NA ZUHURA JUMA, PEMBA
NAIBU Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Korea (KOICA) Jieun Seong amesema, uboreshwaji wa masomo ya hesabati, sayansi na kiengereza utasaidia kuimarisha mfumo mzima wa elimu kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo kazini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Benjamin Wete Mkoa wa Kaskazini, Naibu huyo alisema kuwa, jukwaa hilo la viongozi watakaopewa mafunzo wanaamini litachangia katika kutekeleza maendeleo ya elimu nchini.
Alisema, elimu ni ufunguo wa maisha, hivyo wanataka kuboresha elimu katika masomo ya hesabati, sayansi na kiengereza kwa kuweka mazingira bora ya ufundishaji, kutoa vifaa pamoja na kuwaongezea uwelewa walimu na wanafunzi.
“Tunawaomba mutoe mapendekezo hapa na tunaahidi tutayafanyia kazi kwa ajili ya kujenga kwani miaka kadhaa tumekuwa tukishirikiana na Serikali katika miradi mbali mbali ya kimaendeleo”, alisema Naibu huyo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari katika masomo ya hesabati, sayansi na kiengereza (Good Neighbors) Ilsun Jung aliishukuru Wizara ya elimu kwa kushirikiana pamoja katika kuleta maendeleo, ambapo wamekuwa wakifikia malengo ya mradi.
Akitaja baadhi ya malengo ya mradi huo, Mkurugenzi huyo alisema ni kuijengea uwezo mifumo ya Wizara ya elimu na vituo vya elimu, ili kuwajenga walimu kutoa huduma bora kwa wanafunzi sambamba na kuboresha jamii ikiwemo Kamati za skuli.
Mapema akizindua mafunzo hayo Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba, Ali Mohamed Mwinyi alilishukuru Shirika hilo kwa kuleta mradi huo na tayari wameona ushirikiano uliopo baina ya Korea na Tanzania.
Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuitendea haki taaluma hiyo na kuwa makini wakati wanapofundishwa ili kupata uelewa zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Ni nafasi nzuri kwetu kupata program hizi ambazo zimetufuata nchini kwetu, kwani ingetupasa kwenda sisi jambo ambalo ingekuwa vigumu kutokana na kutomudu gharama”, alisema Katibu huyo.
Nae Meneja mradi Layla Ghaid alisema, wataungana na Serikali katika kuboresha vitu vidogo vidogo, ambapo skuli zisizo na vifaa hata kidogo watazipa kipaombele.
Afisa Mwandamizi wa mradi huo John Massenza alifahamisha, wanataka kuboresha kiwango cha ufaulu kwa miaka mitatu ijayo, hivyo ni vyema kuyasema mapungufu yaliyopo ili Wizara zipate kuwasaidia.
Akiwasilisha mada Afisa Tathmini na Ufuatiliaji katika mradi huo, Fransis Forodha alitaja changamoto ambazo walizoziona baada ya kufanya utafiti kuwa ni, uhaba wa walimu wa sayansi, utoro na uelewa mdogo wa wanafunzi, madarasa kidogo pamoja na wanafunzi wengi kwenye darasa moja.
Mwalimu mkuu wa skuli ya Sekondari ya Sheikh Idrisa Albdulwakil Kizimbani Wete Sabah Mussa Said na Msaidizi kituo cha Ubobezi wa Masomo ya Sayansi Mussa Omar Khamis walisema, mafunzo hayo yatasaidia uelewa na ufaulu kwa wanafunzi, kwani walimu watafuatilia na kusomesha kwa ushindani.
Mkurugenzi Elimu ya Sekondari Zanzibar, Asya Iddi Issa aliwataka walimu wafanye kazi kwa pamoja, wasaidiane maarifa, maelekezo pamoja na kuwa makini kwenye usajili wananafunzi, ili kuepusha usumbufu wanaoupata.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa mashirikiano na Serikali, Good Neighbors, UNOPS na NIRAS chini ya ufadhili wa KOICA ambayo yamewashirikisha maafisa elimu, maafisa taaluma pamoja walimu wakuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba.