Thursday, January 9

Dk. Khalid ameuopongeza uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kufanya vizuri zoezi la uwekaji wa anuani za makaazi

Waziri wa Ujenzi, Mawasilaino na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed ameuopongeza uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kufanya vizuri katika zoezi la uwekaji wa anuani za makaazi linaloendelea katika Mkoa huo.

Waziri Dk. Khalid ametoa pongezi hizo wakati akiwa katika ziara maalum ya kukagua na kuangalia jinsi zoezi hilo linavyotekelezwa na watendaji waliopewa kazi hiyo katika Shehia ya Jumbi barabara ya Makontena Mkoa wa Kusini Unguja.

Ameeleza kuwa, Mkoa wa Kusini Unguja umepiga hatua nzuri katika zoezi la uwekaji wa Anuani za Makaazi (Post Code) katika Shehia na Mitaa ambapo hadi sasa Mkoa huo umefikia Asilimia Saabini na Sita (76%) na amewataka viongozi wa Mkoa wa Kusini kuiga mfano huo.

Aidha, Dk. Khalid amesema Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi itaendelea kufuatilia utekelezaji wa zoezi hilo katika Mikoa mengine kwa lengo la kuhakikisha zoezi linakamilika ndani ya wakati uliopangwa ili kutekeleza agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar ambapo zoezi hilo linatakiwa kukamilika ndani ya mwezi Mei mwaka huu.

“Zoezi hili linatakiwa likamilike ndani ya mwezi Mei, hivyo sote kwa pamoja tunapswa kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia lengo lililokusudiwa” Alisema Dk. Khalid

Akizungumzia juu ya fursa zikazopatikana mara baada ya kukamilikja kwa zoezi hilo Mhe. Dk. Khalid amesema kukamilika kwa zoezi hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha shughuli mbali mbali za kijamii ikiwemo kufungua fursa kwa wafanyabiashara.

Alifafanua kwamba, endapo zoezi hilo litakapokamilika na kuunganishwa na mifumo maalum itasaidia kuiweka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika ramani ya Dunia sambamba na kufungua milango kwa shughuli mbali mbali zitakazokuwa na maslahi kwa jamii.

“Kukamilika kwa zoezi hili kutaiweka Zanzibar katika ramani ya Dunia, pamoja na kufungua milango ya fursa mbali mbali jambo ambalo nchi nyingi ulimwenguni zimeanza kwa muda mrefu” Alifafanua Mhe. Waziri

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid amesema zoezi la uwekaji wa anuani za makaazi katika Mkoa huo linakwenda vizuri kutokana na mipango na mikakati imara waliojiwekea.

Mhe. Hadid amesema Mkoa wa Kusini unatarajia kulikamilisha zoezi hilo ndani ya kipindi cha wiki moja ambapo alitoa wito kwa wananchi wanaomiliki majengo kuviacha vitambulisho nyumbani ili kuwarahisishia watendaji wanaofanya kazi hiyo kufanya usajili bili ya usumbufu wowote.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Mkuu wa Mkoa huo amesema zoezi hilo lina faida nyingi litakapokamilika ambapo mwananchi hatopata usumbufu wa kuuliza uliza wakati anapotaka kwenda sehemu na baadala yake ataweza kutumia anuani hizo kumuelekeza sehemu anayohitaji kufika.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Jumbi Muhidini Haji Machano amesema wananchi wanaoishi katika shehia hiyo wamelipokea vizuri zoezi hilo ambapo ameshauri elimu zaidi itolewe ili kujenga uwewa kwa wananchi.

Akiwaelezea viongozi waliokuwa katika ziara hiyo juu ya harakati za usajili kupitia zoezi linaloendelea Afisa usajili Ndugu Fadhil Mohamed ameeleza kwamba katika kazi hiyo hakuna nyumba au eneo linaloachwa kuekewa anuani ya makaazi.

Kassim Abdi

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar.