Friday, November 15

WAZIRI utekelezaji mradi wa Viungo unasaidia serikali kufikia lengo la kuinua vipato na uchumi

WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Shamata Shame Khamis amesema utekelezaji mradi wa VIUNGO, Mboga na Matunda Zanzibar unaisaidia serikali kufikia lengo lake la kuinua vipato na uchumi wa wananchi wake kwa kujiingiza katika shughuli za uzalishaji mazao ya kilimo kupitia taaluma na uwezeshwaji ambao wakulima wanapata kwenye mradi huo.
Waziri ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea mashamba ya wakulima wanufaika wa mradi huo kisiwani Pemba unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa lengo la kukagua maendeleo na mwelekeo wa mradi katika kuleta tija kwa wakulima.
Alisema dhamira ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara, ni kutambua wadau wote wanaoisaidia kufikia malengo yake kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ili kujua ufanisi na uhalisia kwenye kuwanufaisha wananchi walengwa.
Akizungumza na wakulima katika shehia ya Ole, Wilaya ya Chake chake, mkoa wa Kusini Pemba, Waziri Shamata alipongeza hatua ambazo mradi wa VIUNGO imezichukua kwa wakulima ili kuhakikisha lengo lake linafikiwa.
“Niwapongeze sana watekelezaji wa mradi huu wa Viungo Zanzibar kwa juhudi zenu za kuendelea kutoa mchango wenu kuisaidia serikali kuinua uchumi wa wananchi kupitia kilimo, huu ni mwelekeo mzuri kwenye sekta ya kilimo kupata miradi kama hii, na mimi nimekuja hapa na kaulimbiu yangu ya ‘toka kijiweni tukutane shambani’ kwasababu huku shambani ndipo kwenye maneno sio vijiweni,”  alisema Mhe. Shamata.
Katika kuhakikisha wakulima wanaondokana na  changamoto za kitaalam zinazowarejesha nyuma kiuzalishaji, Waziri huyo amemuagiza afisa mdhamini wizara hiyo kupeleka jopo la watafiti wa udongo kwa wakulima wa Nyanya shehia ya Mjini Ole ili kubaini chanzo cha mazao yao kushambuliwa na wadudu waharibifu.
 Alisema, “Afisa mdhamini nakuagiza leta hapa timu yako ya watafiti waje wapime udongo na tujue chanzo cha huu ugonjwa unaoathiri mazao haya ni kipi kwani yanarejesha sana nyuma juhudi za hawa wakulima, hatutaki nguvu zao ziendelee kupotea bure.”
Aidha katika hatua nyingine waziri huyo alisisitiza watekelezaji mradi huo kuandaa mpango maalum wa kushajihisha jamii juu ya umuhimu wa kutumia matunda kwa wingi ili kuwezesha matunda hayo kupata soko zaidi na kuongeza lishe za wananchi.
“Nakuombaeni watekelezaji wa mradi huu, tunafahamu wananchi wengi bado hawana utamaduni wa kutumia matunda, hivyo tuweke mkakati maalum wa kuhamasisha matumizi ya matunda hasa mapapai kwa wingi kwenye jamii ili kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa mazao yanayozalishwa na hawa wakulima wetu,” alisisitiza.
Malik Hamad Khamis,  Mkulima wa matunda mnufaika katika mradi huu kutoka Shehia ya Ole, Chake chake Pemba alisema uwepo wa mradi umemfungulia fursa ya kuwekeza katika kilimo hicho kutokana na taaluma ya uzalishaji bora wa mazao aliyopata kwenye mradi.
Alimweleza waziri, “mradi ulipokuja ulituhamasisha sana wakulima kujiingiza katika kilimo hiki kwa kutupatia mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia shamba darasa, tukapatiwa mbegu na mbolea za kuanzia. Baada ya hapo mimi mwenyewe niliamua kuuza ng’ombe wangu ili niwekeze zaidi kwenye kilimo hiki na nashukuru mpakasasa kwenye shamba langu kuna mipapai isiyopungua 300 na inaendelea vizuri.”
Mapema meneja uendeshaji wa mradi huo kanda ya Pemba Sharif Maalim Hamad alimueleza waziri kwamba mradi unatumia mbinu za kuwashirikisha wakulima viongozi kwenye shehia ili kufikisha haraka elimu kwa wakulima.
“Mradi umewafundisha wakulima viongozi 90 kwa Unguja na 90 Pemba kutoka kwenye shehia zote ambazo mradi unatekelezwa ili iwe rahisi kukutana moja kwa moja na makundi ya wakulima  kwenye shehia kutokana na kwamba huko ndipo wakulima wenyewe walipo.
Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea maeneo mbalimbali ya wakulima ambayo mradi wa VIUNGO unatekelezwa ikiwemo mashamba ya matunda, Viungo na Mboga katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba ambapo pia alipata fursa ya kushudia jinsi wakulima hao wanatumia taaluma ya kilimo chenye kuzingatia mabadiliko ya Tabianchi katika shughuli zao za uzalishaji.
Mradi wa VIUNGO, Mboga na Matunda Zanzibar ni wa miaka minne ambao unatekelezwa Unguja na Pemba kwa mashirikiano ya yaasisi za People’s Development Forums (PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar) kupitia mpango wa AGRI-CONNECT kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.