Friday, February 28

Dk.Mwinyi azindua safari kuelekea uchumi wa buluu Pemba na kuwakabidhi futari wasio na uwezo

 

HANIFA SALIM, PEMBA.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk, Hussein Ali Mwinyi amesema, sasa sio wakati tena wa wananchi wanaofanya shuhuli za uvuvi kulalamikia ukosefu wa vifaa na mitaji kwani Serikali ikishirikiana na wadau mbali mbali imeanza kutekeleza azma ya kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutowa vifaa.

Hayo imedhihirika baada ya kukabidhi boti 4 kwa wavuvi wa Makangale na Kengeja na mashine 16 kwa wavuvi wa shumba mjini iliokwenda sambamba kukabidhi hundi ya Shilingi Million 192 kwa ushirika wa wavuvi Tumbe, katika hafla iliofanyika bandarini Shumba Wilaya ya Micheweni Pemba.

Alisema, pamoja na vifaa hivyo lakini tayari ziko Bank mbali mbali na mashirika mengine kama ZAFICO wameshatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitaji ambayo itatolewa kwa wavuvu ili kufikia safari ambayo inalengo la kuwabadilisha kimaisha.

Alitolea mfano wa mabenk hayo ikiwa ni pamoja Amana benk kutenga fedha Billion 10, Wizara ya Uchumi wa buluu 36 Billion, CRDB imetenga shilingi Billion 31 na ZAFICO wenyewe shilingi 7.6 Billion.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na wahisani mbali mbali yakiwemo Mabenk ili kuwajengea mbinu za maendeleo wananchi ikiwemo kuwapatia nyenzo mbali mbali za kujikwamuwa na umaskini,”alisema.

Dk, Mwinyi alieleza kuwa zoezi hilo la utowaji wa boti na vifaa vyake ni miongoni mwa kufikia safari ya ajira laki tatu (300,000) zilizotangazwa na Serikali ambazo miongoni mwake zitatoka katika sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi.

Aliyaagiza mabenk ambayo ameshatenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kufanya hivyo ili kuwasaidia wananchi wengine ambao bado hawajapatiwa vifaa vya uvuvi ili kuungana na wenzao katika safari hiyo ya kutumia rasilimali zitokanazo na  bahari ili kufaidika na sera ya uchumi wa Buluu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi alizishukuru Benk na wahisani mbali mbali wanaoiunga mkono Serikali katika harakati zake za kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha aliwataka wananchi waliopatiwa vifaa hivyo kuvitumia kwa malengo yaliokusudiwa na sio kwa shuhuli nyengine zisizokuwa na makusudio wa vifaa hivyo kwani Serikali anayoiongoza itahakikisha inatekeleza ahadi zake ilizozitowa kwa wananchi kwa muda mfupi ujao.

Alisema, tayari serikali imeweza kushirikiana na wahisani mbali mbali ikiwemo Mabenk katika kuwaletea maendeleo wananchi ikiwemo vifaa vya uvuvi ili kufikia uchumi wa buluu sambamba na kutowa mitaji kwa wafanyabiashara.

“Serikali imeazimia kuwapatia vifaa vya uvuvi wananchi wanaojishuhulisha na matumizi ya sera ya uchumi wa buluu ili waweze kufanyakazi zao kwa uhakika zaidi,”alisema.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepanga kuwawezesha wananchi katika shuhuli mbali mbali za kiuchumi ili kuweza kuwabadilisha kimaisha yao, kwa kuzingatia inatekeleza kauli yake ya kuwapatia ajira laki tatu (300,000) ambazo miongoni mwake zitatokana na shuhuli za uvuvi.

Alisema safari ya kufikia uchumi wa buluu Zanzibar imeanza rasmi ambapo utekelezaji wake kwa wavuvi na wajasiriamali unaanza kwa kuwapatia nyenzo zitakazoweza kufikia malengo yao kwa kuzitumia rasilimali zilizomo baharini.

Wakati huo huo Dk, Mwinyi aliiagiza Mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha kijiji cha Shumba ya mjini kinapata huduma ya maji safi na salama haraka iwezekanavyo na kipindi atakacho fika kijiji hapo hataki kusikia kero hiyo.

Aidha aliitaka Wizara ya Fedha kuwalipa fidia wananchi ambao wametowa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha miundo mbinu ya aina mbali mbali ili kuondowa malalamiko yanayoendelea kutokana na kutolipwa fidia zao.

Akitowa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa buluu Zanzibar, Dk, Aboud Suleiman Jumbe alisema, wizara imejipanga katika utekelezaji wa azma ya Rais  ya uchumi wa buluu, dira ya maendeleo na mpango wa maendeleo.

Alisema, utekelezaji wa mpango wa uwezeshaji wa uchumi wa buluu Zanzibar ni ishara kubwa inayowapa matumaini ya utekelezaji wa sera uchumi wa buluu chini ya uwongozi wa Rais wa Zanzibar Dk, Hussein Ali Mwinyi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, kukabidhiwa boti hizo kwa wavuvi hao ni muarubaini wa kuondowa changamoto waliokuwa nayo   hivyo aliwataka wavuvi hao, kuzitumia boti hizo katika uvuvi wa bahari kuu kama ilivyoelekezwa.

“Kwa ambao wataendelea na shughuli za uvuvi tutawaunga mkono lakini nasisitiza boti hizi zitumike kwa uvuvi na sivyenginevyo, boti hizi zisitumike kwa magendo ambae atakwenda kinyume hatua za kisheria zitachukuliwa”, alisema.

Nae Mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni ya uvuvi Zanzibar ZAFICO Dk, Ameir Khaidar Mshenga alisema, ZAFICO imejipanga kuwafikia wajasiriamali wanaojishughulisha na uvuvi wa samaki na dagaa kwa Kisiwa cha Unguja na Pemba ambapo lengo ni kuwasaidia kukuza uchumi wao binafsi na kuongeza pato la taifa.

Alieleza, juu ya mradi huo wa kuwasaidia wajasiriamali zana za kisasa ZAFICO kwa kushiririkiana na Amana bank imejipanga kutoa mashine za boti kwa wavuvi 650 na kuwapatia boti na mitego wavuvi 887 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

Hata hivyo kwa upande wa  wananchi wa Shumba ya mjini Mkoa wa Kaskazini Pemba walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kwa imani yake alionayo kwa wananchi wa Shumba kwa kutekeleza ahadi zake kwa wakati sahihi.

                                     MWISHO.