NA ABDI SULEIMAN.
KUTOKUVUMILIA kwa Jamii pale inapotokea mifarakano miongoni mwano husababisha kuvunjika kwa amani na athari katika familia zao.
Kauli hiyo imetolewa na viongozi wa dini mbali mbali Kisiwani Pemba, huko katika chuo cha Benjamini Mkapa Mchangamdogo Wilaya Wete, katika mjadala wa vijana juu ya utunzaji wa amani uliowashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu na kuandaliwa na Taasisi ya ZANZIC.
Walisema jamii inapaswa kuondosha tafauti zao kwa kuvumiliana, ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kuepukika na kuondoka kabisha katika jamii.
Mwalimu Fadhili Juma Mohamed mjumbe kutoka ZANZIC, alisema watu wanaoishi katika jamii moja hakika inafika wakati mambo yanatafautiana, neno kuvumiliana linaweza kupelekea watu wakaishi kwa umoja.
Alisema kama hakutakua na neno kuvumiliana basi jambo hilo linaweza kupelekea uvunjifu wa amani, jambo ambalo ni hatari kwa jamii ya wazanzibari.
“Miongoni mwa mambo yanayokwaza amani ni neno kuvumiliana, kama hakutakua kuvumiliana jambo hilo linaweza kupelekea uvunjifu wa amani kwenye jamii,”alisema.
Naye katibu wa umoja wa viongozi wa dini mbali mbali upande wa Pemba, Mchungaji Benjamini Kissanga alisema jambo la amani linagusa kila mtu, na amani ikikosekana mifarakano inashika nafasi.
“akinukuu kitabu cha dini ya wakristo, kupitia kitabu cha waimbaria sura ya 12 mstari wa 14 unasema “tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, huu utakatifu ambao hapana mtu atakekuona bwana asipokua nawe”, amani inazungumzwa katika maandiko yote,”alisema.
Alisema nchi ikikosa amani, inapelekea kuwa na mgawanyiko na mfarakano pia yanaweza kupelekea maafa, viongozi wa dini wanaendelea anashirikiana na serikali kuitangaza amani kwa kila mtu.
Aidha aliwataka wanafunzi kuendelea kuziyunga mkono Serikali, pamoja na kuelimishwa kwa kina wanajamii mbali mbali juu ya umuhimu wa amani.
Nao baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu Pemba, wamesema amani inapokosekana hata utulivu unakuwa haupo na hakuna hata moja linaloweza kufanyika.
Walisema ili amani iendelea kuwepo ni vyema kwa vijana kujielewa, kufuata sheria na taratibu za nchi, sambamba na kusuluhisha migogoro pale inapotokea.
Walisema vijana wanapaswa kujielewa kama wao ndio nguvu kazi ya taifa, pia wanapaswa kupendana katika jamii ili amani iweze kuwepo.
Jumla ya mada mbili zilijadiliwa katika mjadala huo, ikiwemo utunzaji wa amani na umuhimu wake, pamoja na haki za kiuchumi na fursa za kiuchumi katika uchumi wa buluu.
MWISHO