NA ZUHURA JUMA, PEMBA
ELIMU inahitajika zaidi katika jamii, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kudumisha amani hata ifikapo kipindi cha uchaguzi mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano, kwa lengo la kujiletea maendeleo katika nchi.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wananchi wa Tumbe Wilaya ya Micheweni walisema, kila inapofikia kipindi cha uchaguzi watu hufarikiana, hali ambayo inasababisha migogoro na uvunjifu wa amani ndani ya jamii.
Walisema kuwa, ni vyema kwa wanajamii kuzika tofauti zao wakati na baada ya kumalizika uchaguzi mkuu na waendelee kushirikiana katika mambo mbali mbali ya kijamii, ili kuleta maendeleo zaidi.
“Tunashukuru kwa sasa tunashirikiana vizuri katika kila jambo kwenye jamii yetu, lakini wakati wa uchaguzi hali huwa sio nzuri hata kidogo, tutaka na kipindi cha uchaguzi iwe kama sasa”, walisema wananchi hao.
Mwananchi Salma Khamis Tumu alisema kuwa, inapofikia kipindi cha uchaguzi hutokea migongano, kwani kila mmoja anatetea upande wake ili apate ushindi.
“Yale maneno wanayotupiana huwa sio mazuri, hivyo hutokea ugomvi baina yao na kusababisha uvunjifu wa amani kwani hufikia kupigana, kuvunjiana nyumba na kuchomeana moto”, alisema Salma.
Akihadithia yaliyomkuta katika uchaguzi wa mwaka 2020 ni kaka yake wa mama mmoja ambae aliiambia familia yake kwamba wamtenge na wasimpe kitu chochote kinachotoka nyumbani kwao, jambo ambalo lilimpa wakati mgumu.
Kwa upande wake Bishara Mohamed Mussa alieleza kuwa, ipo haja kwa jamii kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali, ili kuepusha matatizo yanayoweza kutokea.
“Tunapewa elimu na nasaha mbali mbali lakini tunamuweka bilisi mbele na hivyo kutuamrisha mabaya ambayo mwisho wake yanasababisha uvunjifu wa amani”, alisema.
“Inapotokezea migogoro wanaoathirika zaidi ni akaina mama na watoto, hivyo tujitahidi kuhakikisha maelekezo yanayotolewa tunayafuata na unapokatazwa sehemu basi usiende”, alieleza mama huyo.
Nae Maulid Salum Adeni alifahamisha kuwa, sababu ya kutokea kwa zogo ni kwamba kila mmoja anawania haki yake, hivyo jeshi la Polisi hufika kwa ajili ya kutuliza ikiwa sehemu kuna dalili ya uvunjifu wa amani.
“Haiwezekani mtu anaekwenda kutuliza ghasia na yeye umuandame, akitaka kukudhuru lazima ujihami, hivyo hapa ndo kunatokea yale mashambulio baina ya raia na waliokwenda kutuliza fujo”, alieleza.
Aliwaomba wale ambalo wanapewa jukumu la kusimamia masuala ya uchaguzi wawe waaminifu na kuhakikisha kila aliepata haki yake anapewa huku wakiwepo watu wa pande zote mbili wakishuhudia kama iliyoelekeza dini ya Kiislamu.
Adeni alifafanua kuwa, ikiwa kuna mmoja kati yao hakuridhika, iwepo fursa ya kutafuta haki yake kwa njia ya amani.
Kaimu sheha wa Shehia ya Tumbe Mashariki Omar Ali Omar aliwataka wananchi kujua kwamba kila mtu ana haki ya kuchagua kiongozi anaemtaka na chombo kinachotangaza matokeo kimewekwa kisheria.
“Uchaguzi ni jambo la mpito hivyo utakapomalizika maisha yanahitaji yaendelee kama kawaida, kwa hiyo tujiepushe na migogoro, pia Serikali iendelee kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, vipeperushi na hata ndani ya jamii”, alisema Kaimu huyo.
Kila ifikapo kipindi cha uchaguzi mkuu, ndani ya wanajamii hutokea migogoro ambayo husababisha mifarakano, hivyo ipo haja ya kujipanga mapema kutoa elimu kila mmoja aelewe madhara ya uvunjifu wa amani.