NA ABDI SULEIMAN.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka wazazi, wanafunzi na walimu wa skuli ya Utaani Sekondari, kuwa wastahamilivu na wavumilivu, na kufahamu kuwa mtihani uliotokea ni mipango ya Mwenyezi Mungu imeshaandikwa.
Imesema kutokea kwa mtihani wa kuungua kwa modo weni la wanafunzi wanawake, haitokua sababu ya kurudi nyuma kimasomo badala yake masomo yataendelea siku zote hususana kwa wanafunzi ambao wanajindaa na mitihani yao ya kidatoi cha sita.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, alipokua akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi huko skuli ya Utaani, kwa lengo la kuwafariji waathirika wa tukio hilo.
Alisema suala la elimu ni jambo muhimu sana kwa watoto, aliwataka wanafunzi kuzidisha juhudi katika masomo yao hususana kipindi hiki wanachoelekea katika mitihani ya kitaifa, huku wahisani mbali mbali wakiahidi kuwasaidia wanafunzi, walimu na basa wiki ijayo.
“Tukio hili lililotokea sio la Wizara ya elimu tu, hili ni tukio la taifa nzima hapa wapo wanafunzi wazazi wao wako mkoani, Chake Chake, lazima tuwe na subra katika kipindi hiki huku tukimshukuru mungu kwa kutokutokea maafa”alisema.
Aidha Waziri huyo alitoa siku tatu kwa wanafunzi wa kidato cha sita, kwenda kuonana na familia zao ili waweze kupatiwa elimu ya saikolojia, ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida.
Akizungumzia juu ya matengenezo ya umeme kwenye bweni la wanafunzi wa kiume, alisema jumla ya shilingi Milioni 28 zinahitajika kufanyia matengenezo mfumo wote wa umeme, ili wanafunzi wakike waweze kutumia kwa muda.
Hata hivyo Waziri Lele, alitoa wiki moja kwa injia wa ujenzi wa Wizara ya elimu kufanya tathmini ya ujenzi wa skuli hiyo na tathmini hiyo izingatie mahitaji ya baadae.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Harous Said Suleiman, aliwataka wanafunzi hao kuwa kitu kimoja na kuendeleza upendo na umoja wao, kama walivyokua kabla ya kupatwa na mtihani huo.
“Huu ni mtihani wa Mwenyezi Mungu ametupa na tunapaswa kumshuku, ikizingatiwa hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha, serikali ipo pamoja na nyinyi nyote na mutasaidiwa kwa kila kitu”alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib alisena ni wanafunzi 22 waliofikishwa spitalini kutokana na kupata mshuto, huku wakilazimika kuchukua maamuzi magumu ya kuwarudisha majumba wanafunzi wa kidato cha tano hadi cha kwanza na kuwabakisha wanafunzi wamkidato cha sita.
“Sinabudi kuwashukuru wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama, kwa juhudi zao kubwa kuhakikisha wanafunzi wanatoka salama, hii iliyotokea ni kudra ya Mwenyezi Mungu”alisema.
Naye Afisa Mdhamini Wizara ya habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau aliwapa pole wanafunzi na uongozi wa Mkoa, kwani wanafunzi hao ni sehemu ya vijana ambao Wizara yake inasimamia.
Afisa mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor, alisema zaidi ya shilingi Milioni 108 zinahitajika ili kuwasaidia wanafunzi 626 ambao wameokoa roho zao katika tukio la moto.
Alisema wanafunzi hao hakuna aliyetoka na kitu chochote ndani ya tukio la moto, zaidi ya walichokuwa nacho mwilini mwao hakuna chengine, hivyo wameathirika kwa kiasi kikubwa.
Alisema kwa sasa kilio kikubwa kwa wanafunzi na walimu ni vifaa vya masomo ya sayansi ambavyo vimepotea, huku ikizingatiwa kuna baadhi ya wanafunzi wanajiandaa na mitihani ya kidato cha sita mwaka huu.
“Jengo limepotea hili jengo lilikua ni lakihistoria sasa limekua gofu, hakuna aliyeamini moto ulivyokua na wanafunzi walivyosalimika, vijana wote wanalia mpaka sasa juu ya kukosa vitu vyao”alisema.
Hata hivyo aliyomba Wizara ya Elimu na wadau wengine wa maendeleo, kuwaangali wanafunzi hao na Ramadhani hiyo hapo inakuja katika suala zima la kuwasaidia futari.
MWISHO