Alikuwa yatima akiwa na umri wa miaka mitatu tu lakini akaja kuwa kuwa mmoja wa watu matajiri zaidi duniani. Kwa sasa uhusiano wa Roman Abramovich na rais Vladimir Putin wa Urusi umeanza kuzongea biashara na kuharibu sifa yake hiyo.
“Nina uhakika watu watanizonga kwa siku tatu au nne lakini litapita,” alisema bilionea huyo wa Urusi wakati alipoinunua klabu ya Chelsea mwaka 2003. “Watasahau mimi ni nani, na hicho ndicho nachopenda.”
Kuna nafasi ndogo ya kujificha, kutokana na matukio ya wiki chache zilizopita. Kufuatia miaka kadhaa ya madai ya uchunguzi zaidi wa shughuli za Bw Abramovich, serikali ya Uingereza imezuia mali zake zinazoshikiliwa zilizoko nchini humo – ikiwa ni pamoja na nyumba zake, kazi za sanaa na Chelsea FC – na kumuwekea marufuku ya kuingia nchini humo.
Imemtuhumu kwa kushirikiana na Putin katika uvamizi wa Ukraine.
Kuanguka huku kutoka kwenye neema kwa mtu huyu ambaye ametawala soka Uingereza lakini mashabiki wa mchezo huo wamegawanyika sana kupitia mchakato huo ambao baadhi wanaufurahiwa na wengine hawaufurahii.
Kutoka yatima mpaka ‘kibopa’
Roman Arkadyevich Abramovich alizaliwa mwaka 1966 Saratov kusini magharibi mwa Urusi, maili kama mia kutoka mpaka na Ukraine.
Mama yake, Irina, alifariki kutokana na sumu kwenye damu Abramavoch akiwa na umri wa mwaka mmoja na baba yake alifariki miaka miwili baadaye baada ya kupata ajali ya mashine ya ujenzi.
Baada ya hapo Bw Abramovich alilelewa na jamaa zake, akitumia muda huko Komi, kaskazini magharibi mwa Urusi.
“Kusema ukweli siwezi kuita utoto wangu mbaya,” aliwahi kuliambia gazeti la Guardian katika mahojiano adimu.
“Katika utoto wako huwezi kulinganisha vitu: mwingine anakula karoti, mwingine anakula pipi, vyote vina ladha nzuri. Kama mtoto huwezi kueleza tofauti.”
CHANZO CHA PICHA,EAST2WEST NEWS
Aliacha shule akiwa na umri wa miaka 16, akafanya kazi kama fundi na alihudumu katika Jeshi Nyekundu kabla ya kuuza vitu vya kuchezea vya plastiki huko Moscow.
Aliendelea na biashara za kuuza manukato, akijenga utajiri wake chini ya kiongozi wa Soviet Mikhail Gorbachev aliyeruhusu uwazi wa biashara na wigo zaidi kwa wajasiriamali.
Kuanza kwa utajiri wake wa ‘utata’
Kuvunjwa kwa Umoja wa Sovieti, na uwepo wa rasilimali ya madini, kulitoa fursa zaidi, na akiwa kwenye uimri wake wa miaka ya 20, Bw Abramovich alijikutana na bahati kuelekea utajiri.
Akanunua kampuni ya mafuta ya Sibneft kwa karibu dola $250m kutoka serikali ya Urusi katika mnada uliojaa ‘magumashi’ mwaka 1995. Aliiuza tena kwa serikali kwa dola $13bn mwaka 2005, yaani miaka 10 baadae.
Mawakili wake wanasema hakuna msingi wa madai kwamba alijipatia utajiri mkubwa kupitia uhalifu. Hata hivyo, mnamo 2012, alikiri katika mahakama ya Uingereza kwamba alifanya malipo ya rushwa ili kusaidia kupata mkataba wa Sibneft.
CHANZO CHA PICHA,EAST2WEST NEWS
Maelezo ya picha,Abramovich,akiwa na marafiki zake
Alihusika katika “vita vya aluminium” vya miaka ya 1990, ambapo matajiri wengi – wale ambao walikuwa na utajiri mkubwa na nguvu za kisiasa baada ya kuanguka kwa Soviet – walipigania udhibiti wa sekta hii kubwa.
“Kila baada ya siku tatu, mtu alikuwa akiuawa,” Bw Abramovich alisema mwaka 2011, na kuongeza kuwa tishio hili kwa usalama wake lilimfanya kusita sita kushiriki ‘vita’ hiyo.
Lakini Bw Abramovich ‘akakomaa’, na kuongeza mamia ya mamilioni ya fesha katikati ya vita hiyo.
Kuingia katika siasa
Alikuwa mshirika wa Rais Boris Yeltsin na mtu muhimu kwenye siasa za Moscow baada yakuvunjika kwa Soviet, na hata kuwa na makazi kwa muda Kremlin.
Wakati Bwana Yeltsin alipojiuzulu mwaka 1999, Bw Abramovich aliripotiwa kuwa miongoni mwa wale waliomuunga mkono waziri mkuu na jasusi wa zamani wa KGB, Vladimir Putin, kuwa mrithi wake.
Bwana Putin alivyojiimarisha zaidi, alianza kuonywesha ‘umwamba’ dhidi ya matajiri. Wengine walienda gerezani, na wengine wakahamishwa ikiwa walishindwa kuonyesha utii kwake.
CHANZO CHA PICHA,REUTERS
Bw Abramovich hakuathirika na hatua hiyo ya Putin. Mwaka 2000, alichaguliwa kuwa Gavana wa eneo la Chukotka, Kaskazini mashariki mwa Urusi. Alipata umaarufu baada ya kuwekeza fedha zake mwenyewe katika huduma za kijamii lakini alijiuzulu mwaka 2008.
Wakati wote huo, aliendeleza biashara yake, akisaka kila fursa ya utajiri mfano kwenye Sanaa ya uchoraji, nyumba na magari.
Wito kutoka London
Katika hatua isiyo ya kawaida kwa mtu anayetajwa kuwa mkimya, mwenye aibu, mwaka 2003 Abramovich alijipatia umaarufu katika ulimwengu wa soka wakati alipoinunua Chelsea, klabu kubwa zaidi magharibi mwa London, katika mkataba wenye thamani ya £140m.
“Falsafa yangu yote katika maisha ni kufanya kazi na timu za kulipwa” aliliambia gazeti la Financial Times. “Huko Chukotka nina timu za kulipwa na nitafanya hivyo hapa pia.”
Chini ya meneja Jose Mourinho na wengine, utajiri wa Abramovich uliisaidia Chelsea kushinda mataji matano ya ligi ya England, mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na vikombe vitano vya FA.
CHANZO CHA PICHA,PA MEDIA
Fedha za matajiri zimekuwa zikitiririka London katika miaka ya hivi karibuni. Jalada la mali ya Bw Abramovich linaaminika kujumuisha jumba la kifahari lenye vyumba 15 vya kulala la Kensington Palace Gardens magharibi mwa London, ikiripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya £150m; gorofa la Chelsea; ranchi huko Colorado; na nyingine French Riviera.
Boti yake ya kifahari – Solaris and Eclipse – ni miongoni mwa boti kubwa zaidi duniani. Bw Abramovich, ambaye ameachana na wake zake watatu mara tatu, pia anamiliki ndege binafsi.
Kesi ya kumchafulia jina
Alipoulizwa na Guardian mwaka 2006 kuhusu kile ambacho fedha inaweza kumfanyia mtu, alijibu: “Haiwezi kununua furaha. Uhuru kiasi, ndio.”
Bila shaka ana pesa nyingi. Chombo kikubwa cha habari za kifedha, Bloomberg inakadiria kuwa utajiri wa Bw Abramovich ni dola $13.7bn.6bn), na kumuorodheshwa kama mtu anayeshika nafasi ya 128 kwa utajiri duniani. Kampuni yake ya Forbes inamtaja kuwa na utajiri wa 12.3bn, na kumuweka katika nafasi ya 142.
Hoja kubwa, hata hivyo, ni kiwango cha uhuru alionayo kwa Putin.
Mwaka jana, Bw Abramovich alilishtaki gazeti la HarperCollins kwa kashfa ya kitabu cha Putin’s People kilichoandikwa na Catherine Belton, ambacho kilidai kuwa rais wa Urusi amemuamuru tajiri huyo ainunue Chelsea.
CHANZO CHA PICHA,REUTERS
Maelezo ya picha,Roman Abramovich ana miliki boti mbili za kifahari
Pande hizo mbili ziliamaliza mzozo wao nje ya mahakama, huku mchapishaji akikubali kutoa ufafanuzi.
Lakini uhusiano wa Bw Abramovich na Putin umeendelea kumsumbua, hasa wakati majeshi ya Urusi yaliposogea kwenye mpaka na Ukraine na kisha kuivamianchi hiyo.
Wakati kufungia mali zake Bw Abramovich na matajiri wengine sita huko Uingereza, Waziri wa Mambo ya Nje Liz Truss alisema: “Damu za watu wa Ukraine ziko mikononi mwao.”
Abramovich alitangaza kuiuza Chelsea siku nane kabla ya kuwekewa vikwazo. Mashabiki hasa wa Chelsea wanaendelea kuliimba jina lake viwanjani kwenye mechi mbalimbali. Lakini wanasiana wanataka mali zake zitaifishwe kabisa na sio kuzuiwa. Kuerejea kwake London Mashariki kwa sasa ni jambo linaloonekana kuwa gumu.
Katika hali ya kushangaza, sasa imeibuka taarifa kwamba Bw Abramovich alipata dalili za sumu mwilini inayoshukiwa kuwekewa yeye na wapatanishi waandamizi wengine wa Ukraine – katika mazungumzo ya amani kwenye mpaka wa Ukraine na Belarus mapema mwezi Machi.
CHANZO CHA HABARI BBC SWAHILI.