NA ABDI SULEIMAN.
KAMATI ya Utalii ya Wilaya ya Micheweni imetakiwa kuibua vivutio vipya vya kiutalii, ambavyo vitaifanya wilaya hiyo kuendelea kupiga hatua katika sekta hiyo.
Alisema Wilaya hiyo licha ya kuwa maarufu nchini kwenye uwekezaji wa mahoteli, lakini imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kiutalii ambavyo havijaibuliwa na vinapaswa kuibuliwa ili jamii iweze kuvifahamu zaidi.
Mkuu huyo wa Wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Utalii ya Wilaya hiyo, alisema wakati umefika wa kiviibua na kuvitangaza vivutio vipya vya kiutalii, ambavyo wageni watweza kuvutikana navyo.
Wito huo aliutoa wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya utalii ya Wilaya ya Micheweni, pamoja na maafisa kutoka Kamisheni ya Utalii Pemba huko katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Aidha alivitaja baadhi ya vivutio hivyo ni pamoja na mapango ya asili, msitu wa hifadhi ya wanajamii micheweni, lugha wanayozungumza wananchi wa micheweni na uwepo wa vyakula vya asili vya micheweni, wanyama waliomo ndani ya msitu huo pamoja na ngoma zake.
“Sisi huku tumejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kiutalii, sasa wajibu wetu wajumbe wa kamati ni kuhakikisha tunaviibua na kuvitangaza na kuviwekea ulinzi”alisema.
Mapema mdhamini wa kamisheni ya Utalii Pemba Hamad Amini Ali, alisema sekta ya utalii ndio nguzo muhimu kwa Zanzibar kwani imekua ikichangia pato la taifa.
Alisema wajumbe wa kamati hiyo wanapaswa kuufanya msitu wa micheweni, kuwa kama msitu wa Ngezi na kuanza kuingiza wageni iwapo wanajamii watakubalia kuutunza.
Naye afisa maendeleo ya Utalii Pemba Said Salim Ali, alisema bado kuna baadhi ya wananchi wanaona utalii ni uhuni, jambo ambalo sio sahihi utalii ni kazi kama ilivyokazi nyengine.
Kamati ya utalii inapaswa kuibua fursa na miradi ya kiutalii kwa kuzingatia rasilimali zilizopo nchini, miradi ambayo itaweza kuwavutia wageni.
Wakichangia katika kikao hicyo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walisema Wilaya ya micheweni imejaaliwa kuwa na vyakula vingi vya asili vinaweza kutumika ikiwa kamati itaweza kuviendeleza.
Mjumbe Kutoka ZIP Ali Rashid, alisema lengo ni kila mmoja kuhakikisha utalii unafikiwa na dhana ya uchumi wa buluu na unatekelezwa kwa vitendo.
Naye Fadhili Hamad alisema msitu wa jamii Micheweni imejaaliwa kuwa na wanyama wengi, ikiwemo vihodi, komba vipepeo hivyo ni wajibu wa wajumbe kuviwekea ulinzi na mikakati zaidi.