Thursday, January 9

Kiungoni watakiwa kuachana na tabia ya kukumbatia muhali .

NA ABDI SULEIMAN

MKURUGENZI wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, amewataka wananchi wa kijiji cha Kimango Shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete, kuachana na tabia ya kukumbatia muhali pale yanapotokea matukio mbali mbali katika kijiji chao.

Alisema suala la muhali kwa jamii limekua ni jambo la kawaida kwa sasa, matukio mengi yanatokea na wanashindwa kuyaripoti katika vyombo vya sheria na mengine kuyatolea ushahidi unapohitajika.

Aidha mkurugenzi hanifa aliyataja baadhi ya matukio hayo ikiwemo Ubakaji, ulawiti, Wizi wa mazao, Wizi wa Wanyama, hali inayopelekea kuwahifadhi na kuwalinda wafanyaji wa matukio hayo.

Mkurugenzi huyo aliyaeleza katika mkutano wa kuhamasisha jamii juu ya masuala ya kisheria, ikiwa ni utoaji wa elimu ya msaada wa kisheria huko Kimango Shehia ya kiungoni.

“Lazima tusimame imara na tukubualiane kijijini kwetu kama tunaondosha neno muhali, hapo tutafanikiwa ikiwa kila mtu na lake basi hawa wanaofanya matukio tutaendelea kuwa nao”alisema.

Aidha aliwataka akinamama kuhakikisha wanakuwa mstari wambele, kutoa ushahidi pamoja na kuwafichuwa maovu yanayotendaka kijijini kwao, kwani waathirika wakubwa wa maovu hayo ni wanawake na watoto.

Naye mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Ali Juma, aliwaitaka jamii kuwasaidia watoto wadogo katika kuwalinda na vitendo vya udhalilishaji vinavyotokea katika jamii.

“Sisi tunajua hapa kiungoni zipo kesi nyingi zinakufa za ubakaji, munapaswa musimame kidete kutoa ushahidi hapa tutakuwa tumewatetea watoto wetu na sio kuoneana muhali”alisema.

Naye naibu mrajis wa Ardhi Asha Suleiman Said, aliwataka wananchi wa shehia ya kiungoni kwenda idara ya ardhi kuchukua hati miliki za ardhi zao kwa kulipia shilingi elfu 70000 tu.

Rashid Ali Hamad maakzi wa kijiji cha Kimango Shehia ya Kiungoni, alisema kesi zaidi ya 30 zinakwamwa kuwenda mbele tatizo ni rushwa muhali katika jamii na kusuluhishana kienyeji.

Aidha aliitaka sheria kuwangaliwa upaya kesi za udhalilishaji kutokuchumua muda mrefu, baada ya kufikishwa mahakamani kwa lengo la kutolewa hukumu ili ziondokane na kufutwa.

Naye Yussuf Khamis Ali alisema suala la muhali limekua tatizo sugu kijijini kwao, hususan katika wizi wa mazao, ubakaji, huku akiwataka wananchi wenzake kuachana na suala zima la muhali katika jamii yao.

Hata hivyo naye afisa sheria kutoka idara ya katiba na msaada wa kisheria Pemba Bakari, aliwataka wananchi kuachana na suala la muhali badala yake pia kuwafichuwa ili vyombo vya sheria kuwachukulia hatua za kisheria.