Thursday, November 14

DC Wete awataka vijana kujikusanya na kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata msaada.

NA ABDI SULEIMAN.

Mkuu wa Wilaya ya Wete Dk.Hamad Omar Bakar, amesema utekelezaji wa vitendo wa miradi inayoanzishwa katika vikundi vya ushirika, ndio mkombozi pekee wa kiuchumi kwa wanaushirika na mtu mmoja mmoja.

Alisema iwapo vijana watajikusanya pamoja na kuunda vikundi vyao, itakuwa ni rahisi kupata msada wa pamoja kutoka serikalini au mashirika mengine.

Dk.Hamad aliyaeleza hayo shehia ya Kambini Wilaya ya Wete, kwenye hutoba yake iliyosomwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wilaya hiyo Seif Salim Mussa, katika mkutano wa msafara wa vijana wa kuhamasisha amani na mtengamano wa jamii, kupitia mradi wa mtengamano wa jamii na amani Zanzibar unaotekelezwa na taasisi za kidini.

Alisema ili kufikia mabadiliko hayo ni vyema kwa akinamama na vijana, kuzitumia fursa zinazoletwa na mashirika za kuanzisha vikundi vya ushirika, ili wapate mitaji itakayowasaidia kuanzisha miradi mbali mbali ya uzalishaji.

Akizungumzia suala la Amani, aliwataka wananchi kutokuichezea amani kwani nchi nyingi zimekuwa katika mashaka kutokana na kuicheza amani hiyo.

“Tusitumie nguvu zetu tukakubali au kushawishiwa na tukakubali kuivunja amani tulionayo, amani hii ni tunu pekee kwa Tunapaswa kuienzi kwa vitendo”alisema.

Kwa upande wa udhalilishaji Dk.Hamad, alisema siao suala la kulichukilia mzaha kwani limekua ni janga la taifa na hatuna budi kuungana na serikali kukea suala hilo.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuwa tayari kuhesabiwa wakati utakapofika, ili serikali iweze kujua mahitaji ya wananchi wake na idadi yake.

Mwakilishi kutoka taasisi za kidini Zanzibar Profesa Issa Haji Zidi, alisema wanahamasisha amani kwa vijana na akinamama vijijini, pamoja na kuunda vikundi mbali mbali vya ushirika na kutumia fursa zinazotokana na vikundi hivyo.

Kwa upande wake Afisa Uchechemuzi na mawasiliano kutoka shirika la NCA Nizar Selemani Utanga, alisema wanatumia mbinu mbali mbali za kuhamasisha amani ili jamii iwe na amani ya kweli.