BAKAR MUSSA-PEMBA.
Vijana kwa tafsiri iliokubalika na Umoja wa mataifa ni wale watu ambao umri wao ni kuanzia miaka 15, ingawaje kwa hapa Tanzania kikomo chake cha ujana ni miaka 35.
Watu hawa ambao kwa sababu ya umri mdogo na wengi wao kukosa muda wakufikiri mambo yanayoweza kujitokeza baadae na wakiwa na harakati za uchangamfu wao mara nyingi hujikuta wamejiingiza katika ushawishi tena kwa urahisi zaidi kuingia katika makundi aidha yawe ya maema au maovu (mabaya) kwa kishindo.
Pamoja na hilo vijana ni hazina muhimu kwa taifa lolote na katika Sensa nyingi kundi hili huwa ni kubwa kuliko makundi mengine ya kijamiina huwa wanategemewa kutowa mchango mkubwa na mzuri katika ushiriki wa maendeleo.
Vijana hushawishika haraka kutokana na mategemeo ya kutekelezwa matarajio yao ikiwemo ingawaje wale wanaowashawishi wanakuwa kinyume na hivyo , matatizo mengi ya vijana katika nchi zinazoendelea ni ugumu wa ajira, ukosefu wa elimu ya ushindani katika soko la ajira na hizi huwafanya kwa baadhi ya nchi wakose uvumilivu.
Amani ni neno fupi lenye herufi tano (5) lakini limekuwa likibeba ujumbe mzito , amani maana yake kwa ufupi ni mfumo wa kuishi na kufanya mambo mbali mbali bila ya kuwepo na vurugu yoyote,ambapo msingi wake mkubwa wa kujenga amani ni upatikanaji wa haki , uvumilivu, haki za binaadamu, demokrasia na maendeleo.
Ukosefu wa amani una madhara makubwa katika mchakato wa maendeleo hivyo ni wajibu wa kila mmoja wakiwemo viongozi wa Siasa, Serikali, jamii nk, kujitahidi ili kuhakikisha neno hili la amani inakuwa ni sauti ya pamoja bila ya kuwa na kinyogo chochote.
Nanukuu usemi wa mwanasiasa mmoja kutoka India Mahatma Ghandi, yeye alisema “ Hakuna njia ya kwenda kwenye amani lakini amani yenyewe ndio njia” na kwa maana hiyo ipo haja yakujenga Utamaduni wa amani katika jamii kwa kuwashirikisha vijana katika mambo yanayowahusu na kuhakikisha hapa tulipo na tunakokwenda nchi na dunia kwa ujumla inakuwa na amani.
Kwa kupitia kalamu yangu naipongeza Serikali inayoongozwa na Dk, Hussein Ali Mwinyi kwa kuweza kuiendeleza wizara maalumu alioirithi kwa mtangulizi wake Dk, Ali Mohamed Shein inayohusiana na mambo ya vijana jambo ambalo limewaweka katika pahala pamoja na kuwapatia mambo mbali mbali yanayoweza kuwaendelea ikiwemo shughuli za ujasiriamali , kilimo nk.
Pamoja na hatuwa hiyo Dk, Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , samabamba na wasaidizi wake wakuu Makamo wa kwanza wa Rais Othman Massoud Othman, makamo wa pili wa Rais Hemed Suleiman Abdalla wamekuwa wakiihimiza amani kwa jamii na sio vijana pekee kila wanapopata muda wakuzungumza na wananchi.
Dk, Hussein Ali Mwinyi hata anapotowa hutuba baada ya sala ya Ijumaa , neno ambalo hawezi kulisahau ni kuhimiza amani , mfano katika hotuba yake kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika masjid Arafa Mombasa , Wilaya ya Magharibi B, aliwataka waumini na wananchi kulinda amani kwani bila ya amani ni vigumu kufikia maendeleo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Alhaj Dk, Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza wananchi kuendelea kuhubiri amani ili kuhakikisha nchi na watu wake wanakuwa salama .
Alieleza hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya watu kuanza kutowa maneno ya kuashiria kuvunja amani , hivyo aliwataka wananchi kukumbushana umuhimu wa kuhubiri amani.
Hata hivyo taasisi mbali mbali za kijamii kama vile Klab ya Waandishi wa habari Pemba (PPC) ndani yamiezi mitatu iliopita ilikuwa na mradi wa kutowa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, viongozi wa dini, Wasanii , Vijana na makundi mbali mbali juu ya kutowa taaluma ya umuhimu wa amani kwa jamii.
Sheikh Said Abdalla Nassor katika moja ya mikutano ilioandaliwa na PPC alisema, jamii haina budi kuacha tabia ya kuwaazima wanasiasa akili zao,hasa wakati wa kipindi cha Uchaguzi na wakakubali kuwa chanzo cha kuvunja amani kwani hawawezi kubaki salama.
Nae mchungaji wa Kanisa la Walokole liliopo Makangale Elius Maganga alieleza kuwa malezi wanayopwea vijana yananafsi kubwa juu ya kujitenganisha na uvunjfu wa amani.
“Tafuteni kwa bidii kuwa na watu wote, na huo utakatifu ambao hapana mtu atakae muona Mungu”Bibilia inasema mchungaji maganga,” alinukuu.
Alifahamisha ili kuhakikisha utakatifu ni kutenda mema ili utawale vizuri na uwe na maamuzi yasio na shaka , uwepo wa amani ni furaha kwa jamii na taifa, kitabu cha waibrania mlango wa 12 msitari wa 14 inaeleza hivyo.
Kwa mujibu wa matokeo ya sense ya mwisho ya mwaka 2012 asilimia 77% ya watu wote wanaumri wa miaka 35 na asilimia 19% wanaumri kati ya miaka 15-24 ambapo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hilo ni kundi la Vijana.
Hivyo basi vijana ambao ndio waliowengi na wenye kushawishika zaidi katika uvunjifu wa amani wanawajibu wakuzingatia vyema suala la kudumisha amani, kwani vijana wanahesabika kama nguzo kuu ya mchango mkubwa katika sekta mbali mbali za maendeleo.