Monday, January 6

TAQWA yazipatia futari familia 502 zinazolea watoto mayatima Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

TAASISI ya TAQWA Orphans Trust Tanzania imekabidhi msaada wa Futari kwa familia 502, zinazolea watoto mayatima zaidi ya 800   Kisiwani Pemba.

Familia hizo ambazo zipo chini ya Jumuiya ya Tahfidhi Qurani na Maendeleo ya Kiislamu ya Ole, ambao ndio wasimamizi wakubwa wa familia zinazolea watoto hao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya Familia ambazo zimekabidhiwa Futari hiyo, wameishukuru taasisi ya Taqwa kwa kutoa msaada huo, katika kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Bimkubwa Husein Hassan aliitaka taasisi hiyo, kutokuwa mwanzo wa kutoa msaada huo, bali iwe ni jambo la kawaida kila mwaka kuwasaidia mayatima.

Alisema mayatima bado wanahitaji misaada kwa hali na mali, ili kuweza kujiona wako sawa na watoto wengine, zaidi kipindi cha Ramadhani hali zao zinakuwa ni ngumu zaidi.

“Hakuna mtoto aliyetaka au kutamani kuondokewa na mazazi wake, bali hiyo ni mipango ya mungu imeshaandikwa, Taqwa ni watu wa mfano katika hili,”alisema.

Naye mlezi wa Mtoto yatima Suwedi Makame mkaazi wa Ole, aliwataka wafadhili wengine kujitokeza kusaidia mayatima kama inavyofanya taasisi ya Taqwa katika kusaidia mayatima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya TAQWA Orphans Trust Tanzania Mhandisi Dr.Salha Mohamed Kassim, alisema kuna umuhimu mkubwa sana wa kushuhulikia watoto mayatima, ni jambo zuri kwa wanafamilia kuwalea wenyewe mayatima na sio kuwapeleka katika nyumba za malezi.

Alisema unapolea mtoto yatima kuna faida nyingi huzipata kwa mlezi, huku akitolea Mfano mtume Muhammad (S.A.W) alilelewa na ami yake na sio kupelekwa sehemu nyengine, hivyo tunapaswa kuiga mfano huo katika kuwalea watoto.

Alisema mtoto anahitaji kusogezwa karibu katika jamaa zake, huku akiwapongeza wanafamilia wanaolea watoto hao sambamba na kutokukata tamaa katika malezi hayo.

Alifahamisha kuwa Taqwa katika mwaka huu imedhamiria kuwapatia futari kaya 2000, ni watoto wengi zaidi katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.

Afisa anayeshuhulikia masuala ya watoto kutoka Taqwa Hajar Bakari Ramadhani, aliwataka wadau wengine kuunga mkono juhudi zinazotolewa na taasisi hiyo,  katika kuhakikisha Taqwa inazifikia familia nyingi zaidi.

Katibu wa jumuiya ya Tahfidhi Quran na Maendeleo ya Kiislamu Ole, Shekhe Sultan Nassor Hamad, aliishukuru Taqwa kwa msaada huo, na kuendelea kusaidia familia zinazolea watoto mayatima.

Alisema kwa mwaka huu Jumiya imepanga kuzipatia futari kaya 502 zinazolewa watoto zaidi ya 800, huku akiwataka wananchi baada ya kufa kwa mwanafamilia kuhakikisha wanawaandikisha mayatima mapema tu.

MWISHO