Saturday, January 4

Waziri Jafo awapongeza wadau kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akizindua jiko banifu ambalo litakalobaidhiwa kwa Shule ya Sekondari Kimani wilayani Kisarawe mkoani Pwani ambalo litasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni ambapo amewapongeza wadau wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha mazingira yanalindwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akifurahia mandhari ya Msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani wakati wa Kongamano la Wasaa wa Mazingira lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) kwa ushirikiano na Taasisi ya Vodacom Foundation Tanzania.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akiwa ameshika mche wa mti kwa ajili ya kuupanda katika Msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani wakati wa Kongamano la Wasaa wa Mazingira lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) kwa ushirikiano na Taasisi ya Vodacom Foundation Tanzania.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akizungumza na wadau mbalimbali wa mazingira (hawapo pichani) wakati wa Kongamano la Wasaa wa Mazingira lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) kwa ushirikiano na Taasisi ya Vodacom Foundation Tanzania na kufanyika katika Msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo amewapongeza wadau wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha mazingira yanalindwa.

Ametoa pongezi hizo wakati aliposhiriki katika Kongamano la ‘Wasaa wa Mazingira’ lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) kwa ushirikiano na Taasisi ya Vodacom Foundation Tanzania na kufanyika katika Msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani.

Akizindua jiko banifu Dkt. Jafo alisema Serikali inatambua mchango wa taasisi zisizo za kiserikali ambazo kwa namna moja ama nyingine zinashiriki kikamilifu katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

Akizungumzia jiko hilo Mratibu wa Taasisi ya Kuendeleza Nishati Asilia (TATEDO) Bw. Shima Sago alisema litasaidia kupunguza kiwango kikubwa cha ukataji wa miti kwa ajili ya kuni.

Alisema waligungua kuwa katika Shule ya Sekondari Kimani wilayani humo ambayo ilitarajiwa kukabidhiwa jiko banifu hilo, walitumia takribani kuni 3,200 kwa wiki hivyo kwa sasa watapunguza na kutumia kuni 400 kwa wiki mbili.

Pia Sago alisema jiko hilo linatunza afya ya mtumiaji kwa kuepuka moshi unaoweza kutoka wakati wa kupika na badala yake utapita kwenye bomba maalumu nje ya mahali pa kupikia.

Hata hivyo akizungumza na wadau mbalimbali wa mazingira mara baada ya kushiriki zoezi la kupanda miti katika eneo la msitu, Waziri Jafo aliitaka jamii kuutunza msitu huo sambamba na kupanda miti kwani unasaidia kunyonya hewa ya ukaa.

Kwa upande wake Balozi wa Mazingira, Bi. Yvonne Cherry ‘Monalisa’ alisema Kampeni ya ‘Soma na Mti’ hiyo haiwahusu tu wanafunzi na wanachuo bali kila mtu anatakiwa ashiriki.

Monalisa ambaye pia anasimamia kampeni hiyo alitoa rai kwa wazazi na walimu kwenye shule na vyuo mbalimbali nchini kuwasimamia wanafunzi katika kushiriki upandaji miti.

Aliongeza kuwa upandaji miti uende sambamba na utunzaji ili kuhakikisha inakua nma hivyo kuifanya nchi yetu kuendelea kuwa ya kijani hatua itakayosaidia kuhifadhi mazingira.