Friday, November 15

KATIBU MKUU akabidhi pikipiki ili kuongeza makusanyo ya kodi

 

 

NA ABDI SULEIMAN.

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Fatma Hamad Rajab, amewataka maafisa Utamaduni wa Wilaya ambao wamekabidhiwa Pikipiki, kuhakikisha vyombo hivyo wanavitumia katika kuongoza ukusanyaji wa mapato na sio vyenginevyo.

Alisema kabla ya kupatiwa usafiri huo, walikuwa wakijitahidi katika ukusanyaji wa mapato, hivyo sasa ni wakati wa kuonyesha uhumuhimu wake kwa kuongeza juhudi na mapato kuongezeka.

Katibu Mkuu huyo aliyaeleza hayo katika hafla ya kukabidhi Pikipiki nne, tatu kwa maafisa Wilaya wa baraza la sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni na Moja kwa afisa wa baraza la Kiswahili, hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara hiyo Gombani Chake Chake Pemba.

“Imani yangu ni kuona sasa kazi itafanyika vizuri, zaidi kipindi kinachofuata cha mfungo mosi maharusi mengi, hapa ndipo tutakapoona ule umuhimu wa vipando hivyo, muliokuwa mukiuhitaji na sio kushuka kwa mapato”,alisema.

Katika hatua nyengine Katibu mkuu Fatma, aliwataka maafisa hao kutambua kuwa pikipiki hizo ni mali ya serikali, pesa zilizotumika ni mali ya wananchi na wafanyakazi, hivyo wanapaswa kuzitunza na kuzithamini na sio kuzifanya bodaboda kwa kupakia abiria na mizigo jambo ambalo litakwenda kinyume na makabidhiano yake.

Hata hivyo alimuagiza Afisa Mdhamini Wizara hiyo Pemba, kutokusita kumchukulia hatua afisa yoyote atake shindwa kuithamini Pikipiki hiyo, sambamba na kwenda kinyume na malengo ya wizara katika suala la ukusanyaji wa mapato.

Naye Katibu mtendaji baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni Zanzibar Dkt.Omar Abdalla Adamu, alisema lengo la kukabidhi vipando hivyo ni kutatua changamoto ya usafiri kwa maafisa utamaduni Wilaya, ili waweze kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Makubaliano yetu ni kununua pikipiki tatu ila na wenzetu wa baraza la Kiswahili wamepata mmoja, sasa kazi iliyobakia Ofisi kuu kuwapatia gari na tayari tumeshaanza maandalizi yake”alisema.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau alisema watendaji waliokabidhiwa vipando hivyo wanakazi kubwa ya kuhakikisha malengo ya vyombo hivyo yanatimika katika ukusanyaji wa mapato.

Aidha aliwataka kuhakikisha vyombo hivyo wanavitunza na kuvithamini ili vidumu muda mrefu na sio kuviharibu na kuona ni mali ya serikali.

Akitoa neno la shukurani mratib wa BAKIZA Pemba Abdalla M.Ali, aliishukuru Wizara kwa kumalia kilio chao cha muda mrefu, huku akiahidi malengo ya ukusanyaji wa mapato yatatimia pamoja na kuzitaka idara nyengine kuiga mfano huo.

Jumla ya pikipiki nne zimekabidhiwa kwa maafisa utamaduni Wilaya na moja kwa baraza la Kiswahili Pemba, pikipiki hizo zimegharimu jumla ya shilingi Milioni 12.6.

MWISHO