Monday, November 25

Walimu wa skuli za msingi kisiwani Pemba watakiwa kuwa na utayari wa kuyatumia mafunzo ya Jifunze kwa hatua.

NA SAID ABRAHMAN.

 

MRATIBU wa Skuli za Sekondari Kisiwani Pemba Suleiman Hamad Suleiman, amewataka walimu wanaoshiriki mafunzo ya “Jifunze kwa hatua” kuwa na utayari ili wawe chachu kwa walimu wengine.

 

Alisema kuwa endapo walimu hao wataweza kuyafuatilia kwa umakini mafunzo hayo, watakuwa ni kigezo kikubwa kwa walimu wenzao ambao wako nyuma na kuwafanya nao waende na wakati.

 

Hayo aliyaeleza kwa niaba ya Ofisa Mdhamini wa Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba, Mohammed Nassor Salim, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya”Jifunze kwa hatua”(TaRL), yaliyoandaliwa na taasisi ya Milele Foundation huko katika kituo Cha science Pujini Wilaya ya Chake Chake Pemba.

 

Mratibu huyo alisema kuwa chanzo Cha baadhi ya wanafunzi kutoweza kusoma, kuandika pamoja na kuhesabu ni kutokana na kukosekana msingi imara kwa watoto hao.

 

Aidha alikiri kuwa ndani ya Wizara ya elimu, kuna walimu wameajiriwa kufundisha Skuli mbali mbali ndani ya Visiwa hivi, lakini nia yao sio hiyo baada ya kukosa sehemu nyengine ikawalazimu kuajiriwa ndani ya Wizara hiyo.

 

“Hivi Sasa imefikia hatua ya wizarani kuna mrundikano wa mabarua mengi ya walimu, tayari wameshindwa kazi ya kusomesha na wanataka wabadilishiwe sehemu nyengine ya kufanya kazi,” alisema Mratibu.

 

“Walimu wenzangu tuna tatizo, tumekuwa na utamaduni Mwalimu anapangiwa vipindi viwili, anakuja na kusomesha dakika (10) tu anaondoka anakwenda sehemu nyengine, huo sio utaratibu wa kusomesha bali ni kuondoa njiani tu,” alifahamisha.

 

Hata hivyo aliipongeza taasisi ya milele Zanzibar Foundation, kwani imekua mstari wambele katika kuhakikisha changamoto zilizopo katika sekta ya elimu, wanashirikiana na Serikali kuu pamoja na Wizara husika wanazitatua kwa pamoja.

 

Nae Mratib wa taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Abdalla Said, alisema taasisi yao imekuwa ikisaidia katika nyanja tatu (3), elimu, afya pamoja uchumi jamii, ambapo wametenga maeneo ya vijijini katika kutekeleza majukumu yao.

 

Aidha alisema taasisi hiyo imeandaa Mipango mbali mbali ya kusaidia jamii, katika maeneo tofauti ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

 

Hata hivyo alisema Milele imekua mstari wa mbele kwa upande wa Zanzibar, katika kusaidia shuhuli mbali mbali za kijamii na kiserikali.

 

Akizungumzia mradi wa “Jifunze kwa hatua” Abdalla alieleza kuwa mradi huo, utakuwa ni miaka mitatu hadi mitano na wako katika mazungumzo na TaRL Afrika ili kuona mradi huo unaendelea.

 

“Niwaombe washiriki wa mafunzo haya waitumie nafasi waliyoipata ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na tunasema wazi kuwa Mwalimu ambae hatofanya vizuri hatopata cheti,” alieleza Mkurugenzi.

 

Nae Meneja wa Miradi ya elimu kutoka Milele Zanzibar Foundation Eshe Haji Ramadhan, alifahamisha kuwa Mradi huo umebuniwa katika nchi ya India ambao unampa nafasi Mwanafunzi kuweza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

 

Aidha alisema taasisi ya Milele Zanzibar Foundation iliona ni vyema na wao kuja na mpango huo ndani ya Visiwa vya Zanzibar kwa lengo la kunyanyua kiwango Cha elimu.

 

“Milele imedhamiria kunyanyua kiwango Cha elimu kwa hali ya juu kwa Zanzibar ila kubwa ni kuwataka walimu watakaopata mafunzo haya kushirikiana kwa pamoja,”alisema Eshe.

 

Katika mafunzo hayo ambayo yatakuwa kwa muda wa siku (10) yameweza kuwashirikisha walimu 30 kutoka Kisiwani Pemba.