Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi, Winnie Byanyima, amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu unyanyasaji wa kijinsia aliopitia.
“Nilishtuka, nilikuwa na umri wa miaka 18… Hili lilikuwa jaribio la ubakaji,” Bi. Byanyima alisema.
Alizungumza hayo katika kipindi cha BBC cha Desert Island Discs kuwa hajawahi kushiriki hadithi hiyo.
Alisema akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu mjini Kampala mwaka 1977, mhadhiri alikwenda chumbani kwake na kusema kama angekuwa mpenzi wake atafaulu mitihani yake.
Bi Byanyima alikumbuka kuwa alikuwa “msichana mdogo anayejiamini”.
“Nilisema: ‘Sihitaji msaada wowote’ na nikamwomba aondoke.”
‘Hakuna neno la unyanyasaji’
Aliwajulisha wazazi wake, ambao walidhani hangeweza kukaa chuo kikuu kwasababu ya “kudanganywa” na kusema anapaswa kuondoka.
Wakati huo, Uganda ilikuwa chini ya utawala wa dikteta Idi Amin.
Rafiki wa familia yake alikuwa na uhusiano mzuri na majenerali fulani, kwa hiyo akajitolea kumsaidia na hati za kusafiri.
Mipango ikafanywa ili aende naye kwenye wizara ya elimu.
Lakini hakuwahi kumpeleka kwa wizara ya elimu kama alivyoahidi.
Badala yake, alimpeleka nyumbani, akijifanya kuwa amesahau kitu.
“Tulipofika nyumbani yake, akaweka muziki ,wimbo ulikuwa The First Cut Is The Deepest na alikuja kuninyakua,” alikumbuka.
“Nilipiga kelele, aliona aibu, akasimama, akaniingiza kwenye gari na kunirudisha chuo kikuu na kusema mimi ni mjinga, mimi ni mtoto. “Mambo haya hutokea.” Alisema: “Mambo hayo hutokea.”
- Winnie Byanyima ni nani?
“Nilishtuka, nilikuwa na umri wa miaka 18. Sijawahi kuwa na uhusiano na mvulana yeyote. Hili lilikuwa jaribio la ubakaji.
“Wakati huo, hakukuwa hata na neno moja linaloitwa unyanyasaji wa kijinsia au unyanyasaji.
Kulikuwa na ubakaji, lakini ilikuwa aibu kukiri,” mkuu wa UNAids alikumbuka.
Alifanikiwa kufika Uingereza lakini alipofika, hakuweza kuwaambia maafisa wa uhamiaji kilichomkuta.
“Nilimtaja binamu yangu ambaye alikuwa ameuawa. Nilisema nilihofia maisha yangu. Lakini sikuweza kusema kulikuwa na jaribio la kubakwa au kuninyanyasa kingono mara kadhaa. Ilikuwa ni aibu sana,” alisema.
Maisha chini ya utawala wa Amin
Alirejea Uganda na kuwa mbunge kabla ya kukaa miaka kadhaa katika Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Mnamo mwaka 2013, Bi Byanyima alikua mkuu wa Oxfam International.
Wakati huo shirika hilo la msaada lilikumbwa na kashfa za ngono, ambayo ilitokea kabla ya wakati wake katika uongozi wa shirika.
“Wakati fulani nilivunjika moyo wakati wa mzozo huo, ilikuwa wakati wa mahojiano ya redio na mwanahabari wa Canada, ambaye alinishambulia sana,” Bi Byanyima alisema.
“Nilikuwa nikijaribu kutojitetea, kusema ninaelewa uchungu wa unyanyasaji wa kijinsia.
Hakumwambia kile ambacho kilimtokea binafsi “lakini moyoni mwangu nilikuwa huko”, alisema.
“Baada ya mahojiano nililia kwa sababu, najua uchungu, au nilijua yote yatarudi. Ndiyo maana sikuweza kuomba msamaha. Sikuweza kuwatetea wafanyakazi, nilimtetea aliyenyanyaswa.”
Bi Byanyima pia alizungumzia maisha yake ya utoto chini ya utawala wa Amin “kuona vifo, kuona vurugu”.
“Katika shule, wakati familia zilikuwa zikija kumuondoa msichana darasani na kisha kumrudisha baada ya wiki moja akiwa amenyolewa nywele zote kichwani na huku akiwa na huzuni.
“Hapo tulijua kuwa baba yake alikuwa ameuawa au kutoweka na hatukuweza kulizungumzia,” Bi Byanyima alisema.
“Watu walizikwa majira ya usiku kwa sababu ilipaswa kujifanya kuwa hakuna mtu aliyekufa. Kwa sababu, ikiwa utazungumza juu yake au kuionesha, basi watakuja kwako pia,” aliongeza.
Akiwa mwanafunzi wa uhandisi mjini Manchester mwishoni mwa miaka ya 1970, Bi Byanyima alifanya kampeni dhidi ya Amin na baadaye akajiunga na kundi la waasi.
“Kuwa sehemu ya harakati kulinisaidia kuelekeza hasira yangu na kuhisi kuwa niko na wengine, nadhani hiyo iliniokoa,” aliongeza.
Aliteuliwa kuwa mkuu wa UNAIDS mnamo 2019.
CHANZO CHA HABARI BBC SWAHILI.