Wednesday, January 1

Sangaiwe wapongeza uwekaji wa kamera maalumu katika hifadhi ya Wanyama Burunge

NA ABDI SULEIMAN, BABATI.

WANANCHI wa Kijiji cha Sangaiwe Wilaya ya Babati Mkoa wa Mnyara, wamesema mradi wa uwekaji wa kamera maalumu katika hifadhi ya Wanyama Burunge, utaweza kuwasaidia kupata mazao yao mbayo walikuwa wakiyakosa kutokana na kuvamiwa na wanyama.

Walisema kamera hizo zitaweka katika maeneo maamulu, ambayo wanyama wakipita kuingia katika mashamba ya wakulima wataonekana moja kwa moja na walinzi kwenda kumfurusha.

Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari za Mazingira kutoka (JET), waliotembelea hifadhi wanyama Burunge shuruba ya kwakuchinja, kupitia mradi wa USAID “Tuhifadhi Maliasili”, unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET).

Mmoja ya wananchi hao Anastazia John Mwanso (50), alisema mradi huo ni mzuri kwani utaweza kuwapunguzia kadhia ya wanyama kuharibu mazao yao.

Alisema kwa sasa matarajio makubwa ni kuona wanapata mazao mengi katika msimu huu, baada ya kufungwa kwa kamera hizo ambazo zitaweza kuwafanya wanyama kuonekana na kuweza kufurushwa.

“Tulikuwa tunajitahidi kulima tena maeneo yetu makubwa, ila kutokana na wanyama wanavovamia mashamba huharibu mazao, wakati mwengine tunapata mwengine tunakosa kabisa”alisema.

Naye Emelda Patrick Sangu (49), alisema kamera zitakuwa pembezoni na kupelekea kuwa walinzi wa mazao, hali inayopelekea matumaini kwa wakulima wengi wanaozunguka hifadhi ya burungwe.

“Uwekaji huo utaambatana na ujengaji wa vibanda pembezoni hifadhi, kwa jili ya walinzi na kuweza kuwarudisha nyuma wanyama wasiweze kuingia katika mazao”alisema.

Kwa upande wake Nicodemas D. Mofulu(33), alisema licha ya mfumo huo kuchelewa kuwafika katika kijiji chao, lakini wakulima wamekuwa na mategemeo makubwa, katika msimu huu kupata mazao mengi.

“Kamera hizi zitakuwa zinamurika umbali wa mita 100 na zitaweza kutoa taarifa mapema, iwapo kuna wanyama wanakaribia kuvuka eneo la hifadhi na kuekelekea kwenye mashamba, hapo walinzi watakuwa tayari kuwafukuza mnyama huyo”alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waanidshi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) John Chikomo, alisema JET inatekeleza mradi wa miaka mitano wa Tuhufadhi Maliasili, ulianza na mafunzo na baadae ni kutembelea katika shoroba sita zinazofanyiwa kazi.

Alisema lengo la ziara ni kuzidi kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuzidi kuandika habari za uhifadhi, wanyamapori na shoroba kwa uhakika.

Katibu wa hifadhi ya jamii Burunge WMA, Benson Mwaise alisema lengo ni kuhakikisha uhifadhi unafikiwa na wananchi wanaozunguka hifadhi hizo wananufaika na hifadhi hiyo.

Alisema hifadhi ya burunge ni miongoni mwa maeneo 16 ya hifadhi za jamii, ipo babati tarafa ya Mbugwe ndani ya kata tatu ikiwemo Mwada, Magara na ukaiti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Burunge WMA Khamis Juma Ngimba, alisema wataalamu kutoka chuo cha Nelson Mandela Arusha, wataweza kuwaweka teknolojia ya kamera itakayo wasaidia katika vijiji vyao, kubaini wanyama wapi wamepita na wanaenda kuharibu mazao ya wananchi.

Alisema kamera hizo zitakuwa msaada mkubwa kwao, kwani wanyama hataweza kwenda kuharibu mazao ya wananchi, huku akiwataka wananchi wa kijiji cha Sangaiwe kuupokea mradi huo ambao umeanza kwao.