NA FATMA HAMAD.
Mwalimu wa madrasa Juhudiya ,Sada Khamis Hamad ( mwenye ulemavu wa Viungo) ilioko Shumba Vyamboni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba amesema anakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa sehemu salama ya kusomeshea Wanafunzi kutokana na hali yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko nyumbani kwao mwalimu huo alisema mazingira ya madrasa yake sio rafiki, kwani anatumia kibaraza cha nyumba yao kuwafundishia Wanafunzi wake.
‘’Nasumbuka sana hususan kipindi cha mvua barazani panakua hapasomeki inabidi wanafunzi wasije madarasa mpaka mvua zikate.’’alisema mwalimu bi Sada.
Sada alieleza kuwa mwanzo alikua akienda madrasa maeneo ya mbali kwa ajili ya kusoma lakini badae akashindwa kutokana na hali yake, kwani alikua hawezi kutembea na akabakia tu nyumbani kwao.
Alisema baada ya kuona anakosa kusoma ndipo akamua anzishe madrasa yake mwenyewe ili aweze kuiendeleza elimu yake.
‘’Nilisema ulemavu wangu isiwe sababu ya kukaa tu nyumbani nikakosa kusoma bali nikanzisha madrasa yangu mimi mwenyewe ili niweze kufundisha Watoto jambo ambalo litanifanya niongeze kipaji changu,”alieleza.
Alieleza kuwa huu ni mwaka wa tatu tangu kuanzisha madrasa hiyo, ambapo alianza na wanafunzi wanne [4] wawili wa kike na wawili wanaume na sasa ana wanafunzi [52] wakiwemo wanawake na wanaume.
Hivyo aliwaomba wahisani na watu wenye nacho kujitokeza kumjengea angalau chumba kimoja ili wanafunzi wapate sehemu nzuri ya kusomea.
Kwa upande mwengine Sada alisema kuwa hakuwahi kusoma skuli hata darasa moja kwani ilikuwa ipo masafa ya mbali hawezi kutembea na alikua hana kigari cha kuendea Skuli.
‘’Sikusoma Skuli hata darasa moja, wazazi wangu walikua hawana uwezo wa kuninunulia kigari, ila tu mungu kanijalia kipaji najua kusoma na kuandika’’ alieleza sada.
Kwa upande wake mama wa msichana huyo alisema mungu amemjaalia kuzaa watoto wanne wote wenye ulemavu wa viungo.
Alisema mwanzo akiwazaa wanakua ni wazima wanatembea wenyewe, lakini kila wakiwa wakubwa ndo wanapata ulemavu hawawezi kutembea tena wala hajui sababu iliyopelekea kuwa hivo.
‘’Nilikua nawazaa ni wazima lakini mwisho wake wanakua walemavu, na sikuwapeleka Hospital nikajua ni sababu gani ilopelekea hivyo’’alisema mama mzazi.
Aidha alieleza kuwa anaishi katika mazingira magumu yeye na watoto wake kwani hata nyumba yao wanayoishi imeshakua mbovu na haina hata huduma rafiki za vyoo kwa ajili yao.
‘’Naomba msaada wa kujengewa nyumba ambayo itakua na choo chao ndani kwani wanapata shida wakati wanapokwenda kufanya haja zao,’’ Aliomba mama mzazi.
Ninakua Napata wasi wasi kila mda kwani nahisi wako hatarini kupata maradhi ya mripuko kutokana na kukosa choo ambacho si maalumu kwa najili yao.