimamizi wa miskiti iliyomo ndani ya jimbo la Mkoani Kisiwani Pemba, wamesema kukabidhiwa kwa matufali 25,000 na mbunge wa jimbo la Mkoni Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, yataweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika harakati zao za Ujenzi waliouwanza.

Walimu hao wamesema tayari harakati zao za ujenzi zilikuwa zimeshakwama, kutokana na kukosekana kwa matufali pamoja na vifaa vyengine.

Hayo waliyaeleza katika hafla ya kukabidhiwa matufali 25,000 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mkoani Kisiwani Pemba, kwa ajili ya kuendeleza na kumalizia ujenzi katika skuli mbali mbali, madrasa za Qurani na misikiti.

Mwalimu Omar Makame kutoka Madrasa Rahman iliyoko Jondeni Mkoani, alimshukuru mbunge wa jimbo la Mkoani Profesa Makame Mbarwa kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake alizozitoa kwa wananchi hao.

Alisema elimu bora inaendana na uwepo wa mazingira mazuri ya kufundishia wanafunzi, hivyo watahakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo hali yaliyokusudiwa.

Naye msimamizi wa msikiti wa Makombeni Mzee Othman Khamis, alisema matufali hayo yatawasaidia katika kumaliza ujenzi wa mnara wa kuhifadhia maji katika msikiti wao.

“Sisi tunaujenzi wa mnara wakuwekea tangi la kuhifadhia maji, sasa msada huu sisi umekuja kwa wakati muwafaka litakapokamilika basi hata wananchi waliobakia wataweza kupata maji ipasavyo”alisema.

Hata hivyo aliwataka walimu na wasimamizi wenzake, ambao wamekabidhiwa matufali kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wazuri ili kuona matufali hayo yanatumika ipasavyo na kwa lengo lililokusudiwa.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa skuli ya msingi na sekondari Michenzani Ussi Issa Said, alisema matufali 2000 atakayopatiwa watayatumia kwa ajili ya ujenzi wa madarasa yaliyopo katika skuli yao.

“Sisi tutayatumia kwa kujengea madarasa yetu na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika skuli yetu,wanafunzi watapata kusoma kwa umakini sana”alisema.

Mapema mbunge wa Jimbo la Mkoani Kisiwani Pemba, Profesa Makame Mbarawa Mnayaa alisema lengo la kukabidhi matufali 25,000 ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo waliinadi wakati wa kampeni kwa kuahidi wananchi.

Alisema matufali hayo yataambatana na mchanga, saruji na kokoto ili kuona harakati za ujenzi wa skuli, madrasa za Qurani na miskiti inaendelea kwa kasi ndani ya jimbo hilo.

Alisema jumla ya shilingi Milioni 27, 000/= zinatarajiwa kutumika katika ununuzi wa matufali, huku skuli ya shidi na Mkoambeni zikipatiwa matufali 2000 saruji na kokoto, huku skuli ya mjimbini ikipatiwa matufali 3000 ya nchi sita kutokana na ujenzi wake wa gorofa.

“Zipo Madrasa za Qurani zitapatiwa  matufali 400,300,200, hii yote ni kuunga mkono juhudi zao mbali mbali wanazozionyesha ndani ya jimbo hili”alisema.

Alisema kukamilika kwa ujenzi huo wa skuli wataweza kuboresha maisha ya wananchi ikiwemo upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wao.

Naye Diwani wa wadi ya Mkoani Ali Abdalla Gairo, alisema misaada hiyo itakuwa ni chachu ya maendeleo katika jimbo la mkoni, kwani imefika kwa wakati muwafaka kwao.